Dec 04, 2017 06:20 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Dis 4

Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tutupie jicho matukio muhimu kadhaa yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita, katika nyuga za spoti, ndani na nje ya nchi. Karibu......

Wanamieleka wa Iran watwaa Kombe la Mashahidi

Timu ya taifa ya mieleka ya vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Mashahidi baada ya kuonyesha michezo mizuri katika mashindano ya kimataifa ya mieleka mtindo wa Greco-Roman hapa nchini. Timu hiyo ya mabarobaro wa Iran ilitwaa ubingwa baada ya kuwapeleka mchakamchaka mahasimu wao wa Russia katika mpambano wa fainali siku ya Alkhamisi, katika Ukumbi wa Michezo wa Enqelab mjini Karaj, yapata kilomita 35 magharibi mwa mji mkuu Tehran.

Mwanamileka wa Greco-Roman wa Iran akipambana na hasimu

Timu A ya Iran iliibuka kidedea baada ya kuitandika Russia alama 6-4 na kutunukiwa medali ya dhahabu. Timu ya Iran ya Tose'eh iliibuka ya tatu baada ya kuicharaza timu nyingine ya nchi hii ya Alborz katika mpambano wa kutafuta mshindi wa medali ya shaba. Azerbaijan ilifunga orodha ya tano bora baada ya kuilemea Timu B ya Iran. Mashindano hayo ya Kombe la Mashahidi katika mchezo wa mieleka mtindo wa Greco-Roman yalianza Novemba 28 na kumalizika kesho yake, kwa kuwaleta pamoja wanamieleka kutoka Armenia, Azerbaijan, Georgia, Iran, Kyrgyzstan, Lebanon, Russia, Syria na Turkey.

Droo ya Kombe la Dunia 2018

Droo ya kupanga makundi ya timu 32 zitakazocheza fainali za Kombe la Soka la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Russia imefanyika Ijumaa usiku nchini humo ambapo Iran imepangwa katika kundi B na itamenyana na Ureno, Uhispania na Morocco. Kundi hilo limetajwa kuwa kati ya makundi magumu zaidi, jambo ambalo amelikiri mkufunzi wa Croatia, Zlatko Dalic.

Maafisa wa FIFA wakitangaza droo ya Kombe la Dunia 

Hata hivyo ni kundi lenye mvuto wa aina yake, kwani kocha wa Timu ya Taifa ya Iran Carlos Queiroz ni raia wa Ureno. Kwa mujibu wa droo hiyo iliyofanyika mjini Moscow, kundi Group A litajumuisha mwenyeji Russia, Saudi Arabia, Misri na Uruguay huku kundi C likiwa na timu za Ufaransa, Australia, Peru na Denmark. Moja ya timu zenye mvuto zaidi barani Afrika Nigeria imewekwa katika kundi D ambalo pia lina Argentina, Iceland na Croatia. Timu ambayo imeshinda Kombe la Dunia mara nyingi zaidi, Brazil iko katika kundi E linalojumuisha Switzerland, Costa Rica na Serbia. Mabingwa watetezo wa Kombe la Dunia, Ujerumani iko katika kundi F ambapo itatetea ubingwa wake kwa kuchuana na Mexico, Sweden na Korea Kusini. Kundi G linajumuisha timu za Ubelgiji, Panama, Tunisia na Uingereza huki kundi H likiwa na timu za Poland, Senegal, Colombia na Japan. Kombe la Dunia mwaka 2018 litaanza Juni 14 na kumalizika Julai 15 nchini Russia.

Michuano ya CECAFA yaanza Kenya

Michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA imeanza kurindima nchini Kenya Jumapili, ambapo mwenyeji ameanza kwa mguu wa kulia huku Tanzania wakilazimishwa suluhu bin suluhu na Libya. Timu ya Soka ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' imeshindwa kutamba mbele ya Libya baada ya kutoka sare ya 0-0 katika mchezo wa Kundi A. Mchezo huo ulifanyika Jumapili katika uwanja wa Kenyatta uliopo Kaunti ya Machakos nchini Kenya na kushuhudia timu zote mbili zikikosa kuona nyavu za mwenzake licha ya Tanzania Bara ambao ni Mabingwa Mara nane wa michuano hiyo kumaliza wakiwa na umiliki wa asilimia 52 kwa 48.

