Jumatatu, Mei 2, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 24 Rajab 1437 Hijria sawa na Mei 2, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1430 iliyopita, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw). Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa benderea mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.
Siku kama ya leo miaka 1098 iliyopita, Abunassr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. Mwanafalsafa huyo mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.
Na tarehe Pili Mei miaka 496 iliyopita alifariki dunia mchoraji na msanifu majengo maarufu wa Italia Leonardo da Vinci. Alizaliwa mwaka 1452 na umahiri wake ulidhihiri haraka katika nyanja mbalimbali za sanaa. Baada ya kufanya safari katika miji kadhaa ya Italia, mwaka 1506 Da Vinci alielekea Ufaransa na kuwa mchoraji wa Mfalme Louis xii. Aliishi katika kipindi cha mchoraji mwingine mashuhuri wa Italia Michelangelo na wasanii hao wawili mashuhuri walitoa mchango mkubwa katika sanaa ya kipindi cha mwamko wa Ulaya (Renaissance(
Mbali na sanaa, Leonardo da Vinci pia alikuwa mahiri katika taaluma ya uhandisi, mwanasayansi na mtaalamu wa hisabati.
Miongoni mwa michoro maarufu ya Da Vinci ni The "Last Supper" na "Mona Lisa" na kazi yake kubwa zaidi katika usanifu majengo ni jengo la kanisa kuu la Milan.