May 06, 2016 01:29 UTC
  • Ijumaa, Mosi 6, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Rajab 1437 Hijria sawa na May 6, 2016.

Tarehe 28 Rajab miaka 1377 iliyopita msafara wa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as) ulianza safari ya kuondoka katika mji mtakatifu wa Madina. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kifo cha Muawiya bin Abi Sufian tarehe 15 mwezi huu wa Rajab na kushika hatamu mwanaye fasiki na muovu zaidi, Yazid bin Muawiya. Baada tu ya kushika hatamu, Yazid alimtaka gavana wake wa Madina amlazimishe Imam Hussein kutoa mko wa utiifu, lakini Imam alikataa akisema kuwa Yazid ni mtu fasiki, muovu na mpotevu. Aliondoka Madina akiwa pamoja na watu wa familia ya Mtume na masahaba zake na kuelekea Makka. Katika wasia wake aliomwachia ndugu yake, Muhammad al Hanafiyya, Imam Hussein alisema: Ninasimama kwa ajili ya kurekebisha Umma wa babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu ya kufuata njia ya babu na baba yangu…".

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa jiografia na msomi mkubwa wa Kijerumani Alexander Humboldt. Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa.

Tarehe 6 Mei miaka 134 iliyopita ilitangazwa habari ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu. Vijidudu hivyo vilgunduliwa na mtaalamu wa Ujerumani, Robert Heinrich Koch. Mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vimeua zaidi ya watu bilioni moja, wiki mbili kabla. Baadaye Prf Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kujitokeza wakati mwafaka.

Mbali na kugundua vijidudu maradhi vya kifua kikuu, Prf Robert Koch pia aligundua vijidudu maradhi vya kipindupindu katika safari zake katika nchi za Misri na India na mwaka 1906 alitengeneza dawa ya Atoxyl inayoshabihiana na Quinine. Prf Robert Koch anatambuliwa kuwa mtaalamu mkubwa zaidi wa vijidudu maradhi duniani baada ya Luis Pastore na alitoa huduma kubwa sana kwa elimu na sayansi ambayo kamwe haitasahaulika.

Na siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, inayosadiana na tarahe 28 Rajab 1337 Hijria, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa Kiirani. Allamah Yazdi alijipata elimu katika mji wa Najaf nchini Iraq kutoka kwa maulamaa kadhaa mashuhuri akiwemo Mirzai Shirazi na hatimaye kufikia daraja ya Ijtihad. Msomi huyo aliandika vitabu vingi, kikiwemo kitabu cha 'al U'rwatul Wuthqa.