Apr 28, 2018 17:58 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (52)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 52.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki, bila shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulizungumzia fikra ya kuanzisha soko la pamoja la kiuchumi kama moja ya nukta za kuuunganisha pamoja Ulimwengu wa Kiislamu. Tulieleza kwamba, licha ya kuwepo suhula na utajiri mkubwa wa maliasili za madini na mazao ya kilimo katika nchi za Kiislamu, kiwango cha uchumi cha aghalabu ya nchi hizo ni cha chini mno huku maisha ya akthari ya watu wake yakiwa yamegubikwa na wingu zito la ukata na ufakiri. Aidha tukabainisha kuwa ushirikiano na muelekeo wa pamoja katika Ulimwengu wa Kiislamu katika sekta ya uchumi na kuzitumia kwa manufaa ya wote suhula na uwezo uliopo wa kiuchumi kutaziletea nchi hizo matunda mengi ikiwemo kujinasua na makucha na minyororo ya ubeberu wa kiuchumi wa kambi za kiuchumi na kisiasa za madola yenye nguvu duniani na kuweza kuwa huru na kujitawala kisiasa na kiuchumi.

Ukweli ni kwamba licha ya kushuhudiwa kwa uwazi kabisa mwenendo wa uchumi wa dunia kuelekea kwenye mfumo wa Soko Huria na kuondolewa mipaka ya ndani na vizuizi vya ushuru wa forodha, hatuwezi kupuuza pia hamu iliyojitokeza ya kuanzisha ushirikiano wa pamoja wa uchumi wa kikanda katika maeneo mbalimbali ya dunia. Hamu hiyo ambayo ni matokeo ya ushindani mkali wa kiuchumi na kisiasa uliopo kwenye upeo wa kimataifa huwa aghalabu inaonyeshwa na nchi ambazo kwa kiwango fulani zina hali zinazofanana katika muundo wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamduni na kukaribiana kijiografia pamoja na kuwa na maslahi yanayolingana kwa pande zote mbili. Soko la pamoja la Kiislamu ni moja ya vielelezo vya ushirikiano huo. Kuanzisha soko la pamoja la Kiislamu ni jambo lenye udharura katika mazingira ya sasa ya uchumi wa dunia pamoja na mageuzi na mabadiliko yanayohusiana na hali ya uchumi huo kama vile kubadilika muundo wa biashara ya dunia na kugawana majukumu nchi za Kiislamu. Sababu ni kwamba hali ya uchumi wa dunia na mabadiliko yanayotokea ndani yake hayalengi kukidhi maslahi na manufaa ya kiuchumi ya nchi zinazoendelea zikiwemo nchi za Kiislamu.

Qur'ani, Kitabu Kitakatifu kinachowaunganisha Waislamu

 

Moja ya malengo muhimu zaidi ya kila nchi ya kujiunga na kambi maalumu za kiuchumi ni kuweza kunufaika nayo kwa ajili ya kufikia kiwango cha juu cha ustawi na maendeleo. Lengo hili peke yake linaweza kuwashawishi viongozi wa nchi mbalimbali kujiunga na jumuiya za kiuchumi za kikanda. Lakini mbali na hayo, suala kwamba ushirikiano ni jambo lenye faida kiuchumi, bali hata lisiloweza kuepukika, ni fikra ambayo imezidi kupata nguvu miongoni mwa nchi zinazoendelea. Sababu hizo pamoja na kuvunjwa moyo na kukatishwa tamaa jamii zenye kiwango cha chini cha ustawi na wapangaji sera za uchumi wa dunia na uchumi wa kimataifa kumezihamasisha nchi nyingi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kujiunga kwa malengo tofauti na kambi za kiuchumi za kikanda na kieneo. Matokeo ya kujiunga na jumuiya hizo za kiuchumi yamekuwa ni kupata tajiriba na uzoefu mkubwa nchi za Kiislamu katika suala la kuanzisha ushirikiano wa kikanda. Hata hivyo licha ya kupata tajiriba na uzoefu wote huo na pamoja na nchi za Kiislamu kuelewa udharura wa kuwa na kauli moja juu ya suala la kuanzisha ushirikiano wa kieneo hususan kuasisi soko la pamoja la Kiislamu, tukichunguza mwenendo wa mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi za Kiislamu tutabaini kuwa kiwango cha mahusiano ya kiuchumi kati ya nchi hizo ni cha chini mno.

