May 04, 2016 06:02 UTC
  • Jumatano, Mei 4, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 26 Rajab 1437 Hijria sawa na May 4, 2016.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia wakati Waislamu walipokuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka. Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Shiibi Abi Twalib akimlinda na kumhami mtukufu huyo mbele ya adha za washirikina. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kikuraishi.

Siku kama ya leo miaka 1010 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria, Khaja Abdullah Ansari. Khaja Ansari alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 83 katika mji wa Herat nchini Afghanistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mahabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Chama cha National Socialism cha Ujerumani mashuhuri kwa jina la Chama cha Kinazi, kilivunjwa rasmi. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa kidikteta, ukandamizaji na mabavu wa chama hicho ambacho kilishika hatamu 1932 nchini Ujerumani, kikafikia tamati. Chama cha Kinazi kiliundwa Oktoba 1920 baada ya kushamiri harakati ya kisiasa ya Munich. Chama hicho kilikuwa na lengo la kuyaunganisha mataifa yanayozungumza Kijerumani na kuanzisha dola moja lenye nguvu litakaloweza kupanua mipaka yake. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia chama hicho cha Kinazi kilisambaratika na kuvunjwa mbali.

Na tarehe 15 Ordibehesht miaka 73 iliyopita mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhullah Khomeini alitoa taarifa yake ya kwanza ya kisiasa akiwa na umri wa miaka 42. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini aliwalingania wananchi kufanya qiyamu na kuanzisha harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Katika taarifa hiyo ya kisiasa Imam Khomeini alichunguza hali ya miaka iliyopita, kipindi hicho na mustakbali wa wananchi na kusisitiza kuwa, kusimama na kufanya harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiyo njia peke ya kurekebisha dunia.