Jumatatu 10 Julai, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 15 Shawwal 1438 Hijria sawa na 10 Julai, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1186 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW kupitia shajara ya Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib (AS). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia mjini Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu. Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika mji wa Rey na wapezi wa Ahlul Bayt AS kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara.

Miaka 276 iliyopita ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark, Vitus Bering. Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari. Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita inayosadifiana na 10 Julai 1940 Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa mkataba wa kivita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa vya Bahamas viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.
