Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (8)
Assalaam Aalaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao
Kipindi chetu kilichopita kilianza kumtambulisha Muhammad bin Muhammad bin Nu’man mashuhuri kwa jina la Sheikh Mufid, mmoja wa Maulamaa na wanazuoni mashuhuri mno katika ulimwengu wa Kishia. Tulisema kuwa, Muhammad bin Muhammad bin Nu’man mashuhuri kwa jina la Sheikh Mufid alizaliwa tarehe 11 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah mwaka 336 Hijria katika kitongoji cha Ukbara kilichoko jirani na Baghdad. Kadhalika tulisema kuwa, kutokana na mchango mkubwa na taathira yake katika kuchanua na kupata mafanikio fikihi na elimu ya teolojia katika ulimwengu wa Kishia, Sheikh Mufid anafahamika kama mbeba bendera mtajika katika uga wa fikra za Kishia na anatambulika pia kama mwasisi wa misingi ya teolojia ya Kishia na mhuishaji wa fikihi iliyochanua na kustawi ya Shia. Sehemu ya nane ya mfululizo huu juma hili itaendelea kumzungumzia mwanazuoni huyu. Endeleeni kunitegea sikio hadi mwisho wa kipindi.
Sheikh Mufid aliandaa mpango na mkakati jumla kwa ajili ya Ijtihad na kunyambua sheria na hukumu za dini kutokana katika vyanzo vyake vikuu, mpango ambao ungali unatumiwa na wasomi na wanazuoni wa elimu ya fikihi. Kama tulivyosema katika kipindi chetu kilichotangulia ni kuwa, kutokana na taathira na mchango wake mkubwa katika uga wa teolojia na fikihi ya Kishia, Sheikh Mufid aliondokea kufahamika kama mwasisi wa teolojia ya Kishia na mhuishaji wa fikihi. Aidha alifahamika pia kama kiongozi wa viongozi wa Mashia.
Sheikh Mufid akiwa na lengo la kujibu shubha na mambo tata, mbali na kuandika makala na vitabu, alikuwa akiandaa vikao vya midahalo na mijadala na kufanya majadiliano na maulamaa wa mapote na makundi ya itikadi mbalimbali. Msomi huyu alikuwa na umahiri mkubwa na alikuwa amebobea kiujuzi kuhusiana na madhehebu mbalimbali za Kiislamu na alikuwa akitumia nguvu zake zote na ujuzi alionao kwa ajili ya kutetea itikadina imani za Uislamu asili.
Moja ya sifa maalumu za Sheikh Mufid ilikuwa ni kuzingatia na kutoa kipaumbele maalumu katika mahitaji ya kifikra ya watu hasa katika zama zile. Daima alikuwa akiwasiliana na watu na kushiriki katika hafla za kielimu. Na kwa kuzingatia kuwa, katika zama hizo yeye ndiye aliyekuwa akitambulika kama Kiongozi wa Madhehebu ya Shia, zilikuwa zikifikia barua za maswali kutoka wa watu wa miji mbalimbali na yeye kwa kutambua mahitaji ya zama zake alikuwa akiandika makala na vitabu. Akthari ya maandiko yake yalikuwa ni majibu ya maswali ya watu au wakazi wa eneo fulani. Mbali na watu wa kawaida waliokuwa wakimwendea Sheikh Mufid kwa ajili ya kutaka kufahamu taklifu zao za kidini, wanazuoni na Maulamaa watajika pia wa zama hizo walikuwa wakimrejea Sheikh Mufid na kumuelezea mahitaji yao mbalimbali ya kielimu. Miongoni mwa vitabu muhimu vya teolojia, fikihi na historia ambavyo aliviandika kwa maombi na matakwa ya Maulamaa wakubwa kama Sheikh Murtadha, Sheikh Radhi na Maulamaa wengine ni Awail al-Maqalaat, Al-Jamal na al-Muqniah.
