Aug 30, 2017 03:10 UTC
  • Jumatano 30 Agosti, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 8 Mfunguo Pili Dhilhija mwaka 1438 Hijria, mwafaka na tarehe 30 Agosti 2017.

Leo tarehe 8 Dhulhija ni siku ya Tarwiya. Siku hii imepewa jina la siku ya Tarwiya kwa maana ya kijitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji  hayakuwa yakipatikana katika jangwa na Arafat na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafat kutoka Makka tarehe 8 Dhulhija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa.  

Katika siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya. Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya. Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa.

Siku hii ya leo tarehe 8 mwezi Shahrivar katika kalenda ya Iran inatambuliwa kama siku ya kupambana na ugaidi. Sbabu ya jina hilo ni mauaji ya aliyekuwa rais wa Iran Muhammad Ali Rajai na Waziri wake Mkuu Muhammad jawad Bahonar. Katika siku kama hii ya leo miaka 35 iliyopita, Muhammad Ali Rajai Rais wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu Hujjatul Islam Walmuslimiin Muhammad Javad Bahonar waliuawa shahidi baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu. Jinai hiyo ya kinyama ilitekelezwa na Kundi la Kigaidi la Munafiqeen (MKO). Rajai alianza kazi ya ualimu sambamba na kushiriki katika harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah na kuendelea katika njia hiyo hadi ulipopatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, shahidi Rajai alihudumia nyadhifa za mbunge, Waziri wa Elimu na Malezi, Waziri Mkuu na hatimaye Rais. Wakati wa kipindi cha urais wake, Rajai alimteua Dakta Muhammad Javad Bahonar kushika wadhifa wa Waziri Mkuu. Kutokana na juhudi, bidii na ikhlasi waliyokuwa nayo katika kulihudumia taifa la Iran ili kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wa mfumo wa Kiislamu hawakufurahishwa na utendaji kazi wao huo na ndio maana katika tarehe kama ya leo, wakatega bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu na kuwauwa shahidi. Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema baada ya kuuawa shahidi Rajai na Bahonar: "Thamani za mabwana hawa Rajai na Bahonar ni hizi kuwa, viongozi hao walikuwa bega kwa bega na wananchi." 

Muhammad Ali Rajai

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Jamhuri ya Azerbaijan ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi ya zamani. Ardhi ya Azerbaijan ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na silsila ya Kiirani ya Wasasani tangu mwanzoni mwa karne ya Tatu Miladia na katika kipindi kikubwa cha historia yake ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Vita kati ya Urusi ya zamani na Iran vilijiri mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, kufuatia kupenda kujitanua kwa utawala wa kifalme wa Tsar huko katika Umoja wa Kisovieti. Iran ilipata pigo katika vita hivyo na kupelekea sehemu moja ya ardhi ya kaskazini ya Azerbaijan kukaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani mwaka 1813 kwa mujibu wa mkataba wa Golestan.

Bendera ya Azerbaijan

Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.

Bendera ya Timor Mashariki

 

Tags