Apr 21, 2018 10:50 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (45)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 45.

Kama nilivyokuahidini wapenzi wasikilizaji mwishoni mwa mazungumzo yetu katika kipindi kilichopita, kwamba katika sehemu ya 45 ya mfululizo huu tutakuja kuzungumzia chimbuko, fikra na vitendo vya kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH, ambalo kwa hatua yake ya kufufua hitilafu baina ya Shia na Suni na kuwasha moto wa mashambulio ya kijeshi limetoa pigo na jeraha kubwa zaidi la kihistoria kwa mwili wa umma wa Kiislamu na umoja wa Waislamu sambamba na kuuimarisha na kuupa nguvu utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Historia ya kuundwa na kujitokeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Dola la Kiislamu la Iraq na Sham, ambalo ufupisho wake kwa lugha ya Kiarabu ni DAESH na kwa Kiingereza ni ISIS, inarejea mwaka 2004, wakati Abu Mus-ab Az-Zarqawi, kiongozi wa mtandao wa Al-Qaeda nchini Iraq alipoasisi kundi liitwalo Jamaatu-Tawhid Wal-Jihad. Zarqawi, ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo alitangaza ba'ia na tamko la utiifu kwa mtandao wa Al-Qaeda uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden na kuwa mwakilishi wa mtandao huo katika eneo hilo. Mwishoni mwa mwaka 2006 vyombo vya habari viliripoti habari ya kuundwa kundi la kijeshi liitwalo Dola la Kiislamu la Iraq linaloongozwa na Abu Omar Baghdadi likiwa ni nembo iliyojumuisha makundi na mitandao yote yenye misimamo ya kufurutu mpaka yaliyokuwa yakiendesha harakati zao ndani ya ardhi ya Iraq. Mtandao wa Al-Qaeda, ambao wakati Iraq ilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Marekani ulikuwa ukijulikana kama kundi la jihadi ya kupambana na majeshi ya Marekani lilifanikiwa kuwavutia vijana wengi wa Kiiraqi waliopinga kuwepo vikosi vya jeshi la Marekani ndani ya ardhi ya nchi yao na kuunda kundi lenye nguvu zaidi la wanamgambo nchini Iraq. Abu Mus-ab Az-Zarqawi aliuliwa na wanajeshi wa Marekani mwaka 2006; na mmoja wa wanachama wakuu wa kundi lake la Jamaatu-Tawhid Wal-Jihad aitwaye Abu Hamzah Al-Muhajir ndiye aliyeshika hatamu za uongozi wa kundi hilo. Al-Muhajir alifanya kazi kubwa ya kupanua harakati za kundi hilo na kupanga operesheni mbalimbali za mashambulio dhidi ya majeshi ya Marekani mpaka hatimaye mnamo mwaka 2010, yeye pamoja na kamanda mwengine mwandamizi wa kundi hilo aitwaye Abu Omar Al-Baghdadi wakauawa katika shambulio lililofanywa kwa ushirikiano kati ya vikosi vya Iraq na Marekani. Baada ya kupita siku kumi, baraza la ushauri la kundi la Dola la Kiislamu la Iraq lilifanya kikao na kumchagua Abubakar Al-Baghdadi kuwa kiongozi wa kundi hilo. Abubakar Al-Baghdadi, alizaliwa mwaka 1971 katika mji wa Samarra, huko nchini Iraq katika ukoo wa kidini wenye itikadi za usalafi wa ukufurishaji. Alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Baghdad. Al Baghdadi anajulikana kama moja ya mihimili ya Usalafi wa kijihadi na mmoja wa wananadharia mashuhuri wa Utakfiri.

 

Baada ya miaka kadhaa ya uwanachama katika mtandao wa Al Qaeda na kushirikiana katika medani za vita na magaidi waliokubuhu wa kundi hilo la kihalifu, mnamo mwaka 2010 Abubakar Al-Baghdadi alishika hatamu za uongozi wa kundi liitwalo Dola la Kiislamu la Iraq.

Mwaka mmoja baada ya kuanza mgogoro wa Syria, Abubakar Al-Baghdadi aliitumia kadhia hiyo kama fursa adhimu kwake ya kupeleka magaidi walio chini ya uongozi wake huko nchini Syria na kupiga hatua ya kwanza ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mtawala wa ile iliyokuwa ikijulikana kama ardhi ya Sham. Katika muelekeo wa kufikia lengo hilo na kwa kutumia mbinu ya Al Qaeda, naibu wa Al Baghdadi aitwaye Abu Muhammad Al Julani alianzisha kundi jengine la watenda jinai kwa jina la Jabhatu-Nusra ndani ya ardhi ya Syria. Lakini baada ya kuongezeka ushawishi wa Al Julani nchini Syria na msimamo wake wa kukataa kundi lake kuwa chini ya uongozi wa Al Baghdadi na kuundwa kundi la Dola la Kiislamu la Iraq na Sham (DAESH), makundi hayo mawili yalitengana na mapigano makali ya umwagaji damu yakatokea baina ya pande mbili.

Hata hivyo ieleweke kwamba mapigano kati ya makundi hayo mawili halikuwa jambo la ajabu wala la kushtukiza kwa wanachama hao wenye ukuruba na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, kwa sababu baada ya kutangazwa kifo cha kiongozi wa mtandao huo Usama bin Laden, Abubakar Al Baghdadi alikuwa ndiye mtu pekee ambaye hakula kiapo cha utiifu cha kumpa mkono wa bai'a mrithi wa bin Laden Ayman Adh-Dhawahiri.

 

Kwa mujibu wa watu wa karibu na Al Baghdadi, yeye alikuwa akiitakidi kuwa kujikita mahali pamoja tu kutawafanya wafuasi wake washindwe na kusambaratishwa na kwamba yeye ana mambo mengi sana ya kushtukiza ya kuwafanyia maadui zake. Daesh waliweza kutumia vyanzo vya mapato ya fedha kujijenga na kujiimarisha. Kwa mujibu wa duru zilizokuwa karibu na kundi hilo la kitakfiri, uuzaji mafuta ya Syria kwa njia za magendo uliijazia hazina ya Abubakar Al-Baghdadi mamilioni ya dola; na baada ya magaidi wa kundi hilo kuingia kwenye mji wa Mosul nchini Iraq walijizolea silaha na zana za kivita chungu nzima kwenye maghala ya silaha za jeshi la nchi hiyo. Duru hizo aidha zilieleza kuwa hatua ya nchi za Kiarabu na za Magharibi ya kuendelea kulipatia kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh misaada ya fedha na silaha kuliliwezesha kundi hilo kujizatiti na kuweza kuendelea kuwepo.

Kundi la kigaidi la Daesh lilikuwa ndilo kundi la ukufurishaji lenye harakati kubwa zaidi na misimamo ya kufurutu mpaka zaidi katika maeneo ya ndani ya ardhi za Syria na Iraq. Kundi hilo lililokuwa na mchanganyiko wa wapiganaji wenye misimamo ya Kisalafi, Kiwahabi pamoja na mabaki ya wafuasi wa Kibaathi lilikuwa likipata misaada ya siri na ya dhahiri ya baadhi ya nchi za Kiarabu na za Magharibi. Tunaweza kuthubutu kusema kuwa kundi la Dola la Kiislamu la Iraq na Sham ni tunda la sumu lililotokana na mti khabithi wa hujuma na uvamizi wa kijeshi uliofanywa na majeshi ya Marekani na Uingereza mwaka 2003 dhidi ya Iraq, ambalo kupitia kaulimbiu ya kupambana na Marekani lilitumia na kushamirisha kampeni bandia za kidini na kujifanya mdhulumiwa ili baada ya kuwatimua wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq lishike hatamu badala yake kwa kuyapa uhalali wa kisheria malengo yake ya kuunda hicho lilichokiita "Dola la Kiislamu la Iraq na Sham", kwa kifupi DAESH au ISIS.

Wasikilizaji wapenzi, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa kwa leo nikiwa na matumaini kuwa mtakuja kujiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo katika sehemu nyengine ya mfululizo huu. Nakuageni basi, huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags