Jan 06, 2021 02:45 UTC
  • Jumatano, 06 Januari, 2021

Leo ni Jumatano tarehe 22 Jamadil Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 6 Januari 2021.

Katika siku kama ya leo 160 iliyopita ilianzishwa nchi ya Romania. Mpango wa kuasisiwa nchi ya Romania ulibuniwa tarehe 13 Disemba 1859 kwa kuunganishwa miji miwili midogo ya Moldavia na Wallachia. Miaka miwili baadaye majimbo na miji mingine ilijiunga na umoja huo na kuundwa nchi ya Romania.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, aliaga dunia Theodore Roosevelt Rais wa zamani wa Marekani. Theodore Roosevelt Rais wa 26 wa Marekani alizaliwa Oktoba 27 mwaka 1857. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana. Alikuwa mwanachama wa chama cha Republican. Alikuwa Makamu wa Rais na baada ya kuuawa William McKinley aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Theodore Roosevelt akawa Rais wa muda wa nchi hiyo. Mwaka 1901 alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani. Mwanzoni mwa utawala wake, Theodore Roosevelt aliimarisha uwepo wa vikosi vya Marekani nchini Cuba iliyokuwa ikikaliwa kwa mabavu na Washington na akaitangaza rasmi nchi hiyo kuwa chini ya mamlaka na himaya ya Marekani.

Theodore Roosevelt

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, Rezakhan Pahlavi mfalme wa wakati huo wa Iran, alitoa amri ya kuwazuia wanawake kuvaa aina yoyote ya vazi la Kiislamu yaani hijabu hapa nchini. Amri hiyo ilitolewa baada ya utekelezwaji wa mpango wa kubadili mavazi ya kiume kwa lengo la kufuta kabisa athari za Kiislamu na kufuata kibubusa siasa za madola ya Magharibi. Kabla ya hapo mfalme huyo alikuwa amefanya safari nchini Uturuki na kukutana na Rais wa nchi hiyo Mustafa Kemal Atatürk, ambaye naye alikuwa amepiga marufuku vazi la Kiislamu la mwanamke wa Kiislamu hijabu nchini humo kwa kufuata siasa za Magharibi. Kufuatia hatua hiyo vibaraka wa mfalme huyo walianza kuwafanyia dhihaka na kuwadunisha wanawake wa Kiislamu waliokuwa wakivaa vazi hilo la heshima.

Rezakhan Pahlavi

Tarehe 17 Dei miaka 43 iliyopita wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi. Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa shakhsia huyo. Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran.

Imam Khomeini

Na siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani