Jun 28, 2020 02:32 UTC
  • Jumapili, tarehe 28 Juni, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 6 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Juni 28 mwaka 2020

Miaka 147 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa, Dakta Alexis Carrel, mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa. Msomi huyo alizaliwa katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Alitumia kipindi fulani katika maisha yake kutalii na kuzitembelea nchi mbalimbali zikiwemo za Kiislamu na kushuhudia kwa karibu mila na tamaduni za nchi hizo. Kwa sababu hiyo Dakta Alexis Carrel amesisitiza mno katika maandishi na vitabu vyake juu ya umuhimu na nafasi ya dini na masuala ya kiroho katika maisha ya mwanadamu. Nadharia nyingi za msomi huyo zimo katika kitabu mashuhuri alichokipa jina la "Mwanadamu, Kiumbe Asiyefahamika" ambamo ndani yake anapinga demokrasia ya kimagharibi.

Alexis Carrel

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Juni 1914 aliuawa Franz Ferdinand, mrithi wa kiti cha ufalme wa Austria akiwa pamoja na mkewe, wakati alipokuwa safarini Sarayevo, mji mkuu wa Bosnia Herzegovina ya leo, baada ya kufyatuliwa risasi na mwanachuo mmoja wa Kiserbia. Mara baada ya kutokea shambulio hilo, serikali ya Austria ilitaka ipewe nafasi ya kuingilia kati uchunguzi wa faili la kesi hiyo, jambo lililopingwa na serikali ya Serbia. Amma baada ya kupita mwezi mmoja tu, Austria ilianza kuishambulia Serbia kwa kisingizio hichohicho, na kuanzia mwezi Agosti mwaka huohuo, vikaanza rasmi Vita vya Kwanza vya Dunia baada ya Ujerumani kuamua kuiunga mkono Austria na kuishambulia ardhi ya Ubelgiji.

Franz Ferdinand

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, yaani tarehe 28 Juni mwaka 1957, kituo cha Kiislamu mjini Washington, Marekani kilianzisha rasmi shughuli zake. Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 1949 kwa ushirikiano wa Waislamu wa nchi hiyo na baada ya kuanza ujenzi huo mwaka 1957 kiligeuka na kuwa alama yao ya kidini. Kituo cha Kiislamu cha Washington, mji mkuu wa Marekani kinajumuisha msikiti, shule, maktaba na kadhalika. Kuwa na ratiba mbalimbali ni sababu iliyowafanya Waislamu na wasiokuwa Waislamu kuvutiwa na kituo hicho muhimu. Shughuli za kituo hicho zilipelekea viongozi wa serikali ya nchi hiyo, kupatwa na wahka na hivyo kusimamisha shughuli zake na hata kukifunga kabisa kituo hicho.

Kituo cha Kiislamu mjini Washington

Na siku kama ya leo miaka 14 iliyopita sawa na tarehe 28 Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza. Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina iliyoongozwa na Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi".

Ukanda wa Gaza

 

Tags