May 05, 2016 00:10 UTC
  • Alhamisi May, 5 2016

Leo ni Akhamisi tarehe 27 Rajab 1437 Hijria sawa na May 5, 2016.


Siku kama ya leo miaka 1450 iliyopita, Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad Mustafa SAW alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad SAW alikuwa amefikisha miaka 40 katika umri wake uliojaa baraka. Mtume Muhammad SAW alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad SAW kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa kaskazini mwa Makka. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumpa bishara ya kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo Mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.


Katika tarehe kama ya leo miaka 970 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa mfasiri mkubwa wa Qur'ani na faqihi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Fakihi na mwanafasihi huyo wa Kiislamu aliishi kwa miaka mingi mjini Makka jirani na nyumba ya Allah al-Kaaba na kwa msingi huu alikuwa mashuhuri kwa jina la Jarullah yaani jirani wa Mwenyezi Mungu. Alipewa heshima maalum na wataalamu pamoja na wanazuoni katika zama zake na ameandika vitabu vingi nikiwemo vya Asasul Balagha na Muqaddimatul Adab". Kitabu muhimu zaidi cha Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al Kash'shaf. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 538 Hijria.


Katika siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Alipata elimu ya msingi kwa baba yake na baadaye alipata elimu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kufanikiwa kulea wanafunzi wengi na vilevile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.


Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, alizaliwa Karl Heinrich Marx mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi. Karl Marx awali alianza kusomea taaluma ya sheria na baadaye historia na falsafa. Mwanafalsafa huyo wa Kijerumani kwa muda fulani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu alichokipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti." Miaka miwili baadaye Marx alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa na hadi mwishoni mwa maisha yake makazi yake yalikuwa nchini Uingereza.


Miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na siku ya Ijumaa usiku wa tarehe 27 Rajab 1415 Hijria, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa mara ya kwanza. Matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa kwa muda wa nusu saa tu usiku, na yalifunguliwa kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa Utume, Bwana wetu Muhammad (SAW).


Lengo la kuasisiwa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikisha sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wanaodhulumiwa wa bara la Afrika, kuelimisha na kufichua njama za ubeberu wa kimataifa dhidi ya bara hilo.