Jumamosi, Aprili 23, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 15 Rajab 1437 Hijria ambayo inasaidiana na tarehe 23 Aprili mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Bibi Zaynab (AS) mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi. Bibi Zaynab AS alizaliwa mwaka wa 6 Hijiria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake Imam Ali AS na mama yake Bibi Fatimat Zahra AS. Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab AS alishiriki katika tukio la Karbala pamoja na kaka yake Imam Hussein AS na watu wengine wa familia ya Mtume SAW. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake. ***
Miaka 1435 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, Kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas. Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas. ***
Katika siku kama ya leo miaka 400 iliyopita, alizaliwa William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza. Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho. ***
Miaka 158 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwanafizikia Max Plank wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hisabati aliyebuni nadharia ya kwanta katika elimu ya fizikia. Mwaka 1918 Max Plank alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia ya kwanta. Plank ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto (sayansi ya uhusiano wa joto na kazi za mitambo), fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika medani hiyo.***
Na katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India. Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kupendwa zaidi na wananchi wa India. ***