Jun 26, 2019 21:54 UTC
  • Alkhamisi, 27 Juni,  2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe 27 Juni mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, sawa na tarehe 6 Tir 1360 Hijria Shamsia, Ayatullahil Udhma Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa mjumbe wa Imam Khomeini katika Baraza Kuu la Ulinzi na Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, alinusurika kifo baada ya kundi la kigaidi la Munafikiin kumtegea bomu wakati alipokuwa akitoa hotuba katika mojawapo ya misikiti ya Tehran. Kwenye tukio hilo la kigaidi, Ayatullah Khamenei alijeruhiwa vibaya mkono wake wa kulia. 

Ayatullah Ali Khamenei

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita inayosadifiana na 27 Juni 1977, nchi ya Djibouti iliyoko karibu na eneo la Pembe ya Afrika ilipatia uhuru  kutoka kwa mkoloni Mfaransa baada ya kupita miaka kadhaa ya harakati ya kupigania uhuru. Tokea mwaka 1896 nchi hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Somalia Ufaransa na kuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini baada ya kupita miongo minane, hatimaye nchi hiyo ilipata uhuru. Djibouti ilikuwa nchi ya mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na inahesabiwa kuwa nchi muhimu iliyoko katika eneo la kiistratijia kwa kuwa inapakana na Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, kweye eneo la lango bahari la 'Bab Mandab'. 

Bendera ya Djibouti

Tarehe 27 Juni 1993, Marekani ilirusha makombora 23 huko Baghdad mji mkuu wa Iraq na pambizoni mwa mji huo. Shambulio hilo lilifanyika kwa kisingizo kwamba viongozi wa utawala wa zamani wa Iraq walitaka kumuuwa George Bush 'baba', Rais wa zamani wa Marekani wakati alipokuwa safarini nchini Kuwait mwezi April mwaka huo huo. Shambulio hilo lilipelekea watu sita kuuawa na jengo la makao makuu ya Taasisi ya Usalama ya Iraq liliharibiwa kabisa. 

Na katika siku kama ya leo miaka 328 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematullah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.

Sayyid Neematullah Jazairi