Jumapili, tarehe 4 Oktoba, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 16 Safar 1442 Hijria sawa na Oktoba 4 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru wake. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukuendelea kwa muda mrefu baada ya Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.
Katika siku kama ya leo miaka 92 iliyopita tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita Imam Khomeini Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu alihama kutoka Iraq na kuelekea Paris Ufaransa. Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu alichukua uamuzi huo wa kufanya hijra hiyo ya kihistoria pale utawala wa zamani wa Iraq ulipokuwa ukijiandaa kuzuia mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikifanya kila linalowezekana ili kulinda uhusiano wao na utawala wa Shah ulimtaka Imam kuacha kufanya shughuli zozote za kisiasa na kipropaganda dhidi ya utawala wa Shah. Hatimaye katika siku kama ya leo Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu alielekea Paris Ufaransa kufuatia kushadidi mashinikizo ya utawala wa Baath wa Iraq na baada ya Kuwait kupinga Imam kuelekea nchini humo.