Sep 09, 2018 14:23 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya nne ya kipindi hiki kipya cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa kwa mujibu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw), wanadamu wote na kwa tofauti zao za rangi, lugha, kaumu na kabila, wako sawa na wanadamu wengine na hakuna mtu mwenye ubora juu ya mwingine ispokuwa tu kwa uchaji-Mungu. Aidha kwa mujibu wa Mtume huyo wa Uislamu, wanadamu wote wako sawa katika uumbaji na natija yake ni kwamba, kuanzia uhuru na hiari wako sawa kwa ajili ya kuainisha mustakbali wao. Leo pia tutazungumzia suala la uadilifu katika jamii, karibuni.

Ndugu wasikilizaji, Imamu Khomein (MA) na kwa kutegemea mwenendo huo hususan katika kufuata nyayo za kipindi cha utawala wa Imamu Ali Bin Ali Twalib (as) hakuutambua tu uadilifu kuwa ni fadhila ya mtu mmojammoja, bali aliamini kwamba uadilifu na usawa ni kati ya mambo yanayohitajika kwa jamii ya Kiislamu. Katika fukra ya Imamu huyo, uadilifu wa kijamii, ni jambo lenye umuhimu na lililo wazi kwa mfumo wa kisiasa na kijamii na pia kwa roho inayotawala shughuli za makundi na asasi za kisiasa na kijamii, na muhimu zaidi kwenye matukufu ya kijamii. Kwa msingi wa fikra hiyo, Imamu Khomeini alitambua kuwa lengo la mwisho la utawala wa kidini, ni kufikiwa uadilifu wa kijamii kwa mujibu wa vigezo vya Uislamu. Ili kufikiwa matukufu ya dhati ya uadilifu aliamini kwamba, sheria zote zikiwemo za kibinaadamu, ni lazima zijengeke juu ya misingi ya uadilifu, kwa kuwa falsafa ya kuweka sheria hizo, ni kufikiwa usawa. Katika kubainisha suala hilo, aliandika katika kitabu cha ‘al-Baiu’ yaani mauzo kwamba: “Hukumu za kisheria, sheria za Kiislamu na masuala ya utawala, yote ni nyenzo kwa ajili ya kutekeleza utawala na kueneza uadilifu.” Mwisho wa kunukuu.

**********

Katika fikra ya Imamu Khomeini (MA) lengo kuu la ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni kufikiwa uadilifu katika uga wa mtu mmojammoja na kijamii, kuhusiana na hilo anasema: “Juhudi zote za Mitume ilikuwa ni kuhakikisha wanaunda uadilifu wa kijamii kwa ajili ya mwanadamu mmojammoja na jamii nzima.” Mwisho wa kunukuu. Kwa mujibu wa fikra hiyo, msingi wa kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuunda uadilifu na usawa wa kijamii na kuondoa dhulma. Imamu anasema: “Katika Jamhuri ya Kiislamu, hakuna dhulma na utumiaji mabavu…..masikini wataboreshewa hali zao na kuzingatiwa haki zao….Uadilifu wa ki-Mungu utaenea juu ya jamii yote.” Mwisho wa kunukuu. Kadhalika katika kitabu cha Sahifat n-Nur, juzu ya 6 ukurasa wa 525 Imamu Khomein amefafanua nadharia ya uadilifu kwa namna tofauti kuhusiana na maisha ya mtu binafsi na jamii na kwamba jambo hilo (uadilifu) ni lenye kukamilisha mambo mengine. Kwa mtazamo wake, kufikiwa uadilifu wa kijamii kunahitajia kwanza kupatikana angalau kwa kiasi kidogo, uadilifu wa mtu binafsi na kwamba mambo hayo mawili ni yenye kuhitajiana. Hii ni kwa kuwa uadilifu wa mtu binafsi unaandaa uadilifu wa kijamii na pia uadilifu wa kijamii ndio sababu ya kupatikana kwa uadilifu wa mtu binfasi.

***********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu nne ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Imamu Khomein anatambua kwamba, kufikiwa usawa wa kijamii kunahitajia kuwepo kiongozi mwadilifu na kama ambavyo anaamini pia kwamba, katika kipindi cha ghaibah ya Imamu Mahdi ambaye atasimamisha uadilifu kamili, wadhifa wa kufanikisha jambo hilo (uadilifu) unategemea faqihi mwadilifu. Katika kitabu cha Wilaayatul-Faqihi amefafanua na kubainisha kwamba katika kipindi cha ghaibah, suala la kufanikisha uadilifu katika jamii lipo kwa faqihi aliyekamilisha masharti. Sambamba na kulaani tawala zilizojengeka juu ya mabavu na dhulma na pia kuhimiza juu ya kuendesha mapambano kwa ajili ya kuzing’oa tawala hizo ovu, aliliona jambo hilo kuwa ni wadhifa wa kila Mwislamu. Aidha aliamini kwamba bila kufikiwa utawala wa kidini ambao kiongozi wake atakuwa faqihi mwadilifu, ni vigumu sana kuweza kufikiwa uadilifu wa kijamii.

