May 26, 2019 02:32 UTC
  • Jumapili, tarehe 26 Mei, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 20 Ramadhani 1440 Hijria, sawa na tarehe 26 Mei, 2019.

Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makka. Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu wengi. Muamala huo wa huruma na upendo wa Mtume (saw) uliwavutia watu wa kabila la Kuraishi kuingia katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu.

Ukombozi wa mji wa Makkah

Siku kama ya leo miaka 898 iliyopita, alifariki dunia Ibn Shajari Baghdadi, fasihi na mtaalamu wa elimu ya nahau wa Waislamu. Abu Sa'adat Hibatullah Ibn Ali Alawi Hassani, mtaalamu wa nahau, lugha ya Kiarabu, fasihi na malenga wa Kishia, alizaliwa mwaka 450 Hijiria. Nasaba ya msomi huyo inarejea hadi kwa Imam Hassan (as) mjukuu wa Mtuke Muhammad (saw) na ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa Alawi, Hassani. Akiwa kijana alianza kusomea fasihi, nahau, hadithi na elimu mbalimbali za zama zake na kamwe hakuwahi kuacha kusoma, kama ambavyo hata alipokuwa mzee, bado aliendelea kujifunza kwa wasomi wa zama zake. Aidha alifundisha lugha ya nahau kwa kipindi cha miaka 70 ambapo alitokea kupata wanafunzi mashuhuri katika uwanja huo. Miongoni kwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al-Aamaal' 'Al-Hamaasah' na 'Mandhumat Ibn Shajarah.' Hatimaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 mjini Baghdad Iraq na kuzikwa mjini hapo.

Ibn Shajari Baghdadi

Siku kama ya leo miaka 814 iliyopita, alifariki dunia Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na msomi mtajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria na mtaalamu mashuhuri wa jiografia. Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadaye akamuachia huru. Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Muujamul-Buldan" na Muujamul- Udabaa."

Yaqut Hamawi

Siku kama ya leo miaka 766 iliyopita, alifariki dunia Ibn Saai Baghdadi, fasihi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Sheikh Tajud-Din Abu Twalib Ali Ibn Anjub Ibn Uthman Baghdadi, Maarufu kwa jina la Ibn Saai, alizaliwa mwaka 593 mjini Baghdad, Iraq. Awali alianza kujifunza elimu za zama zake kwa walimu mbalimbali na kuibukia kielimu. Kwa miaka kadhaa Ibn Saai alikuwa akisimamia maktaba ya utawala wa wakati huo mjini Baghdad na ambayo ilitumiwa kwa ajili ya kutwalii. Na baada ya mji wa Baghdad kudhibitiwa na silsila ya utawala wa Wamongolia, hatimaye Ibn Saai Baghdadi aliteuliwa na Nasir al-Din al-Tusi kwa ajili ya kusimamia maktaba mbalimbali za mji huo. Ni katika kipindi hicho ndipo akatokea kuwa mwandishi mkubwa, jambo ambalo lilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Kitabu cha 'Alkhulafaau' ni miongoni mwa athari mashuhuri za Ibn Saai. Aidha ameandika kitabu cha 'Akhbaarul-Udabaa' 'Akhbaarul-Hallaj' na 'Akhbaaru Qudhaatu Baghdad.' Abin Saai, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa mjini Baghdad.

Ibn Saai Baghdadi

Siku kama ya leo, miaka 220 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru.

Alexander Pushkin

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita Charles Louis Alphonse Laveran, daktari wa Kifaransa aligundua chanzo cha ugonjwa wa malaria duniani. Baada ya kupata shahada yake ya uzamifu, Daktari Alphonse Laveran alisafiri Algeria kwa lengo la kuhudumia watu wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya afya na tiba. Akiwa huko alipata fursa ya kuchunguza na kufanya utafiti wa kina kuhusiana na malaria, ugonjwa ambao ulikuwa ukiwaangamiza watu wengi katika pembe tofauti za dunia, ambapo mwaka 1880 alifanikiwa kupata chanzo cha ugonjwa huo. Aligundua kuwa ugonjwa huo ulisababishwa na mbu waanaoitwa Anopheles ambao huishi katika sehemu za unyevunyevu na zilizo na maji yaliyotuama. Mwaka 1907 Alphonse Laveran alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na juhudi kubwa alizofanya katika uwanja wa tiba na ugunduzi wake wa chanzo cha ugonjwa wa malaria.

Charles Louis Alphonse Laveran

Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita Ufaransa iliikoloni rasmi nchi ya Kiarabu ya Tunisia. Kabla ya hapo Wafaransa waliingia nchini humo kama wafanyabiashara. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini katika muongo wa 1930 wananchi wa Tunisia wakaanzisha harakati za ukombozi chini ya uongozi wa Habib Bourguiba, ambapo mwaka 1975 waliung'oa madarakani utawala wa kifalme na kumtawaza Bourguiba kuwa rais wa nchi hiyo. Baada ya kuingia madarakani, Bourguiba alianza kuitawala nchi hiyo kidikteta hadi mwaka 1987 ambapo alipinduliwa na Zein al-Abedeen bin Ali, afisa mkuu wa polisi wakati huo. Zein al-Abedeen pia aliitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma na ukanadamizaji hadi Januari 2011 ambapo alipopinduliwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu na kulazimika kukimbilia Saudi Arabia.

Bendera ya Tunisia

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, kisima cha kwanza cha mafuta cha Iran kilianza kuchimbwa huko katika mji wa Masjid Suleiman kusini magharibi mwa Iran. Mafuta ya kisima hicho yalifikiwa umbali wa kina cha mita 600, mafuta ambayo hatimaye yaliruka hadi kufikia urefu wa mita 25 kutoka uso wa ardhi. Mji wa Masjid Suleiman una umuhimu mkubwa kutokana na upatikanaji wa madini na vyanzo vya mafuta. Ni vyema kutaja hapa kuwa Iran ni moja ya nchi muhimu duniani kwa kuwa na akiba kubwa ya mafuta na ni nchi ya pili yenye akiba kubwa ya gesi duniani baada ya Russia.

Kisima cha kwanza cha mafuta nchini Iran

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, yaani sawa tarehe 26 Mei mwaka 1966 Miladia, Guyana inayopatikana kaskazini mwa Amerika ya Kusini ilipata uhuru wake. Ardhi ya Guyana iligunduliwa na mabaharia wa Kihispania huko kaskazini mwa Amerika ya kusini karibu miaka 500 iliyopita na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya mkoloni Mhispania. Hata hivyo mwanzoni mwa karne ya 17 Miladia, vita vilizuka kati ya makoloni ya Ulaya kwa ajili ya kulidhibiti eneo hilo ambalo lilijumuisha Guyana, Guyana ya Ufaransa, Surinam na baadhi ya maeneo ya Brazil na Venezuela ya sasa. Mwaka 1815 kulifanyika mkutano wa Vienna ambao uliainisha mipaka ya sasa ya nchi ya Guyana.

Bendera ya Guyana

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi lilibuniwa rasmi. Baraza hilo linazijumuisha nchi sita zilizoko kusini mwa Ghuba ya Uajemi za Saudi Arabia, Kuwait, Imarati, Bahrain, Qatar na Oman. Lengo kuu la kubuniwa baraza hilo lilikuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi na kuungana mkono dhidi ya uchokozi na vitisho vya nje. Pamoja na hayo lakini baraza hilo hadi sasa limeshindwa kudhamini usalama wa eneo hili nyeti pamoja na maslahi ya kitaifa ya nchi wanachama kutokana na kutegemea kwake nguvu za kigeni na vilevile kutoshirikishwa vyema wanachama wake katika msuala yanayowahusu. Viongozi wa nchi wanachama hukutana mara mbili kwa mwaka ili kuchunguza masuala ya ndani ya baraza hilo na vilevile ya kieneo.

Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi