Jan 05, 2021 02:45 UTC
  • Jumanne tarehe 5 Januari 2021

Leo ni Jumanne tarehe 21 Jamadil Awwal 1442 Hijria sawa na Januri 5 mwaka 2021.

Siku kama ya aleo miaka 1122 iliyopita sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijiria, kwa mujibu wa nukuu za wanahistoria alizaliwa Abu Jaafar Ahmad bin Ibrahim Qiravani, katika mji wa Shirvan ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Msomi huyo alijulikana kwa jina maarufu la Ibn Jazzar, na alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu mema na aliandika kitabu kiitwacho "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini." Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu 20. Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.

Ibn Jazzar

Siku kama ya leo miaka 330 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya. Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne. Moja kati ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, inahifadhiwa kwenye makumbusho ya Benki ya Stockholm.

Noti ya kwanza huko Ulaya  

Miaka 212 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa Dardanelles (Treaty of the Dardanelles) baina ya utawala wa Othmania na Uingereza. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uingereza iliahidi kuondoka katika ardhi zote zilizokuwa chini ya utawala wa Othmania ikiwemo Misri na kuhitimisha ukaliaji mabavu wa ardhi hizo. Mkabala wake, utawala wa Othmania uliahidi kutambua rasmi haki za kibalozi za Uingereza katika ardhi za utawala wa Othmania. 

Picha ya satalaiti ya Dardanelles

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita alifariki dunia Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi na kutokuwa na wizani. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".

Nima Yushij  

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita kulitokea hamasa ya mashahidi wa Huweize iliyoongozwa na Shahidi Alamul Huda katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Iran. Mwezi Dei mwaka 1359 Hijria Shamsia na baada ya jeshi la Iran ya Kiislamu kuvishinda vikosi zaidi ya viwili vya jeshi la Iraq huko kusini mwa eneo la Susangerd, kundi moja la Jeshi al Sepah la Ahwaz huko kusini mwa Iran lilitumwa katika mji wa Huweize kwenda kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya Iraq. Hata hivyo kutokana na kuchelewa kufika zana na hujuma kubwa ya Iraq, jeshi la Iran lililazimika kurudi nyuma. Wakati huo zaidi ya wapiganaji mia moja wa Jeshi la Sepah, wapiganaji wa kujitolea na wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi waaminifu wa Imam Khomeini wakiongozwa na Sayyid Muhammad Hussein Alamul Huda walibakia katika mji huo wa Huweize wakipambana na adui na wakauawa shahidi. Baadaye jeshi la Iraq liliuvunja kabisa mji wa Huweize na kuusawazisha na ardhi. Pamoja na hayo ushujaa wa vijana hao shupavu wa Iran waliosabilia roho zao kulinda ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu umebakia hai katika historia ya Iran. 

Kumbukumbu ya mashahidi wa Huweize

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1985, utawala wa Kizayuni wa Israel uliwachukua maelfu ya Mayahudi wa Ethiopia "Mafalasha' kupitia ardhi ya Sudan. Mafalasha hao ambao idadi yao ilikuwa watu 8,000 walipelekwa huko katika ardi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina. Nchi za Kiarabu ziliikasirikia Sudan kwa kushirikiana na Israel katika kuwahamisha Mayahudi wa Kiethiopia na kuwapeleka Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

Na miaka 6 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Eusébio da Silva Ferreira, nyota wa mpira wa miguu nchini Ureno. Alizaliwa Januari 25 mwaka 1942 huko Maputo, Msumbiji. Alionyesha hamu na kipaji cha hali ya juu ya kusakata kabumbu akiwa shuleni. Alikuwa nyota katika timu ya taifa ya soka ya Ureno katika zama zake. Alifunga jumla ya magoli 733 katika mechi za kimataifa 745 alizocheza na anahesabiwa kuwa, mmoja wa wafungaji bora duniani katika ulimwengu wa soka. Mwaka 1956 Eusébio da Silva Ferreira alishinda tuzo ya mchezaji bora barani Ulaya. Aidha katika miaka ya 1970 na 1973 alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa soka nchini Ureno. Baada ya kuugua moyo kwa muda na kulazwa mara kadhaa hospitali hatimaye Eusébio da Silva Ferreira aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 71. 

Eusebio