May 09, 2016 01:30 UTC
  • Jumatatu, Mei 9, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe Pili Shaaban 1437 Hijria sawa na Mei 9, 2016.

Siku kama ya leo miaka 363 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22. Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Issa Isfahani. Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu. Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe, Nur Jahan.

Siku kama ya leo miaka 1041 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari katika mji wa Herat nchini Afghanistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Miaka 100 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa.

Tarehe 9 Mei miaka 211 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Christoph Friedrich von Schillerakiwa na umri wa miaka 46. Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi.

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, alifariki dunia Hujjatul-Islam wal-Muslimin, Dakta Sayyid Jawad Mustafawi, mwandishi na mtafiti wa zama za leo wa Kiirani. Sayyid Jawad alizaliwa mnamo mwaka 1301 katika familia ya kidini na elimu mjini Mash’had nchini hapa. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali na ya kati na kuchukua shahada ya diploma, msomi huyo alijiunga na Hawza ya mjini Mash’had na kusoma kwa maulama wakubwa kama Adiib Nishaburi, Sheikh Hashim Qazwini, Sheikh Mujtaba Qazwini na Sayyidi Ahmad Mudarres Yazdi. Akiwa na umri wa miaka 29, Dakta Sayyid Jawad Mustafawi aliwasili mjini Tehran ambapo mbali na kuhudhuria masomo ya ngazi za juu, akaanza kufundisha na kutokea kuwa alimu mkubwa na mashuhuri wa zama hizi.