Kwa hakika sehemu kubwa ya athari za Sheikh Mufid zilikuwa fupi na katika kiwango cha makala. Kiuhakika ni kuwa, kuandika kwa mukhtasari ni miongoni mwa zilizokuwa sifa za dhahiri za athari za Sheikh Mufid. Alimu huyu alikuwa akihesabiwa kuwa mhakiki mahiri na stadi ambaye alikuwa akijiepusha na kukariri ibara, sentensi au maneno bali alikuwa akibainisha maana ya ndani nay a kina kwa kutumia maneno na ibara fupi isipokuwa kama matilaba au maudhui anayoongelea itakuwa tata na inahitaji ubainishaji, maelezo na tafsiri pana zaidi.
Lugha nyepesi na inayoeleweka na wote ni sifa nyingine ya athari na maandiko ya Sheikh Mufid. Katika athari za Sheikh Mufid kunaonekana kwa uchache mno maneno yaliyojifunga na istilahi tata na ngumu. Sheikh Mufid alibainisha masuala muhimu ya teolojia, fikihi, historia na mambo tata ya kielimu kwa namna ambayo inaeleweka kwa matabaka yote ya jamii yaani kwa wanazuoni na watu wa kawaida.
Harakati nyingine ya Sheikh Mufid ilikuwa ni ufundishaji. Alifanya hima kubwa ya kuandaa vikao vya kufundisha kwa ajili ya watafutao elimu na kufanikiwa kulea na kutoa wanazuoni wengi. Miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Mufid ni Sheikh Tusi, Sayyid Murtadha, Sayyid Radhii na Najjashi ambapo kila mmoja wao aliondokea na kuwa alimu na msomi, ingawa katika kipindi chote cha uhai wa Sheikh Mufid hakuna mwanafunzi miongoni mwa wanafuzni wake hao ambaye alikuwa na daraja ya juu kuliko mwalimu wao huyo. Ni katika zama hizo ndipo Sheikh Mufid akajulikana kama kiongozi wa viongozi wa Mashia.
Pamoja na kuwa Sheikh Mufid alijihusisha mno na harakati za kielimu na kijamii, lakini hakughafilika pia na masuala ya kimaanawi na kuilea nafsi katika mambo mazuri. Wanafunzi na watu wake wa karibu siku baada ya siku walikuwa wakishuhudia kuongezeka utukufu wa kimaadili na nuru ya umaanawi katika ujudi na uwepo wa Sheikh Mufid. Historia inaonyesha kuwa, Sheikh Mufid alikuwa akiswali na kufunga sana kama ambavyo alikuwa mwingi wa sadaka. Unyenyekevu na kuvaa mavazi ya kawaida na yasiyo ya kifahari ni mambo yaliyowafanya watu wampende zaidi mwanazuoni huyu aliyesifika kwa ucha Mungu, ukweli na ukarimu. Sheikh Mufid alikuwa akijiweka sawa na watu wa kipato cha chini katika jamii. Sheikh Mufid hakuwa kabisa na raghba, hamu au hamu ya uongozi na jaha.
Sharif Abu Ya’ala mkwe wa Sheikh Mufid anasema: Sheikh Mufid alikuwa akilala sehemu ndogo tu ya usiku na kisha alikuwa akiamka na kuswali na kunong’ona na Mola wake. IMara nyingi alikuwa ima akisoma kitabu, kufundisha au kusoma Qur’ani Tukufu.
Wapenzi wasikilizai hii ni sehemu ndogo tu ya maisha ya Muhammad bin Muhammad bin Nu’man mashuhuri kwa jina la Sheikh Mufid, alimu ambaye licha ya kupita miaka elfu moja, lakini mwangwi wa elimu na maarifa yake ungali unasikika.
Muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulama wa Kishia Katika Uislamu ambacho kitaendelea kumzungumzia Muhammad bin Muhammad bin Nu’man mashuhuri kwa jina la Sheikh Mufid.
Shukrani kwa kunitegea sikio. Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh……