Ruwaza Njema (2)
(Kumfuata al-Mustafa (saw) mwenye huruma na rafiki wa watu)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na karibuni kusikiliza sehemu ya pili ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema, ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutoka mjini Tehran. Katika kupindi che leo tutazungumzia sifa ya huruma na urafiki ya Mtume wetu Mpendwa Muhammad al-Mustafa (saw), hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi.
*********
Wapenzi wasikilizaji, moja ya sifa nzuri na za kuvutia ambazo Mwenyezi Mungu amemsifu kwazo Nabii na Mtume wake mpendwa (saw) ni sifa ya upole na huruma ambapo anasema katika Aya 128 ya Surat at-Tauba: Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayokutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.
Salamu za Mwenyi Mungu zimuendee Bwana huyo wa walio na maadili na akhlaqi njema inayomridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu.
************
Wapenzi wasikilizaji, na tunasoma katika kitabu cha Tahdhib al-Ahkam cha Sheikh Tousi, mfano huu wa kupendeza wa sifa njema ya upole na huruma ya Bwana Mtume kwa watoto, huku akiwa amezama kwenye ibada na swala kwa ajili ya Mola wake, swala ambayo alikuwa akiipenda sana. Kuhusu suala hili, Maulana al-Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) anasema: 'Mtume (saw) aliswalisha watu swala ya Adhuhuri na kuharakisha katika rakaa mbili za mwisho. Alipomaliza watu walimuuliza: Je, kumetokea jambo miongoni mwa watu? Mtume akauliza: Kwa nini? Wakasema: Umeharakisha kwenye rakaa mbili za mwisho (ya tatu na nne)! Akawaambia (saw): Kwani hamkusikia mtoto akilia?'

Wapenzi wasikilizaji, moja ya sifa bora na za kipekee alizosifika nazo Mtume Mtukufu (saw), kati ya Mitume wengine wote wa Mwenyezi Mungu, ni kuwa hata alipokuwa katika kilele cha maudhi kutoka kwa kaumu yake, kamwe hakuitakia mabaya bali aliitakia mema na kuionyesha huruma kubwa. Imepokelewa katika kitabu cha al-Manaqib cha al-Hafidh as-Sarwi al-Halabi kwamba Mtume alipofikia kilele cha maudhi ya kabila lake la Quraish, Malaika alifika mbele yake na kumwambia: 'Ewe Muhammad! Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako na juu ya kizazi chako. Mimi ni Malaika ambaye amepewa jukumu la kusimamia milima. Mwenyezi Mungu amenituma kwako niteremshe juu ya vichwa vyao milima ya al-Akhshabain (nayo ni milima miwili inayopatikana Makka). Ikiwa utaniamuru nifanye hivyo nitafanya. Mtume (saw) akasema: Hapana, kaumu yangu haifahamu (haidiriki mambo).'
Tunamwomba Mwenyezi Mungu aangaze nyoyo zetu na kutupa taufiki ya kuweza kufuata mfano huu mwema wa upole na huruma ya Mtume Mtukufu (saw) katika maisha yetu.
*********
Sifa nyingine ya kuvutia ya Mtume Mtukufu (saw) ni jinsi alivyokuwa akiamiliana kwa mapenzi na upendo mkubwa na watu na vilevile kusamehe makossa yao na kuheshimu rai na maoni yao. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 159 ya Surat Aal Imran: Basi ni kwa sababu ya rehema inayotoka kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukishakata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaomtegemea.
Na tunasoma katika maisha yake Mtume (saw) mifano mingi ya sifa hii njema inayozungumziwa na Aya hii, ambapo tutaashiria baadhi ya mifano hiyo hivi punde.
***********
Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Katika vita vya Dhatu ar-Riqaa' Mtume (saw) aliteremka chini ya mti mmoja uliokuwa kwenye bonde. Alipokuwa hapo, mafuriko yalitokea na kumtenganisha na masahaba zake. Mtu mmoja kati ya mushrikina alimwona Mtume (saw) akiwa katika hali hiyo na Waislamu nao walikuwa upande wa pili wa bonde wakisubiri mafuriko yakatike. Mushrik huyo akiwa na wenzake alisema: Mimi nitamuua Muhammad! Akamkaribia Mtume (saw) na kumyanyulia upanga huku akisema: Ewe Muhammad! Sasa ni nani atakayekunusuru kutoka kwenye makucha yangu?! Mtume akamjibu: Ni Mungu wangu na Mungu wako! Hapo Ghafla Malaika Jibril akamuangusha kichalichali mushrik huyo kutoka juu ya farasa wake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasimama na kuchukua upanga wake, akaketi kwenye kifua chake na kumuuliza: Ni nani atakayekuokoa mbele yangu, ewe Ghaurath? Akasema: Ni msamaha na ukarimu wako ewe Muhammad! Mtume akaachana naye, naye (huyo mushrik) akawa ameamka huku akisema: Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, wewe ni mbora na mwenye ukarimu zaidi kuniliko mimi.'

Wapenzi wasikilizaji, Mtume (saw) pia alikuwa mwingi wa kuomba msamaha na maghfira hata bila ya kuwa na dhambi (Mtume hafanyi dhambi) ili watu wafuate mfano wake katika kuomba maghfira na toba kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtume pia alikuwa akiwaombea sana msamaha waumini. Imepokelewa katika kitabu cha az-Zuhd kutoka kwa Imam as-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Hakika Mwenyezi Mungu humpenda anayekiri na kutubu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akitubia kwa Mwenyezi Mungu mara sabini kila siku bila ya kuwa na dhambi yoyote.'
**********
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji, tunakushukuruni nyote kwa kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.