Jan 17, 2018 02:39 UTC
  • Jumatano tarehe 17 Januari, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 29 Rabiuthani 1439 Hijria, inayosadifiana na Januari 17, 2018

Miaka 766 iliyopita, alizaliwa Muhammad bin Ahmad Dhahabi, anayejulikana kwa lakabu la Shamsuddin, mpokezi wa hadithi na mwanahistoria mashuhuri wa zama hizo. Dhahabi alikuwa akipenda sana kukusanya hadithi na alifanya safari nyingi katika pembe mbalimbali duniani ili kukamilisha elimu hiyo. Muhammad bin Ahmad Dhahabi alisimuliwa hadithi nyingi sana kutoka kwa wazee na maulamaa katika safari zake hizo. Miongoni wma vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni al Kashif, Tabaqatul Qurraa, al Mu'jamul Saghiir na al Mu'jamul Kabiir. Mwanazuoni huyo alifariki dunia mwaka 748 Hijria katika mji wa Damascus. 

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita, mlima mrefu zaidi duniani uligunduliwa na mpanda milima wa Kiingereza kwa jina la George Everest na mlima huo ukapewa jina lake. Hata hivyo, George Everest alishindwa kufika juu ya kilele cha mlima huo. Wapanda milima wawili kutoka India na Uingereza walifanikiwa kufika juu ya kilele cha mlima huo mwaka 1953. Mlima Everest una urefu wa mita 8800 na ni katika silsila ya milima ya Himalaya ambayo inaanzia kaskazini mwa India hadi magharibi mwa Uchina.

Mlima Everest

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita yaani tarehe 27 Dey 1334 Hijria Shamsia, Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Navvab Safavi

Miaka 57 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliuliwa Patrice Lumumba, mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokipa jina la "Kongo, Nchi Yangu."

Patrice Lumumba

Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na mmoja wa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein.

Sayyid Mahdi Hakim

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa chini ya uongozi wa Marekani vilizishambulia ngome za wanajeshi wa Iraq huko Kuwait na Iraq ili kukomesha kukaliwa kwa mabavu Kuwait na jeshi la utawala wa Saddam. Mgogoro huo ulianza tarehe Pili mwezi Agosti mwaka 1990 baada ya utawala wa zamani wa Iraq kuikalila kwa mabavu ardhi ya Kuwait.

Askari wa Marekani katika jangwa la Saudi Arabia

Na miaka 9 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni maghasibu walilazimika kutangaza usitishaji vita baada ya jeshi la utawala wa Israel kufanya mashambulizi ya kinyama ya siku 22 dhidi ya raia wa Ukanda wa Ghaza. Katika mashambulizi hayo, utawala wa Kizayuni ulikusudia kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas au kwa uchache kuilazimisha harakati hiyo ikubali mazungumzo eti ya mapatano. Hata hivyo uungaji mkono wa Wapalestina kwa harakati ya Hamas na vilevile malalamiko makali ya walimwengu dhidi ya jinai za wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Ghaza, yaliulazimisha utawala haramu wa Israel usitishe mashambulio yake.

Ukanda wa Ghaza

 

Tags