Apr 21, 2018 10:56 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (47)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 47.

Kwa wale wasikilizaji wetu mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika sehemu iliyopita ya 46 tuliizungumzia nafasi ya Marekani katika uundwaji wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Tulieleza kwamba kwa mujibu wa ungamo la Michael Flynn, Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Intelijinsia ya Ulinzi ya Marekani, (Defence Intelligence Agency), mnamo mwanzoni mwa mwaka 2012, yaani ukiwa umepita mwaka mmoja tangu ulipoanza mgogoro wa Syria mwezi Aprili mwaka 2011, shirika hilo la Intelijinsia lilikuwa limeshatabiri kuhusu kujitokeza kwa Daesh nchini Iraq; lakini badala ya kulichukulia kundi hilo kuwa ni tishio na hivyo kukabiliana nalo, lililiangalia kama wenzo wa kistratijia ili kuweza kufanikisha malengo ya Marekani katika eneo. Lakini mbali na Marekani, tulibainisha kwamba hatuwezi kughafilika pia na nafasi ya baadhi ya nchi za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia, katika uundaji na uimarishaji wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh.

Kwa mfano tu tuliashiria duru za kuaminika zilizoripoti mara kadhaa taarifa kuhusu maelfu ya malori yaliyosheheni silaha na zana za kivita ambayo yalivuka mpaka wa Saudia na kuingizwa ndani ya ardhi ya Iraq katika kipindi cha siku tano tu tangu Daesh ilipotangaza uwepo wake. Aidha tulieleza kwamba kuna taarifa zilizothibitisha kuwa mbali na kuyasaidia kwa silaha makundi ya kitakfiri nchini Iraq, Saudi Arabia ilikuwa na nafasi kubwa pia katika utoaji rushwa na kuwanunua maafisa wa jeshi la Iraq ili badala ya kupambana na magaidi wa kundi la Daesh, askari wa jeshi la nchi hiyo wakimbie na kurudi nyuma na kuyaacha maeneo mbalimbali ya ardhi ya Iraq yaingie mikononi mwa kundi hilo.

 

Lakini mbali na Marekani na Saudi Arabia, utawala wa Kizayuni wa Israel ni mhimili mwingine wa tatu katika mkakati wa uundaji na utoaji uungaji mkono kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Kwa hatua yake ya kuliimarisha kundi la Daesh, utawala wa Kizayuni umewasha moto wa vita na uadui baina ya Waislamu ili kuweza kuupatia kinga ya miaka kadhaa uwepo wake haramu. Kwa kushirikiana na Saudi Arabia na kwa njia ya kuliimarisha kundi la kigaidi la Daesh, Wazayuni wamekuwa wakijaribu kulidhibiti vuguvugu la muqawama wa Kiislamu linaloongozwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Matunda ya mfungamano wa kuaibisha na kufedhehesha uliopo baina ya Israel na Saudi Arabia ni kuudhoofisha Ulimwengu wa Kiislamu, kuimarisha misingi ya utawala wa Kizayuni na kudhaminiwa maslahi ya madola ya Magharibi. Profesa Anthony James Hall anaitakidi kuwa "ili kuelewa barabara muundo na uundwaji wa Daesh, kuna udharura kwanza kuielewa sawasawa sura na dhati halisi ya mhimili wa pamoja wa Saudia na Israel. Madaesh ni wapiganaji wabeba silaha wa utawala wa Kizayuni na Magharibi ambao wanaendesha harakati dhidi ya Waislamu wenyewe; na kwa hakika hii ni changamoto ya Wazayuni dhidi ya Waislamu. Daesh ni kielelezo cha uadui na uhasama wa kihistoria wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Uislamu. Katika maeneo mengi ya mapigano zimeshuhudiwa alama za Uzayuni na stratijia za Uzayuni wa kimataifa, ambao lengo lake ni kupanua zaidi ufa wa mpasuko na hitilafu kati ya Waislamu; na huu kwa hakika ni mkakati wa mfumo wa ubeberu wa Magharibi wa kuzusha mfarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu ili kuweza kuudhibiti. Mfumo huo unawekeza ili kufikia lengo hilo; na kwa kupitia stratijia na mikakati yake, unazitumia baadhi ya pande za Ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya ulimwengu wenyewe wa Kiislamu; na mchakato huo una chimbuko la kihistoria”.

