Jumapili, tarehe 23 Februari, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 28 Mfunguo Tisa Jamaduth-Thani 1441 Hijria, sawa na tarehe 23 Februari 2020.
Siku kama ya leo miaka 851 iliyopita yaani sawa na tarehe 28 Jamaduth-Thani mwaka 590 Hijiria, aliaga dunia katika mji mkuu wa Misri, Cairo Abul Qassim Shatibi, alimu na qarii mashuhuri wa Qur'ani ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Imam al-Qurra. Alizaliwa mwaka 538 Hijria ambapo mbali na elimu ya usomaji Qur'ani, alikuwa amebobea pia katika elimu ya tajwidi, Tafsiri ya Qur'ani, hadithi, nahau, lugha na elimu nyingine. Abul Qassim Shatibi ameacha athari nyingine katika nyuga mbalimbali ambapo Qasidat al-Shatibiyah ni moja tu ya vitabu vyake mashuhuri, kitabu ambacho kinazungumzia masuala jumla yanayohusiana na elimu ya tajwidi na kimechapishwa mara chungu nzima katika nchi mbalimbali.

Siku kama ya leo miaka 221 iliyopita, yaani sawa na tarehe 23 Februari 1799 Miladia, Napoleon Bonaparte mfalme wa Ufaransa, alianza kuishambulia Sham, ambayo wakati huo iliundwa na nchi za Syria, Jordan, Lebanon na Palestina. Mashambulio ya Bonaparte dhidi ya Misri yalifanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa Uingereza iliyokuwa mkoloni wa Misri. Sababu ya mashambulio ya Napoleon Bonaparte dhidi ya Sham iliyokuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmania, ilikuwa ni hatua ya mfalme wa utawala wa Othmania ya kutangaza vita dhidi ya Ufaransa. Katika mashambulio hayo, na licha ya kwamba awali Bonaparte alipata ushindi, lakini baadaye alilazimika kuacha vita na kurejea kwao kutokana na uungaji mkono wa Uingereza na Urusi kwa utawala wa Othmania na kuharibika hali ya mambo ndani ya Ufaransa.

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita yaani sawa na tarehe 28 Jamaduth-Thani 1302 Hijiria, alifariki dunia alimu na mwanafasihi wa Kiirani Mirza Muhammad bin Sulaiman Tonekaboni. Mbali na Tonekaboni kubobea katika elimu ya fiq'hi, pia alikuwa mtaalamu wa fasihi na mshairi mkubwa katika zama zake. Msomi huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Al Fawaidu fii Usulud Din" na "Qasasul-Ulama."

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita yaani sawa na tarehe 4 Esfand 1323 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi Dorchehi, faqihi na alimu mkubwa. Alizaliwa yapata mwaka 1240 Hijiria Shamsia katika kijiji cha Dorcheh karibu na mkoa wa Isfahan ndani ya familia ya kisomi na uchaji-Mungu. Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi alijifunza kwa baba yake elimu mbalimbali hadi mzazi wake huyo alipofariki dunia, na baada ya hapo akiwa na kaka yake, alifunga safari hadi mjini Isfahan kwa ajili ya kujifunza masomo ya kidini. Licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kimaisha Ayatullah Dorchehi alifanya juhudi kubwa katika kusomea elimu za fiqhi na usulu fiqhi ambapo mwaka 1271 Hijiria Shamsia alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake ya ngazi ya juu. Aliishi mjini Najaf kwa kipindi cha miaka saba akisoma kwa maulama wakubwa kisha akarejea mjini Isfahan na kujishughulisha na ufundishaji wa elimu za Kiislamu ambapo alikuwa na makumi ya wanafunzi mashuhuri. Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi Dorchehi ameacha turathi kama vile kitabu cha 'Kitabut-Twaharah' 'Kitabus-Swalat' na 'Yek Daureh Usul.'

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, yaani sawa na tarehe 23 Februuari 1970 Miladia, mfumo wa utawala nchini Guyana ulibadilishwana kuwa wa jamhuri na siku hii inajulikana nchini humo kuwa Siku ya Jamhuri. Pwani ya Guyana ilivumbuliwa na wavumbuzi wa Kihispania. Mwanzoni mwa karne ya 17 Miladia, Uingereza iliikoloni nchi hiyo hadi mwaka 1966 ilipojipatia uhuru wake.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, yaani sawa na tarehe 4 Esfand 1358 Hijiria Shamsia, Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa Mahakama Kuu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hatua hiyo ilichukuliwa na Imam Ruhullah Khomeini MA baada ya kupasishwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuundwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge. Dakta Beheshti alikuwa miongoni mwa wanafikra wakubwa na shakhsia mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu. Msomi huyo aliuawa kigaidi katika shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO mwaka 1360 Hijria Shamsia.

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, Abdul-Malik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi la Jundullah lenye makao yake huko Pakistan, alitiwa mbaroni katika oparesheni ya kipekee na ngumu ya kiintelijinsia iliyofanywa na maafisa wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi, gaidi huyo katili alikuwa safarini kuelekea nchini Kyrgyzstan akitokea Dubai, Imarati, kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani. Hata hivyo maafisa usalama wa Iran waliokuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo zake waliweza kuitambua ndege iliyokuwa imembeba gaidi huyo na kuisubiri iingie katika anga ya Iran na hivyo kuilazimisha kutua katika uwanja wa ndege wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran na baadaye wakamtia mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Jundullah. Rubani wa ndege hiyo alifanya jitihada kubwa za kutoroka na kutoka nje ya anga ya Iran, lakini alizidiwa nguvu na maafisa usalama wa Iran, na kulazimishwa kuiteremsha. Abdulmalik Rigi alifanya jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kutega na kuripua mabomu katika maeneo ya umma nchini Iran, kuwauwa kwa umati raia pamoja na kuwateka nyara. Rigi hakuwa na huruma hata kwa watu wake wa karibu. Alikiri kwamba alikuwa anapata misaada ya kila namna ikiwemo ya kifedha na kisilaha kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kuliwezesha kundi lake lifanye mauaji ya watu ndani ya Iran hususan katika maeneo ya kusini mashariki mwa Iran na kusababisha mizozo ya kimadhehebu katika maeneo hayo. Gaidi huyo alinyongwa tarehe 30 Khordad mwaka 1389 Hijria Shamsia sawa na tarehe 20 Juni, 2010 Milaadia yaani miezi minne baada ya kutiwa mbaroni. Kukiri huko kwa Rigi kunaonyesha wazi madai ya uwongo ya serikali ya Marekani ya eti kupambana na ugaidi duniani.
