Jumamosi, 28 Septemba, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 28 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria mwafaka na tarehe 28 Septemba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 785 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi ulitekwa na Hulagu Khan Mongol baada ya kuuawa Mustaasim aliyekuwa mtawala wa mwisho wa utawala wa Bani Abbas. Mauaji ya mtawala huyo yalihitimisha utawala wa kizazi hicho uliotawala sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kislamu kwa kipindi cha miaka 500. Hulagu Khan Mongol hakusita kufanya mauaji na jinai za aina mbalimbali katika uvamizi wake wa nchi mbalimbali, na baada ya kuteka baadhi ya maeneo ya Iran na kuua watu kwa umati katika maeneo ya mijini na vijijini, aliushambulia mji wa Baghdad na kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya maelfu ya wakazi wake. Vilevile aliharibu na kuvunja nyumba na majengo muhimu ya mji wa Baghdad. ***

Miaka 128 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kimarekani Herman Melville. Melville alizaliwa mwaka 1819 na kuanza kujishughulisha na ubaharia. Katika moja ya safari zake, meli ya Melville ilizama na kusukumwa na maji hadi katika kisiwa kimoja ambako wakazi wake walikuwa wala watu. Melville ameelezea kisa hicho na jinsi alivyowatoroka watu hao katika kitabu alichokipa jina la Typee. Kuchapishwa kitabu hicho, kuliongeza zaidi umashuhuri wake. ***

Katika siku kama ya leo miaka 99 iliyopita nchi ya Oman ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na siku hii huadhimishwa nchini humo kwa anuani ya sikukuu ya taifa. Nchi ya Oman inayoongozwa Kifalme kijiografia ipo kusini mwa Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ikipakana na Saudi Arabia, Imarati na Yemen. Oman ilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya mkoloni Mreno mwaka 1508 na baada ya miaka 150 yaani mwaka 1659 ikadhibitiwa na utawala wa Othmaniyah. ***

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, alifariki dunia rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Abdel Nasser alizaliwa mwaka 1916. Alishiriki katika vita vya kwanza vya Waarabu na utawala wa Kizayuni hapo mwaka 1948 na kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kushirikiana na Jenerali Najib, dhidi ya Mfalme Faruq 1952 na kuung'oa utawala wa kisultani nchini humo. Miaka miwili baadaye Gamal Abdel Nasser alimuondoa madarakani mshirika wake Jenerali Najib na kuchukua jukumu la kuiongoza Misri sambamba na kufanya juhudi za marekebisho, kupambana na ukoloni na utawala ghasibu wa Israel. Mwaka 1956 aliutaifisha mfereji wa Suez na kuufanya kuwa mali ya taifa la Misri, hatua iliyozifanya nchi za Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuishambulia nchi hiyo. ***

Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likiutaka utawala wa Kizayuni kukomesha operesheni ya kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Rasimu ya azimio hilo ililaani uchimbaji huo wa mashimo kinyume cha sheria chini ya eneo hilo takatifu. Hata hivyo upinzani wa Marekani ulipelekea kuondolewa kipengee hicho katika azimio hilo. Uchimbaji huo wa mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa unaofanywa na Israel ulizusha machafuko ya umwagaji damu mkubwa hapo tarehe 23 Septemba 1996 kati ya askari wa utawala huo ghasibu na Wapalestina ambapo askari hao waliua na kujeruhi mamia ya Wapalestina. ***

Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Intifadha ya wananchi wa Palestina kwa mara nyingine tena ilipamba moto. Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Likud na mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika kambi za Sabra na Shatila ya kuingia katika Msikiti wa al -Aqswa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu, iliwatia hasira Wapalestina na kuwafanya waanzishe maandamano na mapambano makubwa dhidi ya utawala huo wa Israel.