***********

Baada ya hayo sasa tuelekeze macho yetu kwenye nukta nyingine ambayo ilisisitizwa sana na Imamu Khomeini (MA) nayo ni uadilifu wa kiuchumi. Ndugu wasikilizaji uadilifu wa kiuchumi kwa namna kamili unagawanyika katika pande mbili kuu, nazo ni uadilifu wa uzalishaji na uadilifu wa ugawaji. Uadilifu wa uzalishaji umejengeka juu ya mtazamo wa uwekezaji kwenye uga wa kiuchumi na ukiwa na maana hii kwamba, kila raia wa jamii husika anayo fursa sawa katika uga wa kuzalisha uchumi ili kwa njia hiyo uzalishaji zaidi upatikane na kusukuma mbele gurudmu la ustawi na maendeleo na hivyo kutokomeza umasikini katika jamii. Ama usawa wa ugawaji, na kwa mtazamo wa kijamii, una maana ya uchumi wenye kuamini kwamba utajiri wa jamii ni lazima ugawanywe kwa usawa kati ya watu wote wa jamii husika ambapo matajiri na wenye nacho watatakiwa kulipia kodi ambayo baadaye huwarudia tena wananchi masikini. Hata hivyo upo mtazamo wa tatu ambao  unajaribu kuzionganisha nadharia hizo zilizotangulia ambayo nayo inaitwa uadilifu jumla. Kwa mtazamo wa Imamu Khomeini (MA) uadilifu wa kiuchumi, umejengeka juu ya nadharia ya tatu ambayo ni uadilifu jumla. Katika mtazamo huo watu wote wa jamii huwa wana fursa kwa ajili ya usawa wa kiuchumi, ili angalau kwa uchache watu wote wa jamii husika waweze kudhaminiwa kupewa maisha bora na matukufu kupitia uchumi huo.

*********

Kudhamini kwa uchache maisha bora na yenye utukufu kupitia uchumi, kuna maana ya jamii kuiahidi serikali kwa ajili ya kuwaunga mkono watu masikini na wanyonge kwa kuwa moja ya misingi ya kuundwa serikali hiyo, ni kudhamini usalama wa kijamii na kufanya maisha bora kwa ajili ya watu katika Nyanja zote. Iwapo katika jamii, kwa akali maisha ya watu wote yanaboreshwa na kuwafanya raia wasiwe na daghadagha ya kimaisha, basi kutaandaliwa uwanja kwa ajili ya kuchanua ua la maisha bora kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii hususan katika uga wa kiuchumi ambapo pia hata uadilifu wa uzalishaji nao utaweza kupata maana yake halisi. Imamu Khomeini na kwa kufahamu nukta hiyo, kudhaminiwa ustawi wa umma yalikuwa ni malengo ya serikali ya jamhuri ya Kiislamu na kuhusiana na hilo anasema: “Matukufu yote na matarajio ya taifa na serikali pamoja na viongozi wa nchi yetu ni kwamba ifikie siku ambayo masikini na ombaomba katika jamii havitokuwa tena na nafasi, na wananchi watukufu, wenye subira na wenye ghera wa Iran waweze kupata ustawi bora wa maisha ya kimada na kimaanawi.” Mwisho wa kunukuu.

*********

Kadhalika Imamu Khomeini (MA) aliutaja ufuatiliaji endelevu wa masuala ya watu masikini na madhaifu katika jamii kuwa ni lazima utapelekea kufikiwa uadilifu wa kijamii ambapo aliwataka viongozi wa serikali ya Jamhuiri ya Kiislamu kuwa na daghadagha kubwa kwenye kufuatilia maisha ya watu masikini na wale wanaoishi vijijini kwa kusema: “Ni lazima kufanywe juhudi kubwa kwa ajili ya kutokomeza umasikini…hususan kwa ajili ya watu hawa wa vijiji wasio jiweza, ni lazima wafikiriwe. Serikali inawahusu watu wote, na ni lazima ifanye kazi kwa ajili ya wote, lakini kwa watu wanyonge inatakiwa ifanye juhudi zaidi ili iwafikishe kwenye tabaka la juu.” Mwisho wa kunukuu. Kadhalika mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa mwito kwa viongozi wa kidini (mubalighina) ambao hufanya safari kwenda katika maeneo tofauti ya Iran, kufanya juhudi katika kuwasaidia watu masikini wakati wa kufikisha kwao neno la Mwenyezi Mungu kati yao, kwani kuwazingatia watu hao hupelekea kupatikana uadilifu wa kijamii. Imamu Khomeini anasema: “Kile ambacho watu wa kiroho hawapaswi kukiacha na hawatakiwi kukitenga mbali na shughuli yao, ni kuwaunga mkono watu masikini na wasio kuwa nacho. Kwa kuwa kila mtu atakayekwenda nalo kinyume jambo hilo, basi atakuwa ameenda mbali na uadilifu wa jamii ya Kiislamu.” Mwisho wa kunukuu.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya nne ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.  

Tags