Sep 28, 2017 03:08 UTC
  • Alkhamisi 28 Septemba 2017

Leo ni Alkhamisi 7 Muharram 1439 Hijria sawa na Septemba 28, 2017.

Tarehe 7 Muharram mwaka 61 Hijria kamanda wa jeshi la Yazid bin Muawiya, Umar bin Sa'd aliliamuru jeshi lake kumzuia maji ya mto Furati Imam Hussein na watu waliokuwa katika msafara wake. Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kumzingira mjukuu wa Mtume (saw) akiwa na jeshi kubwa katika medani ya Karbala, alimwandikia barua Umar bin Sa'd akimtaka amlazimishe Imam Hussein kutangaza utiifu wake kwa mtawala Yazid. Vilevile alimwandikia barua nyingine akimtaka kumzuia Imam Hussein na wafuasi wake wasitumie maji ya mto Furati. Imam Hussein, ndugu, watoto na masahaba zake waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka huo wakiwa na kiu tena kandokando ya maji ya mto Furati.

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kimarekani, Herman Melville. Melville alizaliwa mwaka 1819 na kuanza kujishughulisha na ubaharia. Katika moja ya safari zake, meli ya Melville ilizama na kusukumwa na maji hadi katika kisiwa kimoja ambako wakazi wake walikuwa wakila watu. Melville ameelezea kisa hicho na jinsi alivyowatoroka watu hao katika kitabu alichokipa jina la Typee. Kuchapishwa kitabu hicho, kulizidisha umashuhuri wake.

Herman Melville

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, alifariki dunia rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Abdel Nasser alizaliwa mwaka 1916. Alishiriki katika vita vya kwanza vya Waarabu na utawala wa Kizayuni hapo mwaka 1948 na kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kushirikiana na Jenerali Najib, dhidi ya Mfalme Faruq 1952 na kuung'oa utawala wa kisultani nchini humo. Miaka miwili baadaye Gamal Abdel Nasser alimuondoa madarakani mshirika wake Jenerali Najib na kuchukua jukumu la kuiongoza Misri sambamba na kufanya juhudi za marekebisho, kupambana na ukoloni na utawala ghasibu wa Israel. Mwaka 1956 aliutaifisha mfereji wa Suez na kuufanya kuwa mali ya taifa la Misri, hatua iliyozifanya nchi za Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuishambulia Misri.

Gamal Abdel Nasser

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likiutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kukomesha operesheni ya kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Rasimu ya azimio hilo ililaani uchimbaji huo wa mashimo kinyume cha sheria chini ya eneo hilo takatifu. Hata hivyo upinzani wa Marekani ulipelekea kuondolewa kipengee hicho katika azimio hilo.

Uchimbaji huo wa mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa unaofanywa na Israel ulizusha machafuko ya umwagaji damu mkubwa hapo tarehe 23 Septemba 1996 kati ya askari wa utawala huo ghasibu na Wapalestina ambapo askari hao waliua na kujeruhi mamia ya Wapalestina.

Msikiti wa al Aqsa, Palestina

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita Intifadha ya wananchi wa Palestina kwa mara nyingine tena ilipamba moto. Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Likud na mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika kambi za Sabra na Shatila ya kuingia katika Msikiti wa al Aqswa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu, iliwatia hasira Wapalestina na kuwafanya waanzishe maandamano na mapambano makubwa dhidi ya utawala huo wa Israel.

Intifadha na mapambano ya ukombozi ya Wapalestina