**********

Wasikilizaji wapenzi kama tulivyowahi kueleza hapo kabla, tunapoyahakiki matukio na mabadiliko yanayojiri katika Ulimwengu wa Kiislamu pamoja na miinuko na mishuko yake tutabaini kuwa katika masuala yanayoweza kuleta umoja, sababu za kisiasa na kiuchumi zinaweza kuwa na nafasi kubwa katika kuleta au kuimarisha umoja na mshikamano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa upande wa kisiasa ni kwa kuchukua msimamo mmoja dhidi ya adui yao wa pamoja yaani Israel. Na kwa upande wa kiuchumi ni kwa kuzingatia manufaa na maslahi yao ya pamoja ya kiuchumi. Katika sehemu hii ya kipindi chetu tutajaribu kuonyesha kuwa suala la Palestina ambalo ni kadhia muhimu zaidi kwa Ulimwengu wa Kiislamu lina uwezo na fursa nyingi mno za kuwezesha kupatikana mshikamano na kuwepo muelekeo wa pamoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, kwa sababu uadui wa Israel kwa Uislamu na nchi za Kiislamu ni jambo la wazi kabisa na lisiloweza kukanushika. Lakini isitoshe pia ni kwamba kupatikana haki za Wapalestina na kukabiliana na uchu wa kutotosheka na wa kutaka kujipanua wa Israel ni moja ya matakwa muhimu zaidi ya wananchi katika nchi zote za Kiislamu. Kwa hivyo ikiwa serikali za nchi za mataifa ya Waislamu zitaishughulikia kadhia hii zitazidi kuimarisha misingi ya uhalali wa kisiasa wa kukubalika kwao mbele ya wananchi wao na kuandaa mazingira ya kupatikana umoja baina yao na nchi nyingine za Kiislamu. Kuna mifano mingi katika historia inayoonyesha ni kwa kiwango gani kuwa na sauti moja nchi za Kiislamu kuhusiana na kadhia ya Palestina kumeweza kuimarisha mshikamano wa umma wa Kiislamu. Na kinyume chake pia kuna matukio mengi ambayo yameonyesha ni kwa kiwango gani kuyapuuza malengo matukufu ya ukombozi wa Quds tukufu na badala yake kuchukua msimamo wa mapatano na maridhiano na utawala haramu wa Israel kumeshadidisha hitilafu na tofauti baina ya nchi za Kiislamu na matokeo yake kuwadhoofisha Waislamu wenyewe.

Kongamano la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran, Iran

 

Katika uhakiki na uchambuzi wa kisiasa, moja ya mambo yanayosababisha kupatikana umoja na mshikamano wa ndani katika nchi mbalimbali ni kuwepo kwa “adui”. Kwa maneno mengine ni kwamba, ile nguvu ya kiadui itokayo upande wa nje wa ajinabi, ambayo kwa mtazamo wa matapo tofauti ya kiutamaduni na kisiasa ya ndani ya nchi inatafsiriwa kuwa ni “adui wa pamoja” wa matapo yote hayo huwa ndiyo inayokuwa sababu na chachu ya kupatikana mshikamano ndani ya nchi hasa pale adui huyo anapotonesha vitu vinavyoyagusa na kuyaunganisha pamoja matapo na makundi tofauti ya taifa fulani na kuyafanya yajihisi kuwa na utambulisho mmoja wa pamoja. Kutokana na kuwa na uelewa wa jambo hilo, na ili kuleta umoja na mshikamano ndani ya mataifa yao, viongozi wa nchi nyingi huamua “kujibunia adui” na kumtumia kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Kuwachochea majirani zao waanzishe uhasama na vita ni moja ya mbinu zinazotumiwa na viongozi wa nchi zinazokabiliwa na hatari ya mfarakano. Kwa kutaka waondokane na shari ya wapinzani na kuepusha mfarakano kati ya matapo tofauti ya ndani, viongozi hao huanzisha chokochoko dhidi ya majirani zao ili kutokana na jibu hasi watakalotoa waweze kuwasha cheche ya mjadala ndani ya nchi zao wa kuanzisha au kuhuisha utambulisho mmoja utakaoleta umoja baina ya wananchi wote.

Wapenzi wasikilizaji, ningependa niitolee ufafanuzi zaidi nukta hii, lakini muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena inshallah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 48 ya mfululizo huu.

Tags