Jumamosi, 7 Novemba, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 21 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawana tarehe 7 Novemba 2020 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 199 iliyopita sawa na tarehe 21 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal, mji wa Yerevan ulidhibitiwa na kutwaliwa na majeshi ya Russia. Tukio hilo lilijiri wakati wa vita vya pili kati ya Iran na Russia. Mji huo ulitekwa katika zama za Fat'h-Ali Shah Qajar na kisha kukabidhiwa kwa Russia. Matokeo ya kushindwa huko kukawa ni kutiwa saini makubaliano yanaliyojulikana kama Mkataba wa Torkamanchay. Kwa mujibu wa mkataba huo na kutokana na udhaifu wa Shah Qajar, sehemu kubwa ya ardhi ya kaskazini mwa Azerbaijan na Caucasia iliyokuwa sehemu ya Iran ikaunganishwa na Russia. ***
Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland. Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne. Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934. ***
Katika siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, Leo Trotsky mmoja wa viongozi wakuu wa mapinduzi nchini Russia alizaliwa. Alibaidishwa Siberia mara mbili katika zama za utawala wa Tsar kutokana na kujihusisha kwake na harakati za mapinduzi. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Russia, Trotsky alirejea nchini Russia. Hiyo ilikuwa mwaka 1917 na akapatiwa wadhifa wa Kamishna wa Masuala ya Kigeni. Mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa Kamishna wa Vita ambapo baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani na Ujerumani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, alianzisha mapambano dhidi ya wapinzani wa mapinduzi. Hata hivyo baada ya kuaga dunia Lenin, mwanamapinduzi huyo alishindwa katika vita vyake na Joseph Stalin ambapo mwakka 1925 alibaidishiwa Siberia na baadayye huuko Uturukki. Hatiomaye aliuawa mwaka 1940 huko Mexico na makachero wa Lenin. ***
Miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Albert Camus mwandishi mashuhuri wa Ufaransa. Licha ya kuwa familia yake ilikuwa masikini, lakini kutokana na kipaji, bidii pamoja na irada thabiti aliyokuwa nayo, Camus alifanikiwa kupata umashuhuri mkubwa. Mwandishi huyo wa Kifaransa ana vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Firs Man, The Fall, The Stranger na A Happy Death. ***
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, ilianza kusikilizwa kesi ya Dakta Muhammad Musaddegh Waziri Mkuu wa wananchi wa Iran. Miezi miwili kabla Musaddegh alikuwa ameondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Marekani na Uingereza. Kosa lake kubwa lilikuwa ni kuifanya sekta ya mafuta ya Iran kuwa mali ya taifa akisaidiwa na vikosi vya kidini na himaya ya wananchi. Hatimaye kutokana na uzee, mahakama ya kijeshi ya Shah ilimhukumu Musaddegh miaka mitatu jela. ***
Na siku kama ya leo miaka 64 iliyopita vita vya mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa. Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la mfereji huo. Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdulnassir, kuutaifisha mfereji huo. ***