Jumatano tarehe tarehe 13 Novemba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 15 Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa Novemba 13 mwaka 2019.
Miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 13 Novemba 1970, tufani kubwa na kimbunga cha kutisha kiliikumba nchi ya Bangladesh. Janga hilo lilitokea wakati mapambano ya Wabangali kwa ajili ya kujitenga na Pakistan na kupata uhuru yalipokuwa kileleni. Tufani hiyo kubwa ilisababisha vifo vya watu laki mbili na kujeruhi wengine laki nane. Kimbunga na tufani hiyo pia iliwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kusababisha hasara kubwa katika mashamba, viwanda, makazi ya raia na miundombinu ya nchi hiyo. Bangladesh ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na majanga ya kimaumbile kama vimbunga, tufani na mafuriko ya mara kwa mara.
Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Tarehe 22 Aban miaka 23 Iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Murtadha Pasandidah kaka yake Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Murtadha alisimamia na kumlea ndogo wake yaani Ruhullah Khomeini akishirikiana na mama na shangazi yake baada ya kuuawa shahidi baba yao. Alipata elimu ya msingi kwa wanazuoni wa Isfahan na kushiriki masomo ya juu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baadaye alirejea katika eneo la Khomein na kuanza kufunza elimu za fiqhi, usulul fiqhi, teolojia na mantiki. Katika kipindi cha utawala wa kifalme wa Reza Khan Pahlavi, Ayatullah Pasandidah alipelekwa uhamishoni kutokana na mapambano yake dhidi ya dhulma za utawala huo na alihukukiwa kifungo jela kwa kupinga amri ya utawala ya kupiga marufuku vazi ya hijabu. Wakati wa mapambano ya Kiislamu ya taifa la Iran mwanazuoni huyo shupavu alifikishwa mahakamani mara nyingi na kuhukumiwa. Imam Khomeini daima alikuwa akimheshimu kaka na mwalimu wake huyo.

Na miaka 4 iliyopita tarehe 13 Novemba saa 3 na dakika 16 usiku kwa wakati wa Ulaya ya kati, milipuko kadhaa ya kigaidi ilitokea katika maeneo nambari 1, 10 na 11 ya jiji la Paris nchini Ufaransa na kuua watu 130 na kujeruhiwa wengine 368. Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France ulioko kaskazini mwa jiji la Paris wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu za taifa za Ufaransa na Ujerumani. Wakati huo huo watu wengine 87 waliuawa katika utekaji nyara uliofanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Bataclan mjini Paris. Mashambulizi hayo yalihesabiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Siku moja baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo.
