Sep 12, 2018 04:37 UTC
  • Jumatano tarehe 12 Septemba 2018

Leo ni Jumatano tarehe Pili Muharram mwaka 1440 Hijria sawa na Septemba 12, 2018.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria Imam Hussein AS mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia yake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo. Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya. Jeshi la Yazidi mlaaniwa liliuzuia msafara wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kuingia katika mji wa Kufa na kuzingirwa katika jangwa na Karbala. 

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita yaani 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa fizikia na kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris. Baba na mama yake walikuwa wasomi mahiri katika fizikia. Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mionzi ya nururishi au radioactive.

Irene Joliot- Curie

Tarehe 12 Septemba 1944, wawakilishi wa Marekani, Uingereza na Urusi walitia saini makubaliano ya kuikalia kwa mabavu Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Utawala wa Kinazi wa Ujerumani ulisambaratishwa kikamilifu mwezi Mei 1945, na kudhibitiwa kikamilifu mji wa Berlin baada ya kutokea mashambulizi yaliyofanywa na majeshi ya waitifaki wa Magharibi na Mashariki. Hatimaye mwaka 1949 nchi hiyo ilizidi kutumbukia kwenye mkwamo baada ya kugawanyika nchi mbili za Ujerumani ya Magharibi na Mashariki.

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, nchini Ethiopia kulitokea mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Haile Sellasie. Haile Selassie alizaliwa mwaka 1892 nchini Ethiopia. Awali alikuwa mkuu wa mikoa kadhaa nchini humo na kisha baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1930 alishika hatamu za uongozi wa Ethiopia akiwa mfalme wa nchi hiyo. Awali alifanya jitihada kubwa za kuyaunganisha makabila ya Ethiopia ili ayafanye yawe chini ya utawala wake. Haile Selassie aliwaahjiri wataalamu wa kigeni na kuanza kufanya mabadiliko ya kiofisi hatua kwa hatua. Hata hivyo mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia mwaka 1953 yalisitisha mpango wake huo.

Haile Sellasie

Tarehe 12 Septemba 1977, alifariki dunia Steve Biko mwanaharakati wa kupigania haki za wazalendo wa Afrika Kusini, akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Steve Biko alikuwa kiongozi wa wanafunzi aliyefanya jitihada kubwa za kuwawezesha wazalendo waliokuwa wakibaguliwa wa Afrika Kusini na kuratibu harakati zao. Baada ya kuuawa na polisi, Biko alitambuliwa kuwa shahidi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Alikuwa mashuhuri kwa kaulimbiu ya "Weusi ni Uzuri" (black is beautiful) ambayo ililenga kuwapa moyo wazalendo wa Afrika Kusini waliokuwa wakibaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.

Steve Biko

 

Tags