May 22, 2017 07:13 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Mei 22

Ufuatao ni mkusayiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita.....

Iran yazoa medali kochokocho Michezo ya Mshikamano wa Uislamu

Wanamichezo wa Iran wamezoa medali kochokocho katika duru ya 4 ya mashindano ya Michezo ya Mshikamano wa Uislamu inayofanyika Azerbaijan. Hadi kufiki sasa wanamichezo wa Iran wamezoa jumla ya medali 82 zikiwemo dhahabu 24. Mwenyeji Azerbaijan inaongoza kwa wingi wa medali, ambapo hadi sasa imekusanya medali 134, zikwemo dhahabu zaidi ya 63, ikifuatiwa na Uturuki yenye medali 172, zikiwemo dhabau 65Nafasi ya nne hadi ya 10 zinashikiliwa na Uzbekistan, Bahrain, Algeria, Indonesia, Misri, Morocco na Kyrgyzstan kwa usanjari huo. Wanariadha na wanamichezo kutoka nchi 54 za Kiislamu kutoka kila pembe ya dunia wanashiriki mashindano hayo yaliyoanza Mei 12 na yanatazamiwa kumalizika Mei 22, chini ya kaulimbiu "Mshikamano Wetu, Umoja wa Wetu". Mbali na riadha, michezo nyingine inayotifua kivumbi nchini Azerbaijan ni pamoja na ndondi, mpira wa mikono, voliboli, tenisi, karate, taekwondo na kunyanyua vitu vizito.

Vijana wa Iran waanza vizuri Kombe la Dunia Korea

Timu ya taifa ya vijana wa Iran imeanza vyema kampeni zake za kuibuka kidedea katika mashindano ya soka ya Kombe la Dunia ya mabarobaro wenye chini ya miaka 20 huku Jamhuri ya Korea mwaka huu 2017.

Hii ni baada ya kuibanjuka Costa Rica bao 1-0 katika mchuano wake wa ufunguzi wa Kundi C. Bao la pekee la kiungo Mohammad Mehdi Mehdikhani lilitosha kuipa Iran ya Kiislamu pointi 3 muhimu. Mabarobaro hao wa Kiirani wanatazamiwa kuvaana na vijana wa Kiafrika wa timu ya Zambia siku ya Jumatano. Zambia pia wameanza mashindano hayo kwa mguu wa kulia chambilecho wanaspoti, kwa kuizaba Ureno mabao 2-1 katika kitimutimu kingine cha Kundi C. Korea Kusini ni mwenyeji wa mashindano haya yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA, kuanzia Mei 20 hadi Juni 11.

********************************

Serengeti ya TZ yaaga Kombe la Dunia U-17

Mwakilishi wa Afrika Mashariki, timu ya Serengeti Boys ya Tanzania imetolewa katika michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana wenye chini ya umri wa miaka 17, baada ya kufungwa bao 1-0 na Niger katika mchezo wa mwisho wa Kundi B Uwanja wa Port Gentil mjini Gentil, Gabon Jumapili. Matokeo hayo yanazifanya Niger na Tanzania zifungane pointi na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo mshindi katika mechi baina yao anafuzu Kombe la Dunia Oktoba mwaka huu India na pia kwenda Nusu Fainali ya michuano hiyo. Niger anaungana na Mali iliyoongoza kundi kwa pointi zake saba, baada ya ushindi wa mechi mbili na sare moja, wakati Tanzania na Angola zote zinatolewa.

Gabon, mwenyeji wa mashindano haya ya kienyeji

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Daniel Laryea wa Ghana, aliyesaidiwa na Seydou Tiama wa Burkina Faso na Attia Amsaad wa Libya, Niger walipata bao lao kipindi cha kwanza, mfungaji Ibrahim Boubacar Marou dakika ya 41 baada ya shambulizi zuri lililowachanganya walinzi wa Serengeti Boys. Lakini Niger wangetoka uwanjani wanaongoza kwa mabao zaidi baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kama si umahiri wa kipa Ramadhan Awam Kabwili kuokoa michomo zaidi ya mitatu ya wazi. Kwa ujumla, Serengeti Boys ilizidiwa mchezo kipindi cha kwanza na kipindi cha pili hali iliendelea kuwa hivyo na hatimaye Niger wakaitoa Tanzania. Wachezaji wa Tanzania walikuwa wenye huzuni baada ya mchezo huku wakilia. Mbali na Mali na Niger, timu nyingine zilizofuzu Nusu Fainali ni Ghana na Guinea kutoka Kundi A.

Yanga yatwaa ubingwa wa Ligi ya Soka Tanzani Bara

Licha ya kutandikwa bao 1-0 na Mbao FC, klabu ya Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu soka Tanzania bara msimu wa 2016/2017. Yanga ambao walikuwa wanatetea Ubingwa wao walikuwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jiji Mwanza kucheza dhidi ya Mbao FC. Mchezo wa Yanga dhidi ya Mbao FC licha ya kuwa Yanga alikuwa tayari ana asilimia 99 ya kutwaa taji hilo kutokana na kuwa na magoli mengi zaidi ya Simba aliyekuwa anamfuatia ilimalizika kwa Yanga kupoteza kwa goli 1-0 lakini ametangazwa Bingwa kwa kuizidi Simba magoli 10 licha ya wote kuwa na point 68. Bao hilo la Mbao lilitiwa kimyani na katika dakika ya 22 likifungwa na Habib Haji kwa shuti kali lililomzidi mlinda mlango wa Yanga Beno Kakolanya na kujaa wavuni. 

