Jan 16, 2021 03:42 UTC
  • Jumamosi, 16 Januari, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe Pili Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria sawa na tarehe 16 Januari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 783 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na msomi wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo. Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia. Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alifundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi. Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi; na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw). ***

Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas

 

Katika siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo. Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas. Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico. ***

 

Miaka 65 iliyopita yaani tarehe 27 Dey 1334 Hijria Shamsia, Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika kipindi cha utawala wa Shah hapa nchini Iran. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu. ***

Sayyid Mujtaba Navvab Safavi

 

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita alifariki dunia mtunzi wa nyimbo mwenye asili ya Italia kwa jina la Arturo Toscanini. Toscanini alizaliwa mwaka 1867 na alianza kupenda muziki akiwa kijana. Arturo Toscanini alikuwa kiongozi wa bendi baada ya kufanya mazoezi mengi na kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. Aidha alipata umashuhuri kutokana uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi na kuwa makini katika utunzi wa nyimbo. Toscanini aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 yaani miaka mitatu baada ya kustaafu kazi ya muziki. ***

Arturo Toscanini

 

Na miaka 20 iliyopita katika siku kkama ya leo ya Januari 16, Rais Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya. Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya kiongozi huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais Laurent Desire Kabila. Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga na kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi vya askari aliokuwa akiwaongoza kuuteka mji wa Kinshasa na kumlazimisha Mobutu Sese Seko, rais wa wakati huo wa Zaire ya zamani kukimbilia nje ya nchi. Tarehe 26 Januari yaani siku nane tu baada kutangazwa kifo cha Rais Laurent Desire Kabila, mwanawe yaani Joseph Kabila alishika hatamu za uongozi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na hivyo kumrithi baba yake.***

Laurent Desire Kabila.