Kwa kutoa mfano, katika usafirishaji bidhaa nje uliofanywa na nchi za Kiislamu katika mwaka 1997 wa kiwango cha jumla ya dola bilioni 416.6, ni asilimia tisa tu ya kiwango hicho, yaani dola bilioni 38.5 ilihusisha mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi zenyewe za Kiislamu, huku asilimia yote 91 iliyosalia ya usafirishaji wa bidhaa ikielekezwa kwenye masoko ya nje ya eneo la nchi hizo. Vilevile katika sekta ya biashara ya bidhaa za chakula; kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), katika mwaka 1989, kiwango cha biashara ya bidhaa za chakula kati ya nchi za Kiislamu kilikuwa ni dola bilioni 3.3 tu, yaani asilimia 11 ya mahitaji yote ya bidhaa za chakula ya nchi hizo. Na sababu ni kuwa kiwango kikubwa zaidi cha bidhaa za chakula zinazohitajiwa na nchi za Kiislamu kinaagizwa kutoka nchi zisizo za Kiislamu. Katika kipindi hicho sehemu kubwa ya mahitaji hata ya nafaka pia kama ngano, mchele, shayiri na mtama iliagizwa kutoka nchi kama Marekani, Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya, Australia, Canada, Thailand na Argentina. Takwimu zinaonyesha kuwa, hali hiyo imeendelea kushuhudiwa pia katika muongo mmoja hadi miwili ya hivi karibuni.

Bwana Mtume Muhammad SAW ni kiungo muhimu mno cha Waislamu wote duniani

 

Tajiriba ya umoja na ushirikiano wa kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya dunia na vilevile historia ya mivutano na mashindano yasiyo na tija kati ya nchi za Kiislamu zinaonyesha kuwa kuthibiti kwa ndoto ya kuasisi soko la pamoja la Kiislamu kunakabiliwa na vizuizi na matatizo mengi, lakini bila shaka yoyote inatupasa pia tuseme kuwa, ili kuweza kuwa na umoja, nchi za Kiislamu hazina budi kuwa na sauti na muelekeo wa pamoja wa kiuchumi; kwa sababu kuongeza kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi na kuwa na chombo kimoja cha kudhamini manufaa na maslahi ya pamoja ya kiuchumi ni moja ya masuala yenye taathira katika kustawisha ushirikiano wa kisiasa na kiutamaduni wa nchi hizo. Ili kuweza kuasisi na kuendeleza soko la pamoja la Kiislamu, kuna ulazima kwa nchi zote za Kiislamu kufaidika na manufaa yanayopatikana kwenye soko hilo na kuwa na hamu na utashi wa pamoja wa kiuchumi na kisiasa. Katika muktadha huo inapasa tuseme kuwa kuunda soko la pamoja kunaathiriwa na kuchochewa na hamu na utashi wa pamoja wa kisiasa katika Ulimwengu wa Kiislamu, na kwenyewe pia kuna taathira ya kushadidisha mshikamano au utengano wa kisiasa baina ya nchi za ulimwengu huo. Kwa maneno mengine ni sawa na kusema kwamba, manufaa na maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya Ulimwengu wa Kiislamu ni mithili ya vikufu vya mnyororo vilivyoshikana pamoja, ambapo uimara wa kikufu kimoja unaathiri uimara wa vikufu vingine vilivyosalia.

Wapenzi waskilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa leo umemalizika. Hivyo sina budi kukomea hapa nikitumai kuwa mumenufaika kwa yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Katika sehemu ijayo ya 53 ya mfululizo huu inshallah tutakuja kuizungumzia Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambayo ni moja ya tajiriba ya kivitendo ya kuwepo sauti moja na muelekeo mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na kujaribu kuchambua na kuhakiki kasoro na mapungufu ya taasisi hiyo katika kufikiwa lengo hilo. Basi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani.

Tags