Feb 19, 2019 06:50 UTC
  • Ruwaza Njema (14)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kama ilivyo kawaida yetu, katika kipindi hiki pia tutachambua baadhi ya Hadithi za kuaminika kutoka kwa watukufu wa Nyumba ya Mtume (saw) ili zitusaidie na kutuongoza katika njia nyoofu ya kuiga na kufuata mfano mwema wa tabia na nyendo za kuvutia za Mtume (saw) katika maisha yetu ya kila siku.

Ni wazi kuwa Mtume Mtukufu (saw) alikuwa mwingi wa ibada na kumwomba dua Mwenyezi Mungu. Jambo hilo limechukuliwa kuwa moja ya sifa zake bora na za kuvutia ambapo waumini wameshauriwa kuiga na kufuata mfano huo bora katika maisha yao ya kila siku. Hii ni kutokana na ukweli kwamba waja wanaoabudu na kumdhikiri zaidi Mwenyezi Mungu ndio wanaokuwa karibu zaidi na Muumba wao kama anavyosema Mwenyezi Mungu mwenyewe katika Aya ya 21 ya Surat al-Ahzab: Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.

************

Tunaanza wasikilizaji wapenzi kwa kunukuu Hadithi ambayo imenukuliwa na Thiqatul Islam, Sheikh Muhammad bin Ya'qoub al-Kuleini kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba alisema: 'Kuna mambo matatu ambayo Manabii (as) walikuwa wakirithishana kwa ajili ya kuyafanyia kazi, tokea Nabii Adam (as) hadi yalipomfikia Mtume Muhammad (saw) ambaye kila siku alipoamka asubuhi alikuwa akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Ninakuomba imani itakayonifariji moyo na yakini ya kweli ili nipate kujua kwamba halitanifika jambo lolote ila uliloniandikia na unifanye niridhie lile ulilonijaalia, ili nisipende kuharakisha lile uliloliakhirisha wala kuakhirisha lile uliloliharakisha, ewe Uliye Hai, Usiye na Mwanzo wala Mwisho (ni wa kudumu milele), kwa rehema Zako, ninakuomba msaada (ninakulilia)! Nirekebishie mambo yangu yote wala usinieche peke yangu kamwe, hata kwa muda wa kufumba na kufumbua, na mswalie Muhammad na Aali zake.'

 

Tunamwomba Mwenyezi Mungu, ndugu wasikilizaji, atupe taufiki ya kuweza kumfuata Mtume wetu mpendwa (saw) katika matendo yake yote mema aliyoyatenda kwa ajili ya kupata ridhaa yake Mungu Muumba, likiwemo suala la zima la namna ya kujitayarisha kulala. Allama Sayyid Hashim al-Bahrani amenukuu katika kitabu chake cha Hilyat al-Abrar Hadithi kutoka kwa Imam Ja'ffar bin Muhammad al-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Je, nikufahamisheni alichokuwa akisema Mtume (saw) alipokuwa akienda kulala kitandani?' Mpokezi wa Hadithi anasema, nilisema: Ndio. Imam (as) akasema: Alikuwa akisoma Ayat Kursiy na kisha kusema: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, nimemwamini Mungu na kumkufuru Taghuti. Allahumma! Nihifadhi katika usingizi wangu na pia nikiwa macho.' Imam Swadiq (as) amenukuliwa katika kitabu hichohicho akisema katika Hadithi nyingine inayofanana na hiyo: 'Mtume (as) alipoenda kulala kitandani kwake alikuwa akisema: Allahumma! Kwa jina lako niko hai na kwa jina lako ninakufa. Na alipoamka kutoka usingizini alisema: Ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenihuisha baada ya kunifisha, na Kwake ni marejeo.'

***********

Tunasoma Hadithi nyingine wapenzi wasikilizaji, kutoka kitabu cha Qurbil Isnad cha mwanahadithi wa kuaminika Abul Abbas Abdallah bin Ja'ffar al-Humeiri akimnukuu Imam Swadiq (as) ambaye amesema: 'Mtu mmoja alifika mbele ya Mtume (saw) na kumwomba haja. Mtume (saw) akauliza: Je, kuna mtu yeyote aliye na mkopo wa kuniwezesha kukidhi haja ya mwombaji huyu? Mtu mmoja katika Answar akasema: Ninao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Akasema: Mpe huyu mwombaji 'ausaq' (kiwango maalumu) nne za tende. Akatoa na kumpa. Imam Baqir (as) anaendelea kusema: Kisha Answari yule alienda kwa Mtume (saw) kumdai deni lake: Mtume (saw) alimwambia: Itatimia (itakuwa) Inshaallah. Alimrudia kwa mara ya pili naye Mtume (saw) akamjibu vilevile: Itatimia Inshaallah. Alimrejea kwa mara ya tatu na Mtume (sw) akamjibu: Itatimia Inshaallah. Hapo Answar yule akamwabia: Umezidi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kuniambia kila mara, itatimia Inshaallah. Akasema: Mtume (saw) alicheka na kusema: Je, kuna mtu aliye na mkopo? Akasema: Hapo mtu mmoja alisimama na kumjibu: Ninao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mtume (saw) akamuuliza: Una kiasi gani? Akajibu: Kiwango chochote utakachotaka. Akasema: Mpe huyu 'ausaq' nane za tende. Answari yule akasema: Lakini nina nne tu, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mtume (saw) akamjibu: Mwongeze nne – yaani mwongeze 'ausaq' nne za tende za ziada kama alama ya huruma na ukarimu wa Mtume (saw).'

 

Na sifa nyingine ya kuvutia katika tabia njema za Mtume (sw) ni sifa ya wingi wa kutoa na kuwakirimu watu. Hakuwahi kumrudisha mwombaji yeyote bila ya kumkidhia haja yake wala kujilimbikizia chochote katika mali ya dunia. Imepokelewa katika kitabu cha Qurbil Isnad, Hadithi kutoka kwa Imam Baqir (as) kwamba alisema:  'Hakika Mtume (saw) hakuacha urithi wowote, iwe ni katika dinari, dirhamu, mtumwa, mjakazi, kondoo wala ngamia, bali aliaga dunia (saw) hali ya kuwa ameweka rehani nguo yake ya vita kwa Yahudi mmoja mjini Madina mkabala wa 'swaa' (kipimo maalumu) 20 za shayiri aliyokopa kwa ajili ya familia yake.'

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.