Jun 06, 2017 02:59 UTC
  • Jumanne, Juni 6, 2017

Leo ni Jumanne mwezi 11 Ramadhani, 1438 Hijria mwafaka na tarehe 6 Juni 2017 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, yaani tarehe 16 Khordad mwaka 1368 Hijria Shamsia, mwili mtoharifu wa Imam Khomeini (MA) ulizikwa hapa mjini Tehran katika maziko yaliyohudhuriwa na wimbi la mamilioni ya watu waliokuwa na majonzi makubwa. Zaidi ya waomboleza milioni kumi kutoka miji mbalimbali ya Iran na nje ya Iran walishiriki katika maziko hayo ambayo hayajawahi kutokea mfano wake. Moja ya sifa za kipekee za maziko hayo ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ambaye alitumia umri wake wote kwa ajili ya ukombozi na kuwaletea heshima wanadamu, ni wimbi kubwa mno la mamilioni ya watu walioshiriki kwenye maziko hayo. Maziko hayo yalikuwa ni medani adhimu ya kuonesha imani na mapenzi ya wananchi wa Iran na wa maeneo mengine mengi duniani kwa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) na kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran. Hivi sasa haram ya mwanachuoni huyo mkubwa iko pembeni mwa maziara matoharifu ya maelfu ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kusini mwa Tehran. Wapenzi wa mwanachuoni huyo kutoka kona zote za dunia hufanya ziara kwenye haram yake na kumuombea dua za kupandishwa daraja kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Haram ya Imam Khomeini (MA) kusini mwa Tehran

 

Siku kama ya leo miaka 585 iliyopita yaani mwezi 11 Ramadhani mwaka 853 Hijria, alifariki dunia mjini Cairo Misri, Ibrahim Karaki, mwanahistoria, jimbi wa sarufi na mpokezi wa hadithi wa Kiislamu. Baada ya kujifunza Quráni Tukufu na elimu za awali za kidini, alielekea kwenye vituo mbalimbali vya kielimu na kidini kwa ajili ya kujielimisha zaidi. Alikuwa na malaka na ustadi mkubwa katika fani kama za fikihi na isimu ya lugha  na ameacha vitabu vingi kama vile Iírab al Mufasswal kinachohusiana na Ulumil Qurán.

Ibrahim Karki

 

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 6 Juni 1966 Milaadia, merikebu ya kwanza isiyo na rubani ilitua juu ya mwezi. Baada ya kupamba moto ushindani wa teknolojia ya anga za mbali baina ya Marekani na Umoja wa Kisovieti hasa katika suala la kuizunguka dunia, mwaka 1966 Milaadia, kilianza kipindi kipya cha ushindani baina ya nchi hizo mbili. Awali, tarehe 4 Aprili 1966, merikebu ya Umoja wa Kisovieti iliuzunguka mwezi kwa mara ya kwanza na kutuma picha zake ardhini kutoka masafa hayo ya mbali. Jambo hilo liliongeza ushindani baina ya madola mawili makubwa wakati huo, na tarehe 6 Juni mwaka huo huo, merikebu ya kwanza ya Marekani isiyo na rubani ilitua juu ya mwezi na kutuma taarifa ardhini kutoka juu ya mwezi. Kasi ya teknolojia hiyo iliongezeka sana baada ya hapo na ilipofika tarehe 21 Julai 1969, raia mmoja wa Marekani akaweka mguu wake kwa mara ya kwanza juu ya mwezi.

Mtu wa kwanza kuweka mguu wake juu ya mwezi

 

Na miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 6 Juni 1901 Milaadia, alizaliwa Ahmad Sukarno, baba wa ukombozi wa Indonesia na rais wa kwanza wa nchi hiyo kubwa ya Kiislamu ya kusini mashariki mwa Asia. Baada ya kumaliza masomo yake ya upili aliendelea na masomo yake katika masuala ya uhandisi hasa fani ya usanifu majengo hadi alipofikia daraja ya uzamivu katika fani hiyo. Ahmad Sukarno alijihusisha na masuala ya siasa tangu akiwa mwanafuzi. Mwaka 1926, aliviandaa vyama vya wenyeji wa Indonesia kuanzisha vita na wakoloni wa Uholanzi. Wakoloni ambao hawakupenda kabisa kusikia neno uhuru, walimtia mbaroni mara kadhaa Ahmad Sukarno na mwaka 1940 wakamfukuza katika kisiwa cha Java na kumbaidishia kisiwani Sumatra. AAhmad Sukarno alitoa mchango mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya Wajapani katika Vita vya Pili vya Dunia. Wakati Indonesia ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uholanzi mwaka 1945, Ahmad Sukarno alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Ahmad Sukarno, Rais Tito wa Yugoslavia na Rais Abdel Nassir wa Misri ndio waasisi wakuu wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, NAM.

Ahmad Sukarno

 

Tags