Apr 28, 2018 18:03 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (54)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 54.

Bila shaka wapenzi wasikilizaji wa kipindi hiki mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulianza kuzungumzia ile iliyokuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC ambayo nayo pia tumeitaja kama ni moja ya nembo na vielelezo vya kuwepo sauti moja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tukaeleza kwamba mbali na sababu nyenginezo, kitu ambacho kilikuwa chachu ya kuasisiwa Jumuiya ya OIC ni tukio la kuchomwa moto msikiti mtukufu wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu lililotokea mwaka 1969. Pamoja na mambo mengine tukabainisha kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu iliasisiwa rasmi katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama uliofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia tarehe 24 Machi mwaka 1972 ambapo hati rasmi ya jumuiya hiyo ilipitishwa.

Hati iliyopitishwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu iliainisha malengo yafuatayo kama dira kuu ya kufuatwa na nchi wanachama: Mosi, kuongeza kiwango cha mshikamano wa Kiislamu baina ya nchi wanachama. Pili, kuunga mkono ushirikiano kati ya nchi wanachama katika nyuga za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kielimu na nyuga nyingine muhimu na kufanya mashauriano na nchi wanachama wa jumuiya zingine za kimataifa. Tatu, kufanya juhudi za kutokomeza ubaguzi wa rangi na kimbari pamoja na ukoloni wa aina tofauti. Nne, kuchukua hatua zinazotakiwa kwa ajili ya kuunga mkono na kutoa msukumo wa kupatikana amani na utulivu katika uga wa kimataifa kwa msingi wa uadilifu. Tano, kuwa na uratibu na mashauriano katika harakati na hatua zinazochukuliwa na nchi wanachama kwa ajili ya kudumisha utulivu na amani katika maeneo matakatifu, kusaidia juhudi za kuyakomboa, kuunga mkono mapambano ya taifa la Palestina na kulisaidia taifa hilo ili kuhakikisha linarejeshewa haki zake na kuzikomboa ardhi zake. Sita, kuunga mkono mapambano ya mataifa yote ya Waislamu kwa ajili ya kulinda heshima, kujitawala na haki zao za kitaifa. Na saba, kuandaa mazingira mwafaka ili kuongeza kiwango cha maelewano kati ya nchi wanachama na nchi nyingine duniani.

 

Mbali na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) kuyakubali malengo hayo saba tuliyoyataja, ziliafikiana pia kuifanyia kazi misingi mitano ifuatayo kama dira na mwongozo utakaofanikisha utekelezaji wa malengo hayo saba. Msingi wa kwanza ni wa kuwepo usawa baina ya nchi zote wanachama wa OIC. Maana ya usawa huo ni kutokuwepo upendeleo na ubaguzi wa kisiasa na kiuchumi kati ya nchi wanachama ambapo utekelezaji wake kivitendo utathibiti katika suala la upigaji kura. Msingi wa pili ni kwamba, nchi zote wanachama zinapaswa kuheshimu msingi wa uhuru wa watu kujiamulia wenyewe mustakabali wao na kwa hivyo kujiepusha na kuingiliana katika masuala yao ya ndani. Msingi wa tatu ni kwamba kila nchi mwanachama iheshimu mamlaka ya kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi yote ya mwanachama mwingine. Msingi wa nne ni kuhakikisha zitokeapo tofauti au mzozote wowote ule kati ya nchi wanachama zitumike njia za amani kama mazungumzo au usuluhishi au upitishaji maamuzi ya hukumu ili kutatua mzozo huo. Na msingi wa tano ni kwamba, haifai wala haipasi kwa nchi yoyote mwanachama kutumia mabavu au vitisho dhidi ya umoja na mamlaka ya ardhi yote au kujitawala kisiasa kwa nchi nyingine mwanachama. Maana ya msingi huu ni kwamba, nchi wanachama wa OIC zinaunda jumuiya hiyo kwa madhumuni ya kuwa na umoja na mshikamano ili kukabiliana na nchi nyingine hususan nchi zisizo za Kiislamu; ndiyo kusema kwamba, kufanya hivyo kunatoa hakikisho kwa viongozi wa nchi wanachama kwamba, nguvu zinazotokana na umoja na mshikamano huo hazitatumika katu dhidi ya nchi yoyote ile mwanachama.

Kwa hivyo Jumuiya ya Nchi za Kiislamu inayojulikana hivi sasa kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu iliasisiwa rasmi kwa lengo kuu la kuleta umoja na kuunganisha Ulimwengu wa Kiislamu. Ili kuweza kuyafikia malengo iliyojiwekea na kutekeleza majukumu na mamlaka iliyojipangia, Jumuiya ya OIC inafanya kazi na kupitisha maamuzi kwa kufuata misingi minne ya kimuundo ambayo ni mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama, unaojulikana kama mhimili wa juu kabisa wa jumuiya hiyo; mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama; Sekretarieti ya OIC na Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu wa Kiislamu, ambayo imeshindikana kuundwa hadi sasa kwa sababu ya kutopitishwa hati yake na nchi wanachama. Lakini mbali na mihimili hiyo minne, kuna vyombo vingine kadhaa pamoja na kamati ndogo ndogo katika muundo wa Jumuiya ya OIC. Kamati hizo ni za kudumu na zinafanya kazi ya kushughulikia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya muawana, masuala ya kiutamaduni, upashaji habari n.k. Mkutano wa viongozi wakuu wa nchi wanachama hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitatu katika mji mkuu wa moja ya nchi wanachama.

Kongamano la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran

 

Nchi inayokuwa mwenyeji wa mkutano huo huwa ndiyo mwenyekiti wa mzunguko wa OIC kwa muda wa miaka mitatu. Hadi sasa imeshafanyika mikutano 13 ya aina hiyo ya viongozi wakuu wa nchi wanachama, ambapo mkutano wa mwisho kabisa ulifanyika Aprili 14 hadi 15 mwaka 2016 katika mji wa Istanbul, Uturuki. Mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ndicho chombo cha juu kabisa cha OIC ambacho kina jukumu la kumchagua Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo.

Lakini kama tulivyotangulia kueleza, kuna vyombo na asasi kadhaa zilizo chini ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ikiwa ni pamoja na Kituo cha Kiislamu cha Ustawi wa Biashara, Kituo cha Utafiti wa Historia ya Sanaa na Utamaduni wa Kiislamu, Baraza la Fiqhi ya Kiislamu, Mfuko wa Mshikamano wa Kiislamu, Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IDB), Shirika la Kiislamu la Elimu, Sayansi na Utamaduni (ISESCO), Jukwaa la Kimataifa la Biashara la Kiislamu (WIEF), Shirikisho la Michezo la Mashindano ya Mshikamano wa Kiislamu, Shirika la Miji na Miji Mikuu ya Kiislamu, Jukwaa la Mkutano wa Vijana wa Kiislamu kwa ajili ya Mazungumzo na Ushirikiano (ICYF-DC) na Baraza Kuu kwa ajili ya Benki na Taasisi za Fedha za Kiislamu (CIBAFI).

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo, sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Katika kipindi chetu kijacho, inshaallah tutakuja kuzungumzia hatua muhimu zaidi zilizochukuliwa na OIC ili kuhakikisha nchi za Kiislamu zinakuwa na muelekeo mmoja na sauti moja; na kwa kuzingatia malengo, majukumu na hatua zilizochukuliwa hadi sasa tutachambua kasoro na upungufu ambao umesababisha kutotekelezwa ipasavyo na kutofikiwa kikamilifu malengo yaliyokusudiwa. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags