Mar 10, 2016 04:03 UTC
  • Alkhamisi, Machi 10, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 30 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1437 Hijria sawa na tarehe 10 Machi 2016 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita mvumbuzi wa Kimarekani, Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake, Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano.

Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka. Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell.

Na siku kama ya leo miaka 71 iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo. Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo Japan haikusalimu amri hadi Mwezi Agosti mwaka huo huo wa 1945 wakati Marekani iliposhambulia kwa mabomu ya nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki na kuua maelfu ya raia wasio na hatia.

Miaka 25 iliyopita mwaka 1368 Hijiria Shamsia, Dakta Abdul Hamid Irfani, mshairi wa Pakistan alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa mwingi wa kuhuisha tamaduni za Kiislamu na kupambana na tamaduni za Wamagharibi. Pia alikuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa na wanafunzi maarufu wa wanafalsafa na mshairi maarufu wa Lahore, Pakistan, Muhammad Iqbal. Dakta Irfani ameandika vitabu 40 katika taaluma mbalimbali, vitabu ambavyo baadhi vimepata kuchapwa nchini Iran.