Jumatano, Machi 9, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 29 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1437 Hijria sawa na tarehe 9 Machi 2016 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, aliuawa Sayyid Jamaluddin Asadabadi mwanazuoni na mmoja wa viongozi wa mapambano dhidi ya ukoloni wa kimaitaifa dhidi ya Waislamu. Sayyid Jamaluddin alizaliwa huko Asadabad magharibi mwa Iran na kupata elimu katika fani za falsafa, nujumu na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki, Sayyid Jamaluddin Asadabad alikuwa mtaalamu pia katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi.
Tarehe 9 Machi mwaka 1992, Menachem Begin mmoja kati ya waasisi wa utawala haramu wa Israel na chama cha mrengo wa kulia cha Likud aliangamia. Begin alizaliwa nchini Russia mwaka 1913 na baba yake ambaye alikuwa Mzayuni mwenye misimamo mikali alikuwa na taathira na nafasi kubwa katika malezi yake. Akiwa na umri wa miaka 12, Begin aliasisi kikosi cha vijana wa Kizayuni na miaka miwili baada ya kuhamia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, sawa na mwaka 1942 akateuliwa kuwa kamanda wa taasisi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu ada kwa jina la "Irgun." Taasisi hiyo ilikuwa moja kati ya makundi makuu ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya Kizayuni iliyokuwa ikitekeleza mauaji dhidi ya raia wa Palestina na kuwafukuza katika ardhi zao. Alikuwa katili sana dhidi ya raia wa Palestina kiasi kwamba David Ben Gorion ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa utawala haramu wa Israel alisema kuwa Begin ndiye Hitler wa kweli.
Miaka 163 iliyopita siku sawa na hii ya leo, alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko Kaskazini Magharibi mwa Iran alimu na mjuzi wa lugha wa Kiirani Ayatullah Sheikh Muhammad Qasim Ardubadi. Baada ya kumaliza masomo yake ya kati alisafiri hadi Najaf ambapo alisoma kwa maulama mashuhuri wa mji huo. Msomi huyo mkubwa baada ya kufikia daraja ya ijtihadi alirejea mjini alikozaliwa na kuanza kufundisha huko. Ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwake ni kitabu kiitwacho "Al Shihabul Mubin fii I'jaazil Qur'an." Alifariki dunia mwaka 1333 Hijria.
Na miaka 158 iliyopita mwafaka na leo alifariki dunia mmoja wa wataalamu na malenga wa lugha ya Kiarabu Abdul Baqi bin Sulaiman Farooqi. Alikuwa na kipawa cha kusoma mashairi ya kuvutia tangu yu kijana. Aidha Abdul Baqi alikuwa mmoja wa wapenzi wa kizazi cha Mtukufu Mtume Muhammad (saw) ambapo aliyadhihirisha mapenzi yake hayo katika mashairi yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Al Baqiyatus Swalihat."