Apr 21, 2018 10:40 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (44)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 44.

Kwa wale wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila ya shaka mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba miaka kumi ya vita vikali kati ya wapiganaji wa makundi ya jihadi ya Afghanistan na majeshi ya Shirikisho la Kisovieti la Urusi kuanzia mwaka 1979 hadi 1989 kwa upande mmoja, na kuvurugika uthabiti na kuzuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya makundi ya mujahidina kwa upande mwengine viliisambaratisha misingi ya uchumi wa Afghanistan na kusababisha ufakiri na umasikini ndani ya nchi. Tukabainisha pia kuwa kuendelea na kushadidi hali hiyo ya umasikini miongoni mwa wananchi ilikuwa moja ya sababu muhimu zaidi za kujitokeza kundi lenye misimamo ya kufurutu mpaka la Taliban. Vilevile tulisisitiza kuwa nukta hiyo ni ya kutiliwa maanani kwa sababu, akthari ya wapiganaji wa kundi la Taliban na vitengo vikuu vya kundi hilo vilitokana na vijana wa matabaka ya chini na ya mafakiri katika jamii ya Afghanistan hususan ya Wapashtun, ambao katika miaka ya baada ya kuondoka majeshi ya Urusi na kumalizika vita vya makundi ya jihadi walikuwa wakisoma kwenye madrasa za kidini nchini Pakistan, ili, kwa msaada mdogo wa kifedha waliokuwa wakipata kutoka kwa viongozi wa kidini wa madrasa hizo wakati wakiwa masomoni, waweze kujiondoa kwenye hali ya ukata na ufukara. Hali mbaya ya uchumi na ukata wa kiutamaduni kwa upande mmoja, na ushawishi wa tangu na tangu wa desturi za kidini pamoja na hamu ya kusoma katika madrasa ni sababu muhimu iliyoziwezesha baadhi ya nchi za eneo kuiunda na kuitumia harakati ya Taliban kama kundi la kidini na kijeshi.

 

Kama ilivyoashiriwa hapo kabla, harakati ya Taliban ambayo ni harakati yenye taasubi za kidini za kufurutu mpaka na ambayo ilikuwa mstari wa mbele katika kuzusha hitilafu baina ya makundi mbalimbali ya Waislamu wa Afghanistan na vilevile katika kuanzisha mashindano na uadui kati ya nchi za Kiislamu, ilishadidisha moto wa vita na mizozo ya kimadhehebu na kupelekea kumwagwa damu za Waislamu wengi. Kutokana na mafunzo waliyopata walipokuwa masomoni kwenye baadhi ya madrasa, wafuasi wa kundi la Taliban waliitakidi kwamba kushiriki katika operesheni za mapambano ya silaha kwa ajili ya kuasisi mfumo wa utawala wa kidini nchini Afghanistan ni jambo la faradhi kwao, na hata wakaipa hadhi harakati ya aina hiyo kuwa ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mtazamo ulio dhidi ya Shia uliokuwemo kwenye mafundisho ya Taliban na kuwachukulia Mashia kuwa ni watu waliotoka nje ya misingi ya dini ulishadidisha taasubi za kidini katika harakati za safu za kijeshi za Taliban katika mauaji na umwagaji wao damu za ndugu zao Waislamu. Bila shaka hatuwezi kuipuuza pia nafasi ya baadhi ya watawala madikteta wa nchi za Kiislamu katika mchakato wa kujitokeza Taliban na muendelezo wa harakati zao. Miongoni mwao, hasahasa ni watawala wa Saudi Arabia ambao walihusika moja kwa moja katika uundaji wa kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji kupitia misaada ya kitita kikubwa cha fedha walizokuwa wakitoa kila mwaka kupitia taasisi ya "Ar-Rabit'atul-Alamul- Islamiyyah" kwa ajili ya mtandao mpana wa ujenzi wa misikiti na madrasa katika kila pembe ya dunia. Hakuna shaka yoyote kuwa misaada hiyo ya Saudia na vilevile misaada ya baadhi ya nchi nyengine za eneo katika kuundwa na kuimarishwa Utalibani ilikuwa na mchango hasi na wenye taathira ya kushadidisha migawanyiko na mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu.

*******

Taathira ya sababu za nje katika kuasisiwa vuguvugu la Utalibani haikuhusiana tu na kujiingiza kijeshi Urusi nchini Afghanistan na uungaji mkono wa Marekani au baadhi ya nchi za Kiislamu kwa mujahidina wa Afghanistan, lakini nchi za Magharibi na hasa Marekani ilichangia pia katika kuliwezesha kundi la Taliban kutwaa madaraka nchini humo. Marekani haikuhisi ni jambo baya Taliban kushika hatamu za utawala nchini Afghanistan, ambapo ingeweza kudhamini maslahi ya mafuta ya mashirika ya Kimarekani na wakati huohuo, kwa sababu ya dhati ya kundi hilo ya kuwa na chuki na Iran, kuzuia ushawishi wa Iran katika nchi hiyo na eneo la Asia ya Kati. Kwa maneno mengine ni kuwa Wamarekani walifanya kila njia kupitia uungaji mkono wao kwa Taliban, kuipa nguvu fikra kinzani ya kundi hilo ya Uislamu wenye sura katili, isiyo na mantiki na inayowiyana na udikteta wa ndani na uingiliaji wa maajinabi, kwa ajili ya kukabiliana na fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran iliyosimama juu ya msingi wa kupinga uimla na uistikbari na kuonyesha sura ya huruma na urehemevu ya Uislamu. Na muhimu zaidi ya hayo, uliiwekea changamoto kali kwa kufufua mipasuko ya kikaumu na kimadhehebu, fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ilikuja na mtazamo mpya wa kuboresha demokrasia katika jamii za Kiislamu kwa njia ya kuutawalisha mfumo wa utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi ndani ya jamii na kuwaunganisha Waislamu kwa kuweka kando hitilafu baina ya Shia na Suni katika upeo wa Ulimwengu wa Kiislamu. Ni dhahiri kwamba hatua ya Marekani ya kuishambulia kijeshi na kuivamia Afghanistan kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi na uamuzi wa kuuangusha utawala wa Taliban baada ya matukio ya Septemba 11 mwaka 2001 haiwezi kutufanya tufumbie macho nafasi ya nchi hiyo katika uundwaji wa kundi hilo la kigaidi.

Wapenzi wasikilizaji katika mifululizo kadhaa iliyopita ya kipindi hiki tumejaribu kuchambua na kuhakiki sababu za kujitokeza kundi la Taliban na nadharia ya ukufurishaji ya kundi hilo kwa kuzingatia taathira za sababu za ndani na za nje zilizochangia kuleta mpasuko katika umma wa Kiislamu kupitia kuundwa kundi hilo ambalo ni moja ya harakati potofu za kisiasa na kiitikadi katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika sehemu ijayo ya 45 ya kipindi hiki tutakuja kuzungumzia kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH ambapo tutaonyesha pia kwamba kundi hilo, kama lilivyokuwa kundi la Taliban, ni matokeo na kielelezo halisi cha mfungamano wa sababu za ndani na nje zilizoungana pamoja kuleta mpasuko na mfarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo, nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani.

Tags