May 07, 2016 23:22 UTC
  • Jumapili, 8 Mei 2016

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Shaban, mwaka 1437 Hijiria, sawa na tarehe 8 Mei mwaka 2016 Miladia.

Leo ni tarehe Mosi Shaban, mwezi wa ibada na msamaha wa Mwenyezi Mungu. Mtukufu Mtume Muhammad (saw) aliutaja mwezi huu kuwa ni wake yeye na wenye fadhila nyingi. Kwa ajili hiyo Nabii wa Allah amehusia kufanya ibada ndani yake hususan kufunga saumu. Hii ni kwa kuwa mwezi huu ni mwanzo wa maandalizi ya kuingia katika mwezi wenye baraka wa Ramadhan ambao ni kwa ajili ya wanadamu. Ndani ya mwezi huu wa Shaban, kuna matukio muhimu kama vile kuzaliwa Imam Hussein (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) na kuzaliwa pia Imam Mahdi (as) ambaye walimwengu wanamsubiri kwa ajili ya kuijaza dunia uadilifu na usawa.
Tarehe nane ya kila mwezi Mei inatambuliwa kuwa siku ya Msalaba Mwekundu au Hilali Nyekundu. Msalaba Mwekundu ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa kwa ajili ya kutuliza machungu ya wanadamu na kulinda maendeleo ya sekta ya afya ya kijamii kwa mujibu wa mkataba wa Geneva, Uswisi hapo mwaka 1864 Miladia. Jean Henri Dunant raia wa Uswisi, alikuwa na nafasi kubwa katika kuundwa shirika hilo la kimataifa. Hii ni kwa kuwa mwaka 1862 alitoa pendekezo la kusaidiwa wagonjwa na majeruhi wa kijeshi, pendekezo ambalo lilipokelewa na asasi za masuala ya misaada ya kibinaadamu na kukubaliwa hapo baadaye na kongamano la kimataifa mjini Geneva mwaka 1864. Ni baada ya hapo ndipo shirika hilo la Msalaba Mwekundu likaundwa na kuanza kuenea duniani. Katika nchi za Kiislamu shirika hilo linaitwa kwa jina la Hilali Nyekundu.
Siku kama ya leo miaka 744 iliyopita, alifariki dunia Ghiyathud-Din Abu Mudhaffar Abdul-Karim Bin Ahmad, aliyekuwa akiitwa kwa lakabu ya 'Ibn Taus' faqihi na msomi mkubwa wa fasihi wa karne ya Nane Hijiria, huko mjini Kadhimain, nchini Iraq. Ibn Taus alizaliwa mwaka 648 Hijiria. Akiwa na miaka 11 alikuwa tayari amehifadhi Qur'ani yote na baada ya hapo akaanza kusomea elimu ya fasihi na sheria za Kiislamu mbele ya walimu wakubwa wa enzi zake. Ibn Taus ameandika vitabu kadhaa hususan katika uwanja wa lugha ya Kiarabu.
Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, Antoine Lavoisier msomi wa Ufaransa alinyongwa kufuatia kujiri harakati ya mapinduzi makubwa ya nchi hiyo. Lavoisier alikuwa mvumbuzi na msomi mashuhuri wa Ufaransa huku akiwa pia mwanzilishi wa kanuni ya kielimu ya elimu ya kemia. Licha ya kuhitimu awali masomo yake ya sheria, lakini kutokana na kwamba alipendelea sana elimu ya sayansi akaamua kuingia uwanja huo. Akiwa na miaka 25 alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Kifalme cha Sayansi. Katika uwanja huo alifanikiwa kuvumbua gesi ya Oxygen na umuhimu wa matumizi na pia kuvumbua muundo wa hewa. Antoine Lavoisier ndiye msomi wa kwanza aliyethibitisha kuwa joto la mwili linatokana na mmeng'enyo wa sukari mwilini na kwa ajili hiyo akatambuliwa kuwa mwasisi wa elimu ya tiba na biokemia. Itafahamika kuwa, baada ya kujiri mapinduzi makubwa ya Ufaransa kila mtu aliyekuwa na mahusiano na utawala wa kifalme wa nchi hiyo alikamatwa na kuhukumiwa. Ni kwa msingi huo ndipo Antoine Lavoisier akatiwa mbaroni na kisha kuhukumiwa na kunyongwa katika siku kama ya leo mwaka 1794 Miladia akiwa na umri wa miaka 51.
Na siku kama ya leo miaka 171 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 Sheikh Muhammad Hassan Najafi, maarufu kwa jina la 'Swahib Jawaahir' mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu. Swahib Jawaahir alifanya utafiti mkubwa wa elimu ya sheria za Kiislamu na kufanikiwa kuainisha kanuni na mitazamo yake mizuri katika uwanja huo. Alifanikiwa kufikia daraja la ijtihadi akiwa na umri wa miaka 25 na kuandika kitabu cha 'Jawaahirul-Kalam akiwa na umri huo.' Swahib Jawaahir ameacha vitabu kadhaa katika sheria za Kiislamu.