Jumamosi, 24 oktoba, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 24 Oktoba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1100 iliyopita, Ali bin Muhammad Tanukhi alimu, mwandishi na malenga mashuhuri wa karne ya nne Hijria aliaga dunia huko katika mji wa Basra, kusini mwa Iraq akiwa na umri wa miaka 64. Ali Tanukhi alizaliwa huko Antakya mashariki mwa Uturuki ya leo na akiwa kijana alielekea Baghdad na kuasisi makazi yake. Ali bin Muhammad Tanukhi alikuwa mahiri katika lugha na fasihi ya Kiarabu na kuwa miongoni mwa malenga mashuhuri wa zama hizo. Mbali na kutunga diwani yake ya mashairi ambayo imebaki kama kumbukumbu hadi hii leo, Tanukhi aliandika pia vitabu mbalimbali kimojawapo kikiwa ni kile alichokipa jina la al Arudh.***
Tarehe 24 Oktoba miaka 91 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street. Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake. Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao. ***
Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa. Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo. Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani. ***
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Iran ilifanikiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa, mlango wa kujiunga na umoja huo uko wazi kwa mataifa yote yanayopenda amani na ambayo yanakubaliana na sheria na maaamuzi ya taasisi hiyo. Nchini Iran, Umoja wa Mataifa una jumla ya ofisi 14 za uwakilishi na utendaji. ***
Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, vita vya nne baina ya Waarabu na Israel vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Ramadhani vilifikia tamati. Tarehe 6 Oktoba 1973 Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri akiwa na lengo la kufidia kushindwa katika vita vya Waarabu na Israel mwaka 1967, alifanya mashambulio ya kushtukiza katika ngome za Israel katika Kanali ya Suez. Muda mchache baada ya mashambulio hayo, wanajeshi wa Syria nao walifanya mashambulio katika miinuko ya Golan ambayo ilikaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya mwaka 1967 na kufanikiwa kuwatimua wanajeshi wote wa utawala huo haramu kutoka katika maeneo waliokuwa wakiyadhibiti. ***
Na miaka 28 iliyopita, aliaga dunia Abul Qassim Halat mshairi, mchekeshaji na mtarjumi wa zama hizi wa Kiirani. Alianza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 16 na akaondokea kubobea katika mashairi ya vichekesho. Malengo huyo alikuwa akizifahamu vyema lugha za Kifarsi, Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu. Miongoni mwa athari zake muhimu ni tarjama ya maneno yenye thamani kubwa ya Bwana Mtume (saw) na Imam Ali bin Abi Talib (as). Abul Qassim Halat ameacha athari nyingi zenye thamani kubwa katika uga wa maishairi.