Mar 14, 2016 05:38 UTC
  • Jumatatu, Mchi 14,  2016

Leo ni Jumatatu tarehe 4 Mfunguo Tisa Jumadi Thani 1437 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 14 Machi mwaka 2016 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita uchaguzi wa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la kwanza la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika hapa nchini na hivyo kutimiza moja ya malengo ya mapinduzi hayo. Kwa sasa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina wawakilishi 290 ambao huhudumu bungeni kwa kipindi cha miaka 4. Wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran kama Wakristo na Wayahudi pia kwa uchache huwa na mwakilishi mmoja katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.

Bunge la Iran hutunga sheria zinazohusiana na masuala ya umma kwa sharti kwamba zisipingane na sharia za Kiislamu. Kazi nyingine muhimu ya Bunge hilo ni kuwasaili, kuwapasisha au kuwauzulu mawaziri wa serikali.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita yaani tarehe 14 Machi 1978, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianza kuivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na operesheni iliyofanywa na wanamapambano wa Kipalestina pambizoni mwa Tel Aviv. Katika mashambulio hayo jeshi la Israel liliua raia wengi wasio na hatia wa Lebanon na Palestina na kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Lebanon. Hata hivyo utawala huo ghasibu uliondoka kwa fedheha katika maeneo ya kusini mwa Lebanon mwaka 2000 baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano shupavu wa Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah na kuondoka kwenye eneo hilo.***

Tarehe 4 Jumadi Thani miaka 62 iliyopita Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi akiwa pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Katika siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, alizaliwa nchini Ujerumani Albert Einstein, msomi mashuhuri wa fizikia na hisabati. Mnamo mwaka 1921 msomi huyo mahiri alipewa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia, baada ya kufanya juhudi kubwa za kiutafiti. Utafiti na nadharia za Einstein katika uwanja wa nyuklia zilikuwa na taathira kubwa duniani. Hata hivyo Einstein alisikitika sana baada ya kugundua kwamba, uchunguzi na utafiti wake umetumiwa na baadhi ya nchi kwa ajili ya kutengeneza silaha hatari za nyuklia. Albert Einstein alifariki dunia mwaka 1955.