Jan 09, 2021 12:25 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

 

Kipindi chetu kilichopita kiliangazia kwa mukhtasari maisha na historia ya Ibn Shahr Ashoub, alimu na msomi mwingine wa Kiislamu aliyeishi katika karne ya sita Hijria. Tulisema kuwa Ibn Shahr Ashoub alizaliwa mwezi wa Jamadu Thani mwaka 488 Hijria na akiwa na umri wa miaka 8 tayari alikuwa amehifadhi kwa moyo Qur'ani yote. Kadhalika tulitaja baadhi ya vitabu vyake na  mashuhuri zaidi ni Manaqib Aal Abi Talib. Tulikamilisha kipindi chetu cha juma lililopita kwa kueleza kuwa, Ibn Shahr Ashoub amezikwa huko Halab, Syria. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 18 ya mfululizo huu kitamzungumzia Sayyid Ibn Tawus. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

 

Sayyid Ibn Tawus ni moja ya fakhari kubwa za ulimwengu wa Kishia na Uislamu. Alimu huyu alifahamika mno kama mwalimu wa akhlaq na Irfan. Msomi huyo wa Kishia ndiye mwandishi wa kitabu cha Luhuf Ala Qatla al-Tufuf ambacho kinaeleza masaibu na mauaji dhidi ya Imam Hussein as na masahaba zake katika ardhi ya Karbala yaliyotokea mwaka 61 Hijria. Ibn Tawus aliishi katika zama za utawala wa Moghul mjini Baghdad ambapo kutokana na taqwa na uchaji Mungu wake pamoja na hali ya kiirfani aliyokuwa nayo alitambulika kwa lakabu ya Jamalul Arifin. Radhiuddin Ali bin Mussa bin Jaafar Ibn Tawus ni katika wajukuu wa Imam Hassan al-Mujtaba na Imam Sajjad AS na alizaliwa tarehe 15 Mfunguo Nne Muharram 589 Hijria katika mji wa Hillah, nchini Iraq. Babu yake wa saba ni Muhammad bin Is'haq.

 

Hillah mahala alipozaliwa Ibn Tawus ni moja ya miji ya Iraq na makao makuu ya mji wa Babul. Mji huu upo katika pembe za Mto Furat yapata kilomita 90 hivi kusini mwa mji mkuu Baghdad na katika njia ya Baghdad kuelekea Najaf. Kwa karne ya tano na ya sita Hijria, Hillah ulikuwa moja ya miji yenye madhari nzuri zaidi ya Iraq ambapo wafanyabiashara, maulamaa na washairi wengi walikuwa wakifanya safari kuelekea katika mji huo. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya sita hadi ya saba Hijria, mji wa Hillah ulikuwa kitovu cha elimu na ijtihadi na kituo cha Chuo Kikuu cha Kiislamu (Hawza) cha Shia. Baadaye Hawza ya Shia ikahamisiwa Karbala na baadaye Najaf.

Awali na mwanzoni mwa masomo yake Ibn Tawus alisoma katika mji wa Hillah ambapo alihudhuria darsa na masomo ya baba yake na babu yake waliokuwa wasomi mahiri. Baadaye akiwa na lengo la kustafidi na elimu ya maulamaa wengine alifanya safari katika miji mingine. Awali alielekea katika mji wa Kadhmein. Baada ya muda akaoa na kukamilisha nusu ya dini yake na akauchagua mji wa Baghdad kuwa makazi yake.

Alibakia katika mji huo kwa muda wa miaka 15 na kujihusisha na kufundisha na kulea wanafunzi. Kuna kipindi cha miaka mitatu pia ambacho aliishi jirani na haramu ya Imam Ridha AS mjini Mash’had Iran ambapo baadaye alihajiri na kuelekea Najaf na Karbalka ambapo aliishi pia katika kila katika moja ya miji hiyo kwa muda wa miaka mitatu.

Mahala alipozikwa Ibn Tawus katika mji wa Hillah Iraq

 

 

Licha ya kuwa, Ibn Tawus anahesabiwa kuwa msomi mwenye nadharia katika elimu ya fikihi, lakini hakujiunga na uwanja wa kutoa fatuwa. Msomi huyu ana kitabu kimoja tu cha fikihi kinachohusiana na hukumu za Swala. Ibn Tawus alielekeza zaidi nguvu zakke katika uga wa masuala ya akhlaq na maanawi ambapo athari na vitabu vyake vingi pia vinahusiana na maudhui hizo. Miongoni mwa vitabu vyake hivyo ni: Misbahul Al-Mujtahid, Muhaasabatun Nafs na Iqbaalul A’mal. Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyu ni al-luhuf alaa Qatla al-Tufuf. Tofauti na vitabu vingine vya Sayyid Ibn Tawus ambavyo vilihusiana na masuala ya dua na ziyara, kitabu hiki kimeelekea upande wa historia.

