Apr 28, 2018 17:56 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (51)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 51.

Kwa wale wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika vipindi viwili vilivyopita tulizungumzia lengo tukufu la kuikomboa Palestina na Quds tukufu kama tunu tukufu ya pamoja ya nchi za Kiislamu, lengo ambalo tulisema linatoa fursa nyingi za kuwezesha kufikiwa ndoto ya umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Kipindi chetu cha leo kitazungumzia mhimili wa uchumi ambao ni wa kuanzisha soko la pamoja la nchi za Kiislamu kama nukta ya kuunganisha Ulimwengu wa Kiislamu na kujaribu kufanya upembuzi na uchambuzi ili kuona kuanzishwa kwa soko la aina hiyo kunaweza kwa kiasi gani kutatua matatizo ya kiuchumi ya Waislamu na kuziimarisha nchi za Kiislamu ili kuwa na kambi moja imara na athirifu ya kiuchumi katika zama hizi za miungano ya kieneo.

Katika chambuzi mbalimbali tulizofanya kuhusiana na sababu za kuwepo mfarakano na mgawanyiko kati ya nchi za Kiislamu tumeeleza kwamba udhaifu wa imani na ushawishi na wasiwasi wa shetani umewafanya watu wajitenge na kujiweka mbali na thamani na mafundisho ya dini. Lakini nukta ambayo inapasa kuzingatiwa na kujiuliza, ni kwa nini licha ya Waislamu wote kuwa na itikadi ya moyoni ya Mungu mmoja, Mtume mmoja na Kitabu kimoja cha Qur'ani, wasiwasi wa shetani unaendelea kuathiri nafsi zao na kudhoofisha imani zao kwa thamani hizo za kiwahyi? Pengine tunaweza kusema kwamba moja ya sababu kuu za kuwa mbali Waislamu na thamani hizo ni umasikini na ukata wa kiuchumi. Imam Ali (AS) amesema katika hadithi yenye mazingatio makubwa kwamba wakati ufakiri unapoingia ndani ya nyumba kupitia mlangoni, imani hutoweka kupitia dirishani. Hadithi hii inabainisha taathira haribifu za ufukara na ukata wa kiuchumi kwa imani ya dini ya mtu. Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa ufakiri unaoshuhudiwa katika nchi za Kiislamu ni moja ya sababu zinazodhoofisha imani za Waislamu na kuwafanya wajitenge na kujiweka mbali na thamani za mafundisho ya kiwahyi ya dini yao.

 

Lakini mbali na hayo, udhaifu na hali mbaya hiyo ya kiuchumi imewafanya watawala wa nchi hizo za Kiislamu wakubali kuburuzwa na kutiwa shemere na madola ajinabi. Historia imeonyesha kuwa ili kuziba mapengo ya hali zao mbaya za uchumi, nchi nyingi zenye hali hiyo huamua kujiegemeza na kujikumbatisha kwa madola yaliyoendelea na yenye hali bora ya ustawi wa jamii. Na tab'an, wakati nchi moja inapokuwa tegemezi kiuchumi kwa nyingine, nchi hiyo bila shaka itakuwa chini ya udhibiti wa kiutamaduni na kisiasa pia wa nchi inayoitegemea; na hiyo inaweza kuwa nukta kuu ya sababu za mifarakano katika nchi za Kiislamu. Kwa masikitiko, leo hii nchi za Kiislamu, ambazo zina suhula nyingi zaidi za kimaada na rasilimaliwatu pamoja na utajiri mkubwa wa maliasili, zinakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kiuchumi. Licha ya nchi hizo kuwa na hazina kubwa ya akiba ya mafuta na gesi iliyoko duniani ambayo kwa hakika ndiyo injini ya kusukumia gurudumu la uchumi wa dunia, na pamoja na nchi hizo kuchangia fungu kubwa zaidi la mazao ya kilimo ikiwa ni pamoja na ngano, mpunga, pamba na malighafi za viwandani, haziko katika nafasi nzuri kiuchumi duniani huku utajiri na matunda ya juhudi zao za kiuchumi vikinyonywa na kuporwa na madola yenye nguvu hususan nchi za Magharibi.

