Jumamosi, 7 Aprili, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 20 ya mwezi wa Rajab 1439 Hijria mwafaka na tarehe 7 Aprili 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1426 sawa na tarehe 2o Rajab mwaka wa 13 Hijria, vilitokea vita vya Yarmuk kati ya jeshi la Kiislamu na jeshi la utawala wa kifalme wa Roma ya Mashariki katika bonde lililojulikana kwa jina hilo huko Palestina. Ushindi wa Waislamu huko Sham, yaani Syria ya sasa ulimpelekea mfalme wa Roma kuandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Lakini, Waislamu waliweza kutoa pigo kwa wanajeshi wa mfalme wa Roma licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiganaji na suhula chache za kivita. Kufuatia ushindi huo Waislamu walisonga mbele na kufika eneo la Mashariki la Ufalme wa Roma na mwaka mmoja baadaye Waislamu wakafanikiwa kuchukua udhibiti wa mji wa Baitul Muqaddas pasina umwagaji damu. ***

Katika siku kama ya leo miaka 297 iliyopita, Peter the Great mfalme wa wakati huo wa Russia aliivamia Sweden. Ruussia na Sweden zikishirikiana na Poland na Denmark kuanzia mwaka 1700 zilikuwa katika vita vya kaskazini. Wakati jeshi la Russia linaishambulia Sweden nchi hiyo ilikuwa imefikia mapatano na nchi nyingine zilizokuwa pamoja vitani na ilikuwa na mpango wa kupatana na Russia pia. Hata hivyo Peter the Great ambaye alikuwa na nia ya kupanua mamlaka yake, akiwa na jeshi lililojizatiti aliishambulia Sweden na baada ya kuishinda akaitwisha nchi hiyo mkataba wa amani. ***

Miaka 96 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kufanya utafiti na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu. Profesa. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu". ***

Katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, aliaga dunia msomi na mvumbuzi maarufu wa Kimarekani Henry Ford. Mvumbuzi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 84. Ford alizaliwa mwaka 1863 katika familia ya kimasikini katika kijiji cha Greenfield nchini Marekani. Akiwa bado barobaro Henry Ford alijishughulisha na utengenezaji wa saa na alipokuwa kijana alifanya kazi ya umakanika. Henry Ford anatambuliwa kuwa mmoja wa wavumbuzi wa magari. ***

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya baraza la kwanza la dunia la afya na kuandika hati ya kwanza ya mkutano wa kimataifa wa afya. Baraza hilo pia lilichukua uamuzi kwamba tangu mwaka 1950 tarehe 7 Aprili itakuwa Siku ya Kimataifa ya Afya. Tangu mwaka huo tarehe 7 Aprili kila mwaka imekuwa ikiadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Afya. ***

Na miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 18 mwezi Farvardin mwaka 1343 Hijria Shamsiya, Imam Khomeini (MA) Kiongozi na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliachiwa huru kufuatia malalamiko na mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. Usiku wa tarehe 15 Khordad mwaka 1342 Hijria Shamsia vikosi vya usalama vya utawala wa Shah vilimtia mbaroni na kumfunga jela Imam Khomeini baada ya kutoa hotuba iliyokuwa ikifichua maovu ya utawala wa Shah. Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakitaka kuachiwa huru kiongozi wao. Radiamali kali ya wananchi wa Iran iliulazimisha utawala wa Shah kumwachia huru Imam Khomeini na baadae kumpeleka nyumbani kwake, ambako huko aliwekwa chini ya uangalizi maalumu. ***