Kitabu hiki kinabaisha harakati na mapinduzi ya Imam Hussein kuanzia alipoondoka Madina hadi kurejea kwa mateka wa Karbala. Miongoni mwa sifa za kipekee za kitabu hiki ni kwamba, kimepangiliwa katika sura ya visa. 

Kitabu cha Ibn Tawus kimepokewa kwa wingi na kinapendwa mno ambapo kimetarjumiwa mara nyingi katika lugha mbalimbali ikiwemo ya Kiswahili. Aidha  kimefafanuliwa, kufupishwa na hata kupangiliwa ambapo hii leo kitabu hiki kinahesabiwa kuwa chenye itibari kubwa katika kusimulia mauaji ya Karbala.

Tukichunguza na kutathmini hali ya kisiasa, kidini na kiutamaduni ya Ulimwengu wa Kiislamu katika karne ya 7 Hijria tutaona kuwa, kipindi hiki kilisadifiana na matukio ambayo yalikuwa na umuhimu mkubwa katika hatima na majaaliwa ya Uislamu. Hujuma na mashambulio ya mara kwa mara ya Mongolia dhidi ya ardhi za Kiislamu na kuanguka ukhalifa na utawala wa Bani Abbas yalikuwa matukio muhimu zaidi katika kipindi hiki cha historia ambacho kilikabiliwa na migogoro ya kifikra, kiutamaduni na kimaadili katika jamii ya Kiislamu.

Kitabu cha Ibn Tawus cha Luhuf alaa Qatla al-Tufuf

 

Katika mazingira haya, Maulamaa wa Kiislamu ambao kwa miaka mingi walikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa Bani Abbas na kukabiliwa na mbinyo, walifanya hima maradufu kwa ajili ya kulinda mipaka ya kiutamaduni na kiitikadi ya Uislamu na hivyo wakitegemea auni na msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu waliweza kubadilisha vitisho vilivyotokana na hujuma ya Mongolia dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu na kuvifanya kuwa fursa ya kukarabati misingi ya ustaarabu wa Kiislamu.

Kwa utaratibu huo Mashia katika karne ya 7 Hijria waliweza kupiga hatua kubwa katika ustawi wa kiutamaduni na kijamii hususan katika mji wa Baghdad.  Hapana shaka kuwa, Radhiuddin Sayyid Bin Tawus alikuwa na nafasi kubwa na athirifu katika ustawi na kuchanua huku kwa ustaarabu na utamaduni wa Kiislamu.

 

Kueneza utamaduni wa dua, ni huduma nyingine ya thamani iliyotolewa na Ibn Tawus kwa jamii ya Kishia. Dua baina ya madhehebu mbalimbali za Kiislamu zilikuwa zikizingatiwa zaidi na mafundisho ya madehebu ya kishia, kiasi kwamba, hilo linahesabiwa kuwa sehemu isiyotenganishika na maktaba ya Ushia. Dua ni njia ya moja kwa moja ya mawasiliano baina ya mja na Mola wake mlezi, ambapo pengine katika mtazamo wa kwanza mtu anaweza kuona kuwa ni jibu pekee tu kwa ajili ya hitajio fulani la ndani la mwanadamu. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, haya mawasiliano, kuzungumza na kunong’ona na Mwenyezi Mungu endapo yatafanyika kwa njia sahihi, itakuwa ni njia nyoofu kwa ajili ya kumlea mwanadamu kamili na kujenga utamaduni na ustaarabu wake stahiki na unaofaa.

Hatimaye Ibn Tawus aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 75 baada ya kuishi maisha yaliyojaa thamani. Mwanazuoni huyu aliaga dunia mjini Baghdad.  Maili yake ilisafirishwa na kwenda kuzikwa mjini Najaf katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib AS. Ibn Tawus aliondoka duniani katika hali ambayo, wasomi na wanazuoni wote wa zama hizo walikuwa wakimtambua kama, mchaji Mungu, mtu aliyeipa mgongo dunia na walikuwa wakitoa heshima na taadhima mbele ya elimu na maarifa yake.

Kaburi la Ibn Tawus

 

Hii leo licha ya kupita karne nyingi tangu alipoaga dunia alimu huyu mkubwa, ulimwengu wa elimu unamtaja kwa fahari na heshima kubwa huku kitabu cha Ibn Tawus cha Luhuf alaa Qatla al-Tufuf kikiwa kingali kiunganishi cha nyoyo za vipenzi na maashiki wa Ahl-Baiti AS na mwanga wa tukio la Ashura.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tukutane tena juma lijalo saa na wakati kama wa leo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh