Ulimwengu wa Spoti, Jul 15
Hujambo mpenzi msikilizaji natumai huna neno, karibu tututupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa…….
Mieleka; Iran yazidi kung'ara
Baada ya timu ya taifa ya mieleka aina ya Greco Roman ya vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutwaa taji la Mashindano ya Ubingwa wa Makurutu ya Asia mwaka huu 2019, katika mji wa Nur-Sultan nchini Kazakhstan siku ya Jumatano, wenzano wa mieleka mtindo wa Free-Style walivuta subra na Jumapili, ilikuwa zamu yao ya kung'ara. Timu hiyo ya Iran ya mieleka ya kujiachia ilitwaa ubingwa wa mashindano hayo ya makurutu nchini Thailand, baada ya kuzoa jumla ya alama 201.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Spoti wa Chon Buri nchini Thailand, wanamieleka wa Iran walifanikiwa kutwaa medali 6 za dhahabu. Jumapili ambayo ilikuwa siku ya mwisho wa mashindano hayo, Wairani waliotwaa dhahabu katika kategoria tofauti ni Mahdi SHIRAZI (61kg), Ali Reza ABDOLLAHI (92kg) na Amir ZARE (125kg). Kabla ya hapo, Wairani wengine walikuwa wamelipa taifa hili nishani nyingine 3 za dhahabu. Japan imeibuka ya pili kwa alama 146, huku India ikifunga orodha ya tatu bora kwa pointi 129.
Voliboli; ndoto ya Iran yazimwa
Ndoto za timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Ligi ya Mataifa ya mchezo huo zimezimwa baada ya timu hiyo ya kuzabwa na Brazil na Poland katika mechi zilizopigwa mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Credit Union 1 Arena mjini Chicago nchini Marekani. Siku ya Jumamosi Iran ilishindwa kutamba mbele ya Brazil na kukubali kichapo cha seti 3-2 za (25-20, 25-23 na 26-24).
Kwa ushindi huo timu hiyo ya Amerika ya Kusini imefanikiwa kujatia tiketi ya fainali, ambapo itakula meza sasa na miamba ya voliboli, Russia, Poland na Marekani. Kabla ya hapo, Iran ilikuwa imezabwa pia na Poland katika mchezo mwingine wa Kundi B. Iran ililazwa seti 3-0 na timu hiyo ya Ulaya, za ((25-18, 25-20, 25-22). Hii ni licha ya timu hiyo ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuisasaga Poland katika mchuano wa huko nyuma, ambapo iliitandika (25-20, 21-25, 18-25, 25-17, 15-8) katika mechi ya Wiki ya 3 ya mashindano hayo hapa nchini. Timu hiyo ya Iran inayonolewa na Igor Kolakovic ilikuwa ya kwanza kujikatia tiketi ya fainali inayofahamika kama Volleyball Nations League Final Six baada ya kuifanya vibaya Serbia.
Fainali Afcon, Senegal kuvaana na Algeria
Siku ya Jumapili timu ya taifa ya soka ya Senegal ilishuka dimbani kuvaana na Tunisia katika nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Misri, huku Nigeria ikivaana na Algeria. Algeria imevuka kiunzi hicho na sasa watakutana na Senegal kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mwaka huu 2019.
Timu hizo ambazo zilianza mashindano katika kundi C na Tanzania na Kenya zimeibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao na kukata tiketi ya kumenyana tena kwenye fainali. Goli la kujifunga la Tunisia katika muda wa nyongeza limewavusha Senegal mpaka hatua ya fainali. Japo wengi waliipigia debe Senegal kushinda mchezo huo, lakini ushindi haukuwa rahisi, Tunisia walipambana kufa kupona.
Nusu fainali ya pili baina ya Algeria na Nigeria ilitimua vumbi, jijini Cairo, ambapo ndoto za Nigeria za kutwaa kombe hilo kwa mara ya 4 zimezimwa kwa kipigo cha magoli 2-1 kutoka kwa mbweha wa jangwani, Algeria.
Algeria sasa ipo mbioni kulinyakua kombe hilo kwa mara ya pili. Mara ya kwanza na ya mwisho kwao kulinyanyua kombe hilo ilikuwa 1990. Fainali hiyo itapigwa Ijumaa katika Dimba la Kimataifa la Cairo kuanzia saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika CAF, mshindi wa kombe hilo atatunukiwa kitita cha dola milioni 4.5, mshindi wa pili dola milini 2.5 na mshindi wa tatu dola milioni 2.
Kombe la Kagame, Azam ana kwa ana na Mazembe
Mabingwa mara tano wa michuano ya klabu bingwa Afrika TP Mazembe ya Congo DR watakutana na klabu ya Azam FC ya Tanzania ambao ni mabingwa watetezi wa kombe la Kagame Jumanne katika mchezo wa robo fainali ya mashindano hayo ya Afrika Mashariki na Kati. Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali Rwanda, ambao utafuatiwa na mchezo kati ya KCCA ya Uganda na wenyeji Rayon Sports. Robo fainali nyingine zitachezwa Jumatano, ambapo wenyeji wengine APR watamenyana na Manyema Union, kabla ya Gor Mahia ya Kenya kutoana udhia na Green Eagles ya Zambia.
Voliboli; Kombe la Afrika
Timu ya taifa ya wanawake ya voliboli ya Kenya, almaarufu Malkia Strikers, siku ya Jumapili ilishuka dimbani katika mchuano wa fainali za Kombe la mataifa ya Afrika nchini Misri dhidi ya Cameroon. Hata hivyo Malkia Strikers walishindwa kufurukuta mbele wa Cameroon, ambaye ni bingwa mtetezi, na kukubali kuzabwa seti tano za 25-17,25-27,25-23,23-25,16-14. Katika mchezo huo uliopigwa katika Ukumbi wa Michezo wa Oktoba 6 mjini Giza, Malkia Strikers walicheza mchezo wa kasi na kujiamini, wakiwa na hamu kubwa ya kutwaa taji hilo kwa mara nyingine tena. Hata hivyo waliangukia pua. Malkia Stars walitinga fainali ya Kombe la mataifa ya Afrika baada ya kuichabanga Senegal seti 3 bila za ((25-13, 25-13, 25-20) katika mechi ya nusu fainali. Timu hiyo ilianza kampeni yake ya kuweka rikodi kwenye michuano ya 10 ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Algeria kwenye mechi ya kundi 'B' iliyochezwa uwanja wa October 6 huko Giza, Misri. Awali kwenye kiwanja hichohicho, mabingwa watetezi Cameroon waliwaonesha Botswana umwamba wao kwa kuwachabanga 3-0 kwenye mechi ya ufunguzi wa mashindano yanayoshirikisha timu saba. Kenya, ikiwa chini ya Muitaliana Shaileen Ramdoo, walianza kudhibiti mchezo toka mechi inaanza, na hawakutulia hadi walipofanikiwa kuwabana mbavu Algeria. Timu hiyo ya Kenya imefanya vyema na kutinga fainali licha ya kutolipwa marupurupu yao. Wakenya katika mitandao ya kijamii wanafanya kampeni ya kushinikiza walipwe, kwa kutumia heshtegi #IstandWithMalkia.
Wakati Malkia Stars wakitolewa tonge mdomoni, wenzao Lionesses wa raga ya wachezaji 15 kila upande walikuwa wanang'ara pia katika fainali ya Kombe la Elgon. Timu hiyo ya Kenya imehifadhi taji hilo baada ya kuichachafya Uganda 16-5 katika Uwanja wa Raga wa Kyadondo mjini Kampala. Hii ni mara ya tano mfulilizo kwa timu hiyo kutwaa Kombe la Elgon. Kadhalika timu ya wanaume ya Kenya ya raga ya wachezaji 15 kila upande maarufu kama Simbas waliibuka kidedea. Robert Sseguya Kocha wa Uganda Rugby Cranes anakiri kuwa, wachezaji wake walikuwa na mapungufu mengi kiwanjani ndiposa wakapoteza.
Dondoo za Hapa na Pale
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Tanzania, Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa rai yake kufuatia uamuzi wa Shirikisho la Soka nchini humo TFF kumtimua kocha Emmanuel Amunike. Dkt. Mwakyembe amesema kuwa kama TFF wameamua kufuata nyayo za Misri katika kumfuta kazi Amunike basi na wao wanapaswa wakamilishe mchakato kwa kujiuzulu nafasi zao. Amebainisha kuwa, ”Sisi hatuna tatizo na maamuzi ya TFF endapo tu yatatupeleka mbele, lakini kama ni uamuzi wa kuwaiga Wamisri baada ya kutolewa AFCON, hayo ni makosa makubwa sana kwa sababu kama unaiga basi nao wakamilishe kwa kujiuzulu safu nzima ya uongozi.”
Aidha, amesema kuwa hadi kufikia Julai 24 mwaka huu, benchi la ufundi la Taifa Stars na Viongozi wa TFF wanatakiwa kutoa ripoti yao ya michuano ya AFCON kwa ajili ya kujadiliwa. Huku hayo yakijiri, Kocha Mkuu wa Azam FC, Etienne Ndayiragije ameteuliwa kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kushika nafasi ya Amunike. Uteuzi wa Ndayiragije ambaye kwa sasa yuko nchini Rwanda akiiongoza Azam FC kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) ulitangazwa mara baada ya kamati ya utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kukutana kwa dharura jijini Dar es Salaam.
Na Novack Djockovic ameshinda taji la tano la mashindano makubwa ya Tenisi ya Wimbledon kwa kumnyuka Roger Federer kwenye viwanja vya Centre Court mjini London. Fainali hiyo iliyokutanisha magwiji hao wa tenisi inatajwa kama mechi bora na ngumu kuwahi kutokea katika historia ya mashindano hayo. Djokovic ametwaa ushindi kwa kumgaragaza hasimu kwa seti 5 za 7-5, 6-1, 6-4, 7-3 na kutwaa taji la 16 la Grand Slam na la tano la Wimbledon.
……………………TAMATI………………