Mar 09, 2016 07:44 UTC
  • Jumanne 8 Machi 2016

Leo ni Jumanne tarehe 28 Mfunguo nane Jamadil Awwal 1437 Hijria sawa na Machi 8, 2016 Milaadia.

Miaka 118 iliyopita na katika sikukama ya leo, Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mamar'ja' mashuhuri wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa Shiraz kusini mwa Iran na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini ambapo alisomo kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama vile Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu mjini hapo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatua yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Fatuwa hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Machi 1985, ulitokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa garini mjini Beirut, Lebanon ambapo watu wasiopungua 45 waliuawa na wengine 175 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti unaotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mlipuko huo ulifuatilia mlipuko mwengine mkubwa zaidi uliotokea mwaka 1983, ambapo watu wasiopungua 61 waliuawa kusini mwa bandari ya Tyre, nchini Lebanon.

Na siku kama hii ya leo mwaka 4 uliopita alifariki dunia Dakta Iraj Afshar mtaalamu wa masuala ya Iran na mwandishi wa Kiirani. Dakta Afshar alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsiya huko Yazd katikati mwa Iran. Iraj Afshar alisomea fani ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran na kuwasilisha tasnifu yake ya duru ya udaktari chini ya anwani ya "Jamii ya waliowachache nchini Iran". Mwaka 1331 Hijria Shamsiya Dakta Afshar alianzisha jarida alililolipa jina la "Utamaduni wa Iran". Mbali na kufundisha, msomi huyo wa Kiirani alifanya utafiti wa thamani kuhusu masuala ya Iran na kuhusu masuala ya uandishi ambapo utafiti wake huo ulichapishwa katika majarida yenye itibari ya nchini Iran na nje ya nchi.