Nchi za Kiislamu ambazo kijiografia ziko kwenye eneo la nyuzi 20 upande wa magharibi, nyuzi 140 upande wa mashariki, nyuzi 10 upande wa kusini na nyuzi 50 upande wa kaskazini mwa mstari wa Ikweta, zina uwezo mkubwa kutokana na kumiliki hazina kubwa ya nishati ya fosili, madini, mazao ya kilimo na bidhaa za viwanda zenye mfungamano na mazao hayo. Zaidi ya theluthi moja ya akiba ya mafuta na karibu asilimia sabini ya akiba ya gesi iliyoko duniani zinapatikana katika nchi za Kiislamu. Vilevile asilimia 40 ya akiba ya madini ya fosfati, asilimia 38 ya bati, asilimia 15 ya madini ya urani na asilimia 12 ya akiba ya kromu iliyoko duniani ni milki ya mataifa ya Waislamu. Si hayo tu, lakini pia aina nyinginezo za madini kama mawe ya madini, makaa ya mawe, shaba, risasi, zinki, ulanga, potasiamu, kobalti na anuani mbalimbali za mawe ya ujenzi zinapatikana kwa wingi kwenye ardhi za nchi za Kiislamu. Kwa upande wa sekta ya kilimo pia kiwango kikubwa zaidi cha mazao ya pamba, tende, zabibu, mpunga, katani na ngano inalimwa na kuzalishwa katika nchi hizo. Lakini licha ya kuwepo suhula na utajiri wote huo katika nchi za Kiislamu, kiwango cha uchumi cha aghalabu ya nchi hizo ni cha chini mno huku maisha ya akthari ya watu wake yakiwa yamegubikwa na wingu zito la ukata na ufakiri.

 

Hii ni katika hali ambayo madola mengi yenye nguvu duniani yamekuwa yakipora fungu kubwa la utajiri huo wa maliasili za nchi za Kiislamu; na kuwa na satua pia ndani ya nchi hizo ya kisiasa na kiutamaduni. Lakini nchi za Kiislamu zenyewe, badala ya kutumia uwezo zilionao na kushirikiana pamoja katika kuzitumia ipasavyo fursa na suhula zao za kiuchumi, zinatumia muda wao mwingi kwa ugomvi na mizozo baina yao huku zikifadhilisha kuzikumbatia na kushirikiana nazo nchi za Magharibi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi kwa ajili ya kujinufaisha na kufikia malengo ya kupita tu ya kisiasa na kiuchumi badala ya kushirikiana na kusaidiana wao kwa wao. Ushirikiano na muelekeo wa pamoja katika Ulimwengu wa Kiislamu katika sekta ya uchumi na kuzitumia kwa manufaa ya wote suhula na uwezo uliopo wa kiuchumi kutaziletea nchi hizo matunda mengi yakiwemo yafuatayo: kwanza ni kujinasua nchi hizo na makucha na minyororo ya ubeberu wa kiuchumi wa kambi za kiuchumi na kisiasa za madola yenye nguvu duniani na kuweza kuwa huru na kujitawala kisiasa na kiuchumi. Pili ni kuweza kutumia uwezo na fursa zilizoko katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kufikia ustawi wa pande zote. Tatu ni kuweza nchi za Kiislamu kuwa na sauti katika uga wa kisiasa na kiuchumi kieneo na kimataifa. Nne ni kuweza kupatikana uthabiti na usalama wa kisiasa na kiuchumi ndani ya nchi za Kiislamu. Tano ni kuweza kupunguza matatizo ya kiutamaduni na kijamii yanayosababishwa na masaibu ya kiuchumi, kama vile matatizo ya ukosefu wa ajira na uraibu wa madawa ya kulevya. Na hatimaye kutoa muelekeo kwa mwenendo na mfumo wa Utandawazi katika nyuga tofauti hususan katika uga wa kiuchumi.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Kiislamu unaozingatia manufaa na maslahi ya pamoja unaweza kutoa mwanga zaidi wa kupatikana muelekeo na sauti moja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Wasikilizaji wapenzi, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umemalizika, hivyo sina budi kuishia hapa huku nikitumai kuwa mumeelimika na kunufaika na yote mliyoyasikia katika mfululizo huu. Tutakutana tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo, katika sehemu ya 52 ya kipinid hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags