Ulimwengu wa Michezo
SPOTI, DISEMBA 9
Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....
Mpira wa Kikapu kwa Walemavu: Iran ya 3
Timu ya taifa ya wanaume ya mpira wa kikapu wa viti vya magurudumu ya Iran imeibuka ya tatu katika mashindano ya mabingwa wa bara Asia. Katika mchezo wao wa mwisho Jumamosi, timu hiyo ya Iran ya basketboli ya walemavu ilitunukiwa medali ya shaba baada ya kuisasambua Japan vikapu 65-55 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu. Ilikuwa fursa nzuri kwa Iran kulipiza kisasi, kwani hapo kabla walikuwa wamebanjuliwa na Wajapan vikapu 71-51 mnamo Disemba Mosi. Iran iliwapelekea mbio Wajapan katika mchezo wa Jumamosi uliopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Mashariki katika mji wa Pattaya nchini Thailand na kupata ushindi huo mnono. Muirani Omid Hadizahar alifunga pointi 33 ambazo ni za juu kabisa katika mchezo, huku Murakami wa Japan akiambulia 15.
Australia iliibuka kidedea na kutwaa medali ya dhahabu, baada ya kuizaba Korea Kusini vikapu 62-45 katika mashindano hayo ya kikanda yanayofahamika kama IWBF Asia Oceania Championships. Siku ya Ijumaa, timu ya wanawake wa Iran katika mchezo huo iliichabanga Afghanistan vikapu 48-35 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tano. Mashindano hayo ya kibara yaliyozivutia timu 14 za wanaume na saba za wanawake yalianza Novemba 27 na kufunga pazia lake Jumamosi ya Disemba 7.
CECAFA yang'oa nanga: Tanzania Bara na Visiwani waanza vibaya
Tanzania Bara imeanza vibaya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Senior Challenge) baada ya kuchapwa bao 1-0 na Kenya katika mchezo wa Kundi B jioni ya Jumapili katika Uwanja wa Lugogo mjini Kampala, Uganda. Bao lililozamisha jahazi la Kilimanjaro Stars inayofundishwa na kocha Juma Mgunda anayesaidiwa na Zubery Katwila lilifungwa na Hassan Abdallah dakika ya nne tu ya mchezo akimalizia pasi safi ya Anthony Wambani aliyewatoka mabeki kiustadi.
Katika mechi nyingine ya CECAFA Challenge ya kundi hilo, Zanzibar ililazimishwa sare ya 1-1 na Sudan mchana wa Jumapili hiyo katika Uwanja huo wa Lugogo. Makame Khamis alianza kuwafungia Zanzibar Heroes katika dakika ya 55, baada ya mabeki wa Sudan kujikanganya.
Hata hivyo mchezaji Montasir Yahya wa Sudan alifanya mambo kuwa suluhu bin suluhu katika dakika za lala salama.
Zanzibar itarejea uwanjani Jumanne kumenyana na Tanzania Bara kabla ya kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na Kenya Disemba 14. Tanzania Bara itakamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na Sudan Disemba 14, wakati Nusu Fainali zitafuatia Desemba 17 na Fainali Desemba 19. Bingwa mtetezi wa kombe hilo la Chaleji ni Kenya ambayo ilitwaa ushindi mwaka 2017 kwa kuifunga Zanzibar Heroes katika fainali iliyoisha kwa sare ya mabao 2 – 2, kabla ya kuibuka kidedea kwa penati 3 – 2.
Tanzania Bingwa Copa Africa Cup
Tanzania iliicharaza Zimbabwe mabao 6-2 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Copa Coca-Cola la Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 16. Mashindanno hayo yalifahyika mjini Thika, umbali kilomia 50 kutoka mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Michezo hiyo ambayo ni mikubwa barani Afrika kwa vijana imezihusisha timu 10 za barani Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya ambao ndio wenyeji wa michuano, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Uganda, Ethiopia, Namibia, Angola, Botswana na Msumbiji. Tanzania ilianza vyema ilipochuana na timu ya mpira wa miguu ya Afrika Kusini na kuibuka na ushindi wa goli 3-1 na baadae kucheza mchezo wa pili dhidi ya Zambia ambapo matokeo yaliisha kwa Zambia kuibuka na ushindi wa 2-0. Mbali ya kutwaa ubingwa huo kwa kishindo, mshambuliaji wa Tanzania, Paul Nyerere aliikubuka mfungaji bora wa mashindano hayo na kuzawadiwa tuzo ya kiatu cha dhahabu. Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa M-Pesa Foundation Academy, Thika, Tanzania ilianza kwa kasi na Nyerere akifunga mabao matatu (hatrick) katika kipindi cha kwanza. Hatrick hiyo ilikuwa ya pili kwa Nyerere ambapo katika mchezo dhidi Uganda, alifunga mabao matatu katika ushindi wa mabao 6-2. Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Pindi Chana aliikabidhi Tanzania kombe na zawadi ya kiatu cha dhahabu kwa Nyerere. Wadau wanasisitiza kuwa, mashindano hayo yanatoa fursa nzuri ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi za bara Afrika.
Riadha: Kenya haishikiki Marekani
Kenya haishikiki kwenye riadha za masafa marefu! Ndivyo unavyoweza kusema kwa mukhtasari, juu ya mbio za Honolulu Marathon zilizofanyika Jumapili nchini Marekani. Mkenya Titus Ekiru aliibka kidedea katika mbio hizo za masafa marefu zilizofanyika mjini Honolulu, alikozaliwa aliyekuwa rais wa Marekani mwenye asili ya Kenya, Barack Obama. Ekiru mwenye umri wa miaka 27, mbali na kuhifadhi taji hilo, alijiwekea rekodi mpya kwa kumaliza mbio hizo kwa kutumia masaa mawili, dakika saba na sekunde 59. Ekiru amewaongoza Wakenya wenza Wilson Chebet na Edwin Koech kutwaa nafasi tatu za kwanza. Mwanariadha huyo ambaye nyota yake ya jaha inang'aa kwa kasi, ametunukuliwa hundi ya dola 40,000, mbali na dola 25,000 kwa kuibuka mshindi, dola 10,000 kwa kuweka rekodi mpya, na bonasi ya dola 5,000 kwa kumaliza mbio hizo za kilomita 42 chini ya masaa mawili na dakika 8. Wakati huohuo, Margaret Muriuki Wangare ameibuka mshindi kwa upande wa wanawake, kwa kutumia masaa 2:31:09. Anasema sehemu kubwa ya dola 40,000 aliyozawadia kwa kuibuka kidedea, atazielekeza kwa ajili ya matibabu ya mamake mzazi anayeugua, kwa jina la Agnes Muthoni Kenyua.
Dondoo za Hapa na Pale
Nchi wadhamini na wakosoaji wa serikali ya Rais Paul Kagame wamekosoa vikali hatua ya Rwanda kujibebesha mzito wa kuidhamini klabu ya soka ya PSG ya Ufaransa. Hata hivyo serikali ya Kigali inashikilia kuwa, mkakati huu wa kupiga jeki sekta ya utalii umekuwa na matokeo chanya kwa uchumi wa Rwanda. Rwanda imetangaza kuingia tena mkataba wa miaka 3 na klabu hiyo ya Ufaransa inayomilikiwa na Qatar kwa ajili ye kuendelea kutangaza utalii wao, ambapo kuanzia msimu ujao Rwanda ndio watakuwa wauzaji wa kahawa ya Rwanda katika uwanja wa nyumbani wa PSG. Mwaka jana, Rwanda iliingia mkataba wa miaka mitatu na Arsenal kutangaza Utalii, kwa ajili ya kupitia upande wa mikono wa jezi za Arsenal na kuandikwa “Visit Rwanda”. Mkataba wa Rwanda na Arsenal uliigharimu Rwanda dola milioni 44.3 lakini ndani ya mwaka huo 2018 ilifaidika kwa kupata mapato ya dola milioni 88.3 kupitia Utalii moja kwa moja. Hayo ni kwa mujibu wa Claire Kamanzi, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB).
Na mchezaji nyota wa klabu ya Bercelona, Lionel Messi ndio mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or 2019, hiyo ikiwa ni tuzo yake ya 6 ya Ballon d’Or akimzidi mpinzani wake wa muda wote Cristiano Ronaldo aliyewahi kutwaa tuzo hiyo mara 5. Maashiki wa soka walikuwa wanasubiri kwa hamu na shauku kuu kujua ni nani atakuwa mshindi kati ya Van Dijk, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Hata hivyo Messi alitangazwa mshindi katika hafla ya kutoa tuzo hiyo iliyofanyika katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris. Wengine waliofanikiwa kushinda tuzo katika usiku wa Ballon d’Or 2019 ni beki wa Juventus Matthijs De Light tuzo ya mchezaji bora kijana (Kopa Trophy). Golikipa wa Liverpool Alisson Becker ameibuka mshindi wa tuzo ya kipa bora wa mwaka na Megan Rapinoe wa timu ya taifa ya wanawake ya Marekani akatwaa tuzo ya mchezaji bora wa kike (Ballon d’Or). Haya yakifanyika, Cristiano Ronaldo alikuwa jijini Milan, kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Italia katika hafla za the Gala del Calcio.
.....................................TAMATI.......................