Yanga Hoyee licha ya kuchachawizwa bao 1-0

Ubingwa wa Ligi Kuu wa Yanga unakuwa ni Ubingwa wao wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu lakini ni Ubingwa wao wa 27 wa Ligi Kuu kwa muda wote, wakati watani zao Simba wao wanakuwa hawajawahi kutwaa taji hilo kwa misimu minne mfululizo, timu za African LyonToto na JKT Ruvu zimeshuka daraja na nafasi zao zitazibwa na Singida UnitedNjombe na Lipuli FC zikipanda. Ushindi huo umeifanya Mbao kukwepa kushuka daraja, na sasa inabaki Ligi Kuu huku timu nyingine kutoka mkoani Mwanza, Toto Africans na African Lyon ya Dar es Salaam zikiungana na JKT Ruvu ya Pwani kushuka daraja. Kwa upande wa wafungaji bora wachezaji Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting na Simon Msuva wa Yanga wamefungana wote wakiwa na mabao 14, hivyo inabidi iangaliwe aina ya mabao aliyofunga kila mchezaji ndipo iamuliwe mshindi.

***********************

Dondoo za Hapa na Pale

Pazia la Ligi Kuu ya Uingereza limefunga rasmi siku ya Jumapili, baada ya kila timu kukamilisha mchezo 38, huku matumaini ya Arsenal kucheza Ligi ya Mabingwa yakizimwa. Nayo, Chelsea imekamilisha mechi yake ya mwisho kwa ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Sunderland, kisha kukabidhiwa kombe la ubingwa msimu huu. Kiu ya Kocha Arsene Wenger ilikuwa ni kumaliza katika nafasi nne za juu. Hata hivyo juhudi za kocha huyo zimegonga mwamba baada ya klabu hiyo kumaliza katika msimamo wa ligi ikiwa nafasi ya tano, licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wapinzani wao Everton. Arsenal imeelekeza matumaini yake kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA utakaopigwa Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Wembley. Timu nne zilizomaliza katika nafasi nne za juu ni Liverpool (4), Manchester City (3), Tottenham Hotspur (2) huku Chelsea wakiibuka mabingwa katika msimu wa 2016/17. Vigogo Liverpool nao waliiadhibu Middlesbrough 3-0, Huku Manchester City ikiifunga Watford mabao 5-0 pamoja na Manchester United ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crystal Palace. Timu zilizoshuka daraja msimu huu; Hull City, Middlesbrough na Sunderland.

Chelsea walivyoshinda EPL msimu wa 2014/15

Jambo la kukumbukwa katika msimu huu ni namba sita ambayo imekuwa kama jinamizi kwa Manchester United katika msimu wote, huku ikimaliza msimu huu kwa kushinda nafasi hiyo. Arsenal imeshindwa kufuzu kwa kombe la klabu bingwa barani ulaya, Champions League kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20 licha ya ushindi wake dhidi ya Everton wa mabao 3-1 katika siku ya mwisho ya mechi za Primia League. Arsenal ilianza mechi vizuri ikiwa pointi moja nyuma ya Liverpool na walikuwa katika nafasi bora kuchukua nafasi yao wakati waliongoza mnamo dakika ya nane. Lakini ukakamavu wa Liverpool uliiwezesha kusalia katika timu nne za kwanza baada ya kuwatandika Middlebrogh mabao 3-0. Manchester City ilishika nafasi ya tatu baada ya kuinyuka Watfoird mabao 5-0. Hii ni katika hali ambayo, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema hatima yake katika klabu hiyo itaamuliwa katika mkutano wa bodi ya klabu hiyo baada ya fainali ya Kombe la FA mnamo 27 Mei. Mfaransa huyo wa miaka 67 amekuwa na Gunners tangu 1996 na mkataba wake wa sasa unafikia kikomo mwisho wa msimu huu.

La Liga: Real Madrid Hoyee

Klabu Real Madrid imetwaa taji la ubingwa wa La Liga baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Malaga na kumaliza ukame wa miaka mitano bila kutwaa kombe hilo. Madrid ilikua ikihitaji alama moja kabla ya mchezo huo walianza kupata bao la kuongoza katika dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa Cristiano Ronaldo, kisha Karim Benzema akifunga bao la pili katika dakika ya 55.

Vijana wa Madrid wakishangilia goli

Madrid wamemaliza msimu wakiwa na alama 93 kwa michezo 38 wakifuatiwa na mahasimu wao Barcelona waliomaliza na alama 90 baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Eibar. Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi amekuwa mfungaji bora wa ligi hiyo akimaliza na mabao 37, akifuatiwa na Luis Suarez, mwenye mabao 29, Cristiano Ronaldo akiwa katika nafasi ya tatu kwa magoli 25.

…………………….TAMATI……………….