Harambee Stars ikishangilia goli dhidi ya Amavubi

Nahodha na mkufunzi wa Kili Stars wanakiri kupoteza nafasi za wazi na wanasema watafanyia kazi mapungufu yaliyoshuhudiwa katika mechi yao ya ufunguzi. Katika mchezo wa mapema wa ufunguzi, wenyeji timu ya soka ya Kenya 'Harambee Stars' waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Rwanda 'Amavubi'.  Katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa michezo wa Bukhungu kaunti ya Kakamega, bao la kwanza la Kenya lilifungwa na Masoud Juma kwa njia ya penati, huku Duncan Otieno akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Amavubi kwa shuti kali nje ya sanduku la hatari.  Huku hayo yakiarifiwa, siku chache baada ya kuapishwa kwa Emmerson Mnangagwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe, Shirikisho la Soka nchini humo (ZIFA) lilitangaza kujiondoa kwa kikosi chao cha taifa kwenye fainali za kuwania ubingwa wa michuano hii ya Cecafa 'Senior Challenge' mwaka huu wa 2017, kutokana na sababu za kiusalama. Kujiondoa kwa Zimbabwe ni pigo kubwa kwa waandalizi wa kivumbi hicho ambacho kilianza rasmi Jumapili ya Desemba 3 na kinatazamiwa kutamatika Desemba 17. Waandalizi wa michuano hii wamekosoa vikali hatua ya Zimbabwe, taifa ambalo kama Kenya, lilishuhudia mtikisiko na kukurukara za kisiasa hivi karibuni. Zimbabwe na Libya zilizoalikwa kuyajaza mapengo ya Djibouti na Eritrea katika fainali hizo za mataifa 12, zilikuwa zimepanga katika kundi moja na Ethiopia, Sudan Kusini, Burundi na washikilizi wa taji la Cecafa, Uganda. Uganda walitia kapuni ufalme wa Cecafa mnamo 2015 baada ya kuwazidi maarifa Rwanda kwenye fainali iliyofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia. Mashindano ya Cecafa hayakuandaliwa mwaka jana 2016 baada ya taifa la Sudan lililotarajiwa kuwa mwenyeji kujiondoa kisha Kenya iliyotwikwa jukumu la kuwa mwandalizi mbadala kujiondoa pia katika dakika za mwisho.

CECAFA

Huku hayo yakirifiwa, Mkenya Doris Petra amechaguliwa kuwa mwakilishi wa wanawake katika Shirikisho la Cecafa. Katika kongamano la Cecafa lililoandiliwa jijini Nairobi mapema Jumamosi jiji Nairobi, Petra alichaguliwa bila kupingwa kuhudumu kwenye Kamati Kuu kwa kipindi cha miaka miwili. Wengine ni Rais wa Cecafa Mutasim Gafar (Sudan), ambaye hatamu yake ya uongozi itakamilika Novemba mwaka 2019, Abdighaani Arab Said (Somalia), Aimable Habimana (Burundi), Juneid Basha Tilmo (Ethiopia) na Wallace Karia (Tanzania). Katika mkutano huo, Kenya na Sudan zilikubali kuandaa mashindano ya Cecafa ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka 2018.

Wachezaji wa soka walaani utumwa Libya

Mchezaji soka mahiri wa klabu ya Manchester United Paul Pogba amepongezwa na Shirika la Wahajiri Duniani IOM kwa kuanzisha kampeni ya kulaani biashara ya utumwa inayofanyika nchini Libya. Pogba alianzisha kampeni hiyo wiki chache zilizopita, wakati timu yake iliposhuka dimbani kuvaana na New Castle katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza. Pogba ambaye alikuwa anashiriki mechi hiyo baada ya kuwa ya uwanja kwa muda, alishangilia goli lake wakati huo kwa kuwekelea mkono mmoja juu ya mwingine mfano wa mtu aliyefungwa pingu. Watu wachache walielewa alichokiashiria Pobga, na kwa ambao hawakuelewa, alitoa ufafanuzi kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram. Aliandika kuwa: Pamoja na kuwa nina furaha kurejea uwanjani, lakini maombi yangu yawaendee wathirika wa biashara ya utumwa Libya.

Pogba

Namuomba Allah asimame na nyinyi na ukatili huu ufikie tamati." Itayi Viriri, Mkuu wa Mawasiliano ya Mtandao wa IOM amesema Pogba alikuwa na khiari ya kusherekehea goli lake hilo kwa mtindo tofauti, lakini akaamua kutoa hamasisho hilo juu ya suala la utumwa. Viriri amesema mchango wa Pogba katika kufikisha kwa walimwengu ujumbe wa kulaani utumwa nchini Libya ni wa kupigiwa mfano na ni kitendo ambacho hakijafanywa na hata mwanasiasa mmoja. Pogba aliazaliwa na kulelewa Ufaransa, na wazazi wahajiri wenye asili ya Guinea. Wachezaji wengine wamefuata mkondo huo wa pogba wa kushangilia goli kwa alama ya kupigwa pingu, wakiwemo Cedric Bakambu wa klabu ya Villareal na mwenye asili ya Kongo DR, Geoffrey Kondogbia wa Valentia mzaliwa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cheikhou Kouyate wa Senegal na Cheikh Doukoure wa Kodivaa. Hivi karibuni ilienea video kwenye mitandao ya kijamii inayoonyesha raia wa nchi za Kiafrika wanaohajiri kuelekea Ulaya wakiuzwa kama watumwa nchini Libya kwa kiasi cha dola 400, jambo ambalo limelaani vikali kote duniani.

......................................TAMATI..........................