Jumapili, Mei 1, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 23 Rajab, mwaka 1437 Hijiria, sawa na tarehe Mosi Mei mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita na kufuatia maamuzi ya Kongresi ya Kimataifa ya Kazi, siku hii ilitangazwa kuwa siku ya 'Wafanyakazi Duniani, maarufu kwa jina la Mei Mosi.' Siku ya kwanza ya mwezi Mei mwaka 1886 Miladia, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano makubwa mjini Chicago, Marekani kwa lengo la kutaka kupewa haki zao za kimsingi. Katika maandamano hayo washiriki walitaka kuboreshwa mazingira yao ya kazi, kuongezwa kiwango cha mishahara na kuwekwa sheria za usawa za kazi. Hata hivyo maandamano hayo yalikabiliwa na hujuma ya polisi ya Marekani ambapo wafanyakazi wengi waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Ni baada ya tukio hilo ndipo mapendekezo ya awali ya Kongresi ya Kimataifa ya Kazi yakaundwa na kutakiwa kuadhimishwa siku ya kazi duniani maarufu kwa jina la Mei Mosi.
Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Hussein Kuh Kamarei, faqihi na alimu mkubwa wa Kiislamu. Kwa miaka kadhaa Sayyid Kuh Kamarei alisoma elimu kwa maulama wakubwa wa zama zake hususan Sheikh Murtadha Answari. Alikuwa mtaalamu katika elimu ya sheria za Kiislamu na pia Usul Faqhi huku akishika nafasi ya pili baada ya Sheikh Murtadha Answari. Karibu maulama wakubwa 800 walipata kusoma kwa Sayyid Hussein Kuh Kamarei. Msomi huyo ameacha vitabu kadhaa katika taaluma mbalimbali za ibada, sheria za Kiislamu na elimu nyinginezo.
Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, sawa na tarehe Mosi mwezi Mei 1915, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland. Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, alifariki dunia Aram Khachaturian, mtunzi wa nyimbo wa Armenia, Urusi ya zamani. Khachaturian alizaliwa mwaka 1903 mjini Tbilisi, mji mkuu wa zamani wa Armenia na akiwa na umri wa miaka 19 akaelekea Moscow, mji mkuu wa Russia na kuanza kusomea elimu ya mziki. Akiwa katika masomo hayo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa Urusi ya zamani na kutokea kuwa mtaalamu katika utunzi wa mziki na baadaye kuwa mashuhuri katika fani hiyo. Kwa kuzingatia kuwa, tenzi zake zilijikita katika mziki wa asili wa Armenia, aliwavutia watu wengi huku akiwa na ushawishi mkubwa kwa watunzi wengine wa mziki duniani.
Na siku kama leo miaka 37 iliyopita aliuawa shahidi Allamah Morteza Motahhari, alimu, mwanamapambano na msomi mkubwa mtajika wa Kiislamu wa nchini Iran. Morteza Motahhari ambaye pia alikuwa mwanafikra mashuhuri wa mapinduzi ya Kiislamu na pia Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, aliuawa shahidi na wanachama wa kundi lililokuwa likipinga Mapinduzi ya Kiislamu la Furqan. Mauaji hayo yalitekelezwa ikiwa ni ndani ya kipindi kilicho chini ya miezi mitatu tangu kufikiwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ni vyema kuashiria hapa kwambha, Allamah Morteza Motahhari alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa wa kielimu, kidini na kisiasa kabla na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu huku akiwa na nafasi kubwa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi nchini hapa.