Mar 20, 2021 02:32 UTC
  • Jumamosi, 20 Machi, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 6 ya mwezi Shaaban 1442 Hijria mwafaka na tarehe 20 Machi 2021 Miladia.

Tarehe 20 Machi miaka 294 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84. Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. ***

Isaac Newton

 

Miaka 117 iliyopita katika siku kama ya tarehe 6 Shaaban 1325 aliuawa shahidi Allama Ibrahim Khui alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu. Alifanikiwa kupata daraja ya Ijihadi baada ya kusoma kwa miaka mingi kwa walimu mahiri wa zama hizo kama Sheikh Murtadha Ansari. Allama Ibrahim Khui alikuwa na umahiri wa aina yake katika elimu za Kiislamu hususan falsafa. Alimu huyo wa Kiirani alikuwa na harakati na juhudi kubwa katika zama za kupigania utawala wa katiba, kupinga dhulma na kupigania uhuru. Hatimaye katika siku kama ya leo aliuawa shahidi nyumbani kwake na makachero wa Muhammad Ali Shah mmoja wa watawala madikteta wa ukoo wa Qajar***

Allama Ibrahim Khui 

 

Miaka 92 iliyopita katika siku kama ya leo, Mirza Lutf-Ai Nasiri alimu, mwanafasihi na mahiri na mtajika wa Kiirani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 82. Alitambulika kwa lakabu ya Sadru-Afaadhil na alikuwa msomi na mwanazuoni mashuhuri katika karne ya 14. Lutf-Ali Nasiri akiwa pamoja na baba yake na wakati huo akiwa mtoto mdogo alihajiri kutoka Shiraz na kuja katika mji wa Tehran. Awali alisoma misingi ya hati na baadaye akaichagua fani ya fasihi. Baadaye aliingia katika uwanja wa masomo kama ya Usul, fikih, hadithi, tafsiri, mantiki na hisabati. ***

Mirza Lutf-Ai Nasiri

 

Na miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 20 Machi 1956, nchi ya Tunisia iliyoko katika eneo la kaskazini mwa Afrika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ijapokuwa harakati za ukombozi nchini humo zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini kutokea Vita vya Pili vya Dunia na kudhoofika Ufaransa kwenye vita hivyo, kuliandaa mazingira mazuri ya kujikomboa nchi hiyo. Baada ya kujipatia uhuru, Habib Bourguiba aliongoza nchi hiyo, kwa karibu miongo mitatu lakini kwa mabavu na ukandamizaji. Baada ya utawala wa Bourguiba, nchi hiyo ilitawaliwa na Zainul Abidin Ben Ali ambaye aliingia madarakani mwaka 1982. Kiongozi huyo naye alifuata mbinu na mwendo uleule wa Bourguiba wa kuwakandamiza wananchi na kupiga vita Uislamu, suala lililopelekea wananchi wa nchi hiyo kusimama kidete na kumng'oa madarakani mwezi Januari mwaka 2011. ***

Tunisia