Ijumaa tarehe 28 Agosti mwaka 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 8 Mfunguo Nne Muharram 1442 Hijria sawa na Agosti 28 mwaka 2020.
Tarehe 8 Muharram mwaka 61 Hijria maji yalimalizika kabisa katika mahema ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala. Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kuwa, katika siku ya nane ya mwezi Muharram mwaka 61 Hijria, Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena.
Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe Umar bin Sa'd akimwambia: Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie, na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake."

Tarehe 28 Agosti 1749 alizaliwa Johann Wolfgang Von Goethe malenga na mwandishi mkubwa wa Kijerumani. Von Goethe alisoma na kujifunza mambo mbalimbali kama uchoraji na kadhalika katika mji aliozaliwa wa Frankfurt nchini Ujerumani, huku akiendelea na masomo yake ya taaluma ya sheria. Von Goethe ambaye anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waenezaji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi, alivutiwa mno na fasihi ya Kifarsi na hasa mashairi ya Hafidh, malenga na mshairi mashuhuri wa Kiirani. Mwandishi huyo wa Kijerumani alikipenda sana Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani pamoja na dini ya Kiislamu. Johann Wolfgang Von Goethe alifariki dunia mwaka 1832.

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita kombora la kwanza la kuvuka mabara lilirushwa hewani na wasomi wa Urusi ya zamani. Siku nne baadaye yaani tarehe 4 Oktoba wasomi wa Urusi walirusha angani satalaiti ya kwanza dunia iliyopewa jina la Sputnik 1 kwa kutumia kombora hilo. Hatua hiyo ilipongezwa kote dunia, na wasomi hao walitangaza kuwa watatuma mwanadamu angani katika kipindi cha chini ya miaka mitatu na kwamba watatuma chombo cha anga katika mwezi miaka mitano baadaye. Wasomi hao wa Urusi walitimiza hadi zao.

Siku kama hii ya leo miaka 57 iliyopita yaani Agosti 28, 1963, Martin Luther King mwanaharakati mkubwa wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani, alihutubia umati mkubwa wa watu waliofanya mgomo wa kutaka wapewe haki ya kijamii nchini humo. Luther King ambaye ni Mmarekani mweusi alihutubia umati huo kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Lincoln mjini Washington. Kwenye mkutano huo, Martin Luther King alieleza ndoto yake ya kuwa huru Wamarekani weusi.

Na katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhimein na Najaf nchini Iraq. Miongoni mwa athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko mjini Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake. Maktaba hiyo ina vitabu zaidi laki tatu.
