Apr 21, 2018 10:53 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (46)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 46.

Katika kipindi kilichopita tulieleza kuwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu la Iraq na Sham ni tunda la sumu lililotokana na mti khabithi wa hujuma na uvamizi wa kijeshi uliofanywa na majeshi ya Marekani na Uingereza mwaka 2003 dhidi ya Iraq, ambalo kupitia kaulimbiu ya kupambana na Marekani lilitumia na kushamirisha kampeni bandia za kidini na kujifanya mdhulumiwa ili baada ya kuwatimua wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq lishike hatamu badala yake kwa kuyapa uhalali wa kisheria malengo yake ya kuunda hicho lilichokiita "Dola la Kiislamu la Iraq na Sham", kwa kifupi DAESH au ISIS.

Kuondoka Marekani nchini Iraq, mgogoro wa Syria, kubadilika medani na uwanja wa harakati za kundi la Daesh kutoka Iraq na kuhamia Syria na kukaribiana mitazamo ya Marekani, Israel na Saudi Arabia kuhusiana na serikali ya Bashar Al-Assad kulifungua ukurasa mpya katika uhusiano wa kundi hilo la kigaidi na nchi hizo. Mwanzo wake, kundi la ukufurishaji la Daesh lilianzisha vita dhidi ya serikali ya Syria kwa kaulimbiu na kisingizio cha kupigania haki za Masuni wa nchi hiyo, lakini baada ya vipigo vya mtawalia lilivyopata kwa jeshi la Syria na kupoteza udhibiti wa miji na maeneo ya kistratijia liliyokuwa limeyakalia kwa msaada wa kiintelijinsia na silaha wa baadhi ya nchi, liliamua kuanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya nchi jirani ya Iraq na kuishikilia baadhi ya miji na maeneo muhimu ya nchi hiyo.

Daesh lilikuwa likijinadi kuwa lengo lake kuu ni kuhuisha utawala wa Khilafa ya Kiislamu na kutekeleza kama inavyotakiwa sheria za Kiislamu; lakini lilitenda jinai za kinyama na za kutisha dhidi ya binadamu kwa kutumia jina hilo hilo la Uislamu. Haikupita hata siku moja bila magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh kutenda jinai mpya iliyodhihirisha na kuweka wazi uovu na uduni wao wa kinafsi. Katika mapigano na harakati zake za kijeshi, kundi la kigaidi la Daesh limekuwa likiwatumia watoto na vijana chipukizi kutekeleza operesheni za kujitoa mhanga na kutosita kutenda kitendo chochote kile kiovu na cha kinyama kwa ajili ya kufikia malengo yake. Mwanachama mmoja wa Daesh aliyejitenga na kundi hilo la ukufurishaji amezungumzia baadhi ya jinai alizotenda yeye mwenyewe kwa kusema: Nilipojiunga na Daesh na kuwa mwanachama wa kundi hili na kupelekwa Syria, badala ya kwenda vitani, kwa amri ya Amir, (akiwa na maana ya kiongozi wa genge hilo), ilinibdi niwe mlinzi wa jela, ambapo niliamriwa niwatandike mijeledi wafungwa wote, wake kwa waume; na hili ni jambo ambalo sitolisahau katu. Mimi sikuwa nikiwasaili wafungwa na mahabusu wala kuwauliza chochote, zaidi ya kuwapiga na kuwaadhibu tu; baadhi ya watu hao nilikuwa nikiwatandika viboko 80 na baadhi ya wengine nikiwapiga viboko 40. Hakukuwa na tofauti kwangu mimi kati ya mwanamke na mwanamme na kitendo hicho kilikuwa kikiitwa Jihadi katika jela.

 

Bila shaka yoyote kuundwa kwa genge la kitakfiri na la kigaidi la Daesh, chanzo chake kinarejea kwenye malengo na nia za nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo la Mashariki ya Kati. Kadiri siku zinavyopita ndivyo nafasi ya Marekani katika uundwaji wa kundi hili inavyozidi kudhihirika. Ungamo la Michael Flynn, Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Intelijinsia ya Ulinzi ya nchi hiyo (Defence Intelligence Agency) ni moja ya ushahidi unaothbitisha ukweli huo. Katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya televisheni ya Aljazeera ya Qatar, Flynn aliweka hadharani nyaraka zinazothibitisha kuwa mnamo mwanzoni mwa mwaka 2012, yaani ukiwa umepita mwaka mmoja tangu ulipoanza mgogoro wa Syria mwezi Aprili mwaka 2011, Shirika la Intelijinsia ya Ulinzi la Marekani lilikuwa limeshatabiri kuhusu kujitokeza kwa Daesh nchini Iraq; lakini badala ya kulichukulia kundi hilo kuwa tishio na kukabiliana nalo, lililiangalia kama wenzo wa kistratijia ili kuweza kufanikisha malengo ya Marekani katika eneo.

Afisa huyo wa zamani wa Shirika la Marekani la Intelijinsia ya Ulinzi ameeleza bayana kuwa kutokupa umuhimu kupata nguvu na kutwaa madaraka makundi yenye misimamo ya kufurutu ada nchini Syria ni hatua iliyochukuliwa kwa “kutaka na kwa makusudi” na serikali ya Marekani; na Washington ilipuuza makusudi hatari ya makundi hayo.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2011, yaani ikiwa imepita miezi saba tu tangu ulipoanza mgogoro wa Syria tarehe 15 Machi 2011, hadi katikati ya mwezi Septemba mwaka 2012, aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo Barack Obama, alikuwa na taarifa kuhusu utumaji silaha zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Benghazi nchini Libya na kupelekewa makundi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu mpaka nchini Syria na yale yanayobeba silaha yasiyo na misimamo hiyo; na licha ya kwamba Umoja wa Mataifa ulikuwa umeweka vikwazo na marufuku ya kutumwa silaha ya aina yoyote nchini humo iwe ni kwa serikali au makundi ya upinzani, Obama hakuchukua hatua yoyote ya kukabiliana na utumwaji huo wa silaha.

 

Mbali na nafasi ya Marekani, hatuwezi kughafilika pia na nafasi ya baadhi ya nchi za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia, katika uundaji na uimarishaji wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh.

Duru za kuaminika ziliripoti mara kadhaa taarifa kuhusu maelfu ya malori yaliyosheheni silaha na zana za kivita ambayo yalivuka mpaka wa Saudia na kuingizwa ndani ya ardhi ya Iraq katika kipindi cha siku tano tu tangu Daesh ilipotangaza uwepo wake. Aidha taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mbali na kuyasaidia kwa silaha makundi ya kitakfiri nchini Iraq, Saudi Arabia ilikuwa na nafasi kubwa pia katika utoaji rushwa na kuwanunua maafisa wa jeshi la Iraq ili badala ya kupambana na magaidi wa kundi la Daesh, askari wa jeshi la nchi hiyo wakimbie na kurudi nyuma na kuyaacha maeneo mbalimbali ya ardhi ya Iraq yaingie mikononi mwa kundi hilo. Baadhi ya wataalamu wamesema, sababu zilizoufanya utawala wa Aal Saud ushupalie kulisaidia na kuliunga mkono kundi hilo ni hofu ya kuchelea kuundwa utawala wa Kishia ndani ya ardhi ya Iraq unaofanana na ule ulioko nchini Iran. Wasaudi wanajua kwamba kuasisiwa utawala wa wananchi kwa mfumo wa wingi wa kura nchini Iraq, kikiwa ni kitovu cha Mashariki ya Kati, ni ishara dhahiri ya kuanza mageuzi na mabadiliko katika Ulimwengu wa Kiarabu na harakati ya nchi za eneo kuelekea kwenye mifumo ya tawala za wananchi. Na hakuna shaka kuwa muda si mrefu upepo wa uundwaji wa serikali za kidemokrasia za Kiislamu utazivumia pia nchi tajiri zaidi na zenye tawala za kiimla na za udikteta mkubwa zaidi katika eneo hili.

 Wasikilizaji wapenzi, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa huku nikitumai kuwa mumeelimika na kunufaika na yote mliyoyasikia katika mfululizo huu. Tutakutana tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo, katika sehemu ya 47 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags