Jumatano tarehe 07 Novemba 2018
Leo ni Jumatano tarehe 28 Safar 1440 Hijria sawa na tarehe 7 Novemba 2018.
Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63. Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.

Miaka 1390 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka wa 50 Hijria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake. Mjukuu huyo wa Mtume aliuawa shahidi kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland. Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne. Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.
Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, vita vya mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa. Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la kanali hiyo. Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdul-Nassir, kuutaifisha mfereji huo.
Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi kote nchini Iran walifanya maandamano makubwa wakipinga kuingia madarakani serikali ya kijeshi ya Jenerali Golam Reza Azhari aliyekuwa kibaraka wa utawala fasidi wa Kipahlavi. Katika maandamano hayo wananchi Waislamu wa Iran walitangaza azimio wakisema kuwa mabadiliko ya kimaonyesho na kubadilisha nafasi za vibaraka wa Marekani hakuwezi kuzuia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Siku hiyo pia Kiongozi wa harakati za Mapinduzi hayati Imam Khomeini alitoa ujumbe kwa mnasaba wa mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu tarehe 13 Aban mwaka huo huo akiwaambia wananchi kwamba: “Ninyi taifa shujaa, mumethibitisha kwamba vifaru, mitutu ya bunduki na mikuki imeota kutu na kwamba haiwezekani kukabiliana na irada ya chuma ya